Habari za Punde

WAZIRI WA AFYA ZANZIBAR APOKEA VIFAA MBALI MBALI VYA AFYA KUTOKA KWA MFANYA BIASHARA SAID NASSIR NASOR (BOPAR

Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohamed akizungumza na Waandishi wa Habari katika Hafla ya kukabidhi Vifaa mbalimbali  kusaidia wenye maradhi mbalimbali ikiwa pamoja na Korona miongoni mwa Vifaa hivyo ni Vitanda ,Mashuka Sabuni za Kunawa mikono , Viti vya Walemavi na Dawa mbalimbali hapo Wizara ya Afya Zanzibar. 

Na Khadija Khamis –Maelezo Zanzibar    31/03/2020.
Wizara ya Afya Zanzibar imepokea msaada wa  vifaa mbali mbali vya afya  kutoka kwa Mdau wa Maendeleo Said Nassir Nassor Bopar kwa ajili ya kupambana na kujikinga na maambukizi ya Corona.
Akipokea msaada huo Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohamed huko katika Wizara ya Afya Mnazi mmoja amesema vifaa hivyo vitasaidia kutoa huduma mbali mbali za matibabu pamoja na kupambana na ugonjwa wa corona nchini.
Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na vitanda 36, mashuka, sanitizer, friji la kuhifadhia damu, mashuka, mask, mito na kiti cha kubebea wagojwa ambavyo vitasaidia kutoa huduma na kujikinga maambukizi ya corona.
Amesema serikali inahitaji vifaa vingi kutokana na kuwepo kwa wagonjwa ambao wanahitaji kupatiwa matibabu na wananchi kujikinga maambukizi ili yasienee nchini
“Mdau huyu wa maendeleo ameleta vifaa hivi wakati mzuri kwa kuangalia shida iliopo hivi sasa kutokana na kufunguliwa kituo kipya cha kidimni ambacho kinahitaji vifaa mbali mbali kwa wagonjwa waliopata maambukizi ya Corona”, alifahamisha Waziri Hamad.
Aidha Waziri wa Afya amemshukuru Mfanyabiashara huyo kwa msaada huo ambao utasaidia kutoa huduma mbali mbali kwa wagonjwa na kupunguza maambukizi  pamoja kuweza kupambana na kupiga vita ugonjwa wa Corona.
Hata hivyo Waziri huyo amewataka wananchi kuchukua tahadhari za mapema kwa kuepuka mikusanyiko na kufuata maagizo yanayotolewa na serikali ili kujikinga na maambukizi ya Corona. 
“Wananchi wasikae vikundi vikundi wabakie Majumbani mwao na kuwadhibiti  watoto wao  kufanya hivyo kutasaidia kuenea kwa maambukizi ya virusi vya Corona nchini”, alisema Waziri wa Afya .
Ameitahadharisha jamii kuchukua tahadhari ya kukaa umbali wa mita moja na kufuata maadili na masharti ya wataalamu wa afya kufanya hivyo kutasaidia kuepusha ongezeko la maambukizi kwa  kufanya hivyo kutapunguza kusambaa kwa maambukizi hayo.
Alisisitiza kuwa wananchi ambao wana  wagonjwa  katika hospitali kuu ya Mnazi mmoja kupanga utaratibu wa kuwahudumia wagonjwa wao kuingia  watu wawili tu ili kuepusha msongamano mkubwa ambao utahatarisha maisha yao kwa kupata maambukizi mapya ya Corona .
Nae Mdau wa Maendeleo ambae ni Mfanyabiashara Maarufu Said Nassir Nassor  Bopar alisema ametoa msaada huo kwa lengo la kuokoa maisha ya jamii kutokana na hali halisi iliyopo ya mripuko wa maradhi ya corona pamoja  na kujikinga maambukizo hayo. 
Alieleza kuwa ataendelea kuisaidia serikali kila hali inaporuhusu ili kuweza kutoa huduma bora kwa wananchi pia anatarajia kutoa msaada mwengine  katika Hospitali ya Kivunge Wilaya ya Kaskazini A pamoja na Kisiwani Pemba .
“Kila panapotokea tatizo kupenda kuisaidia jamii ili kuepukana na athari ambazo zitaweza kujitokeza tuweze kuzikabili kwa namna moja au nyengine kwa wakati muafaka “alisema Bopar

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.