Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Iddi akiyapongeza Mashirika na Taasisi mbali mbali Nchini kutokana na kuguswa kwao kusaidia mapambano dhidi ya kuenea kwa maambukizo ya Virusi vya
Corona.
Pichana – OMPR – ZNZ.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeendelea
kupokea Michango mbali mbali ya Fedha Taslim jumla ya Shilingi Milioni Arubaini
{70,000,000/-} zilizotolewa na Taasisi tofauti Nchini kwa ajili ya kusaidia
nguvu za Serikali katika Mapambano yake dhidi ya kupiga vita kuenea kwa Virusi
vya Corona Nchini.
Michango hiyo imetolewa na Uongozi wa
Benki ya NMB iliyokabidhi Shilingi Milioni 30,000,000/-, Benki ya Maendeleo
Vijijini {CRDB} Shilingi Milioni 30,000,000/- pamoja na Uongozi wa Bodi ya
Uhaulishaji wa Ardhi Zanzibar Shilingi Milioni 10,000,000/-.
Akipokea Michango hiyo hapo Afisini kwake
Vuga Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Mashirika
na Taasisi zinazotoa huduma kwa Jamii zikiwemo zile za Kifedha zinapaswa
kuendelea kuwahamasisha Wananchi katika kuzingatia njia zinazopaswa kutumiwa
katika mapambano dhidi ya Virusi vya Corona.
Alisema Serikali Kuu kwa upande wake
inajitahidi kutumia nguvu zake kubwa katika juhudi za kutoa elimu ili kuona
ufahamu wa kutambua hatari ya kuyaepuka maradhi yanayosababishwa na Vizuri
hivyo unamfikia kila Mwananchi mahali popote alipo Mijini na Vijijini.
Alisema Mashirika na Taasisi hizo kwa vile
zimekuwa zikitoa huduma kila siku kwa kundi kubwa la Jamii. Hivyo ni vyema wakaitumia fursa hiyo kuendelea
kutioa elimu hata kwa kutumia vipeperushi vitakavyosaidia utoaji wa Elimu ya
kujiepusha na Maradhi hayo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
aliupongeza Uongozi wa Taasisi na Mashirika hayo kwa michango inayoendelea
kutoa na kuwahakikishia kwamba itatumiwa kwa utafutaji wa Vifaa na zana
zitakazosaidia mapambano dhidi ya kudhitibi kuenea kwa Virusi vya Corona.
Alisema Mashirika na Taasisi hizo zimeamua
kutoa michango yao ya hali na mali zikielewa vyema kadhia iliyoipata Jamii na
Dunia ya kuvamiwa na Janga hilo baya la
Kirusi cha Corona.
Balozi Seif aliutanabahisha Umma kwamba ni vizuri kwa
baadhi ya Watu kuacha mzaha kwa vile haustahiki kipindi hichi kizito kutokana
na kidonda kikubwa cha kupotea kwa Maisha ya Watu Zaidi ya Milioni Tatu kwenye
Mataifa mbali mbali Ulimwenguni.
Alikumbusha ni vyema Zanzibar ikarejea
katika Historia yake ya kuwa mfano wa matukio mengi Duniani inayotoa fursa kwa
baadhi ya Mataifa Duniani kufika kujifunza akitolea mfano ufanisi ulipatikana
katika mapambano dhidi ya kuondoa Malaria, Kipindupindu, Ugonjwa wa Ndui na
hatimae hivi sasa juhudi ziongezwe katika kupiga vita kuenea kwa Virusi vya
Corona.
Mapema Meneja wa Benki ya NMB Tawi la
Zanzibar Nd. Abdullah Duchi alisema mchango wa Taasisi yao ya Kifedha tayari umeshaingizwa
kwenye Akaunti Maalum iliyoanzishwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa
ajili ya kusaidia mapambano dhidi ya Virusi vya Corona Nchini.
Alisema Uongozi wa Benki ya NMB umeguswa
na tukio hilo lililoikumba Tanzania na Dunia kwa ujumla ambapo wanapaswa
kuingiza nguvu zake katika kuona mapambano hayo yanafanikiwa vyema.
Nd. Abdullah aliziomba Taasisi na
Mashirika mengine kujitokeza kuchangia nguvu zao kwa kushirikiana na Serikali
Kuu ili kuondosha kabisa janga hilo linalomgusa kila Mwananchi hapa Nchini.
Naye Afisa Biashara Mkuu wa Benki ya CRDB
Tanzania Dr. Joseph Vicent Taasisi hiyo ya kifedha Nchini imejitolea kushiriki
kwenye Mapambano dhidi ya Virusi hivyo tokea kuibuka kwake kwa mara ya kwanza
Nchini Tanzania huko Mkoani Kilimanjaro.
Dr. Joseph alimueleza Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar kwamba Uongozi wa Taasisi hiyo umedhamiria kusaidiana na
Serikali zote mbili katika kuona ustawi wa Wananchi wote ambao ndio Mtaji mkubwa
wa kazi zao kwa kuongeza Mapato unaendelea kuimarika vyema.
Kwa upande wake Makamo Mwenyekiti wa Bodi
ua Uhaulishaji wa Ardhi Zanzibar Bwana
Enzi Talib Aboud alisema Uongozi wa Bodi hiyo umeguswa na janga hilo pamoja na kufanya
vyema katika majukumu yake ya kila siku ya ushughulikiaji na ufuatiliaji wa masuala
ya Ardhi lakini umelazimika kushirikiana na Taasisi nyengine Nchini katika
kuungana na Serikali kwenye mapambano hayo.
Bwana Enzi alisema mapambano dhidi ya
Virusi vya Corona {COVIC – 19} yanapaswa kushirikisha kila Taasisi, Mashirika ya
Umma, yale ya Kimataifa na hata Jamii ili kuiona Zanzibar na Tanzania kwa
ujumla inabakia salama.
Alisema Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania
ikijumuisha Bara na Zanzibar bado inaendelea kuwa na unafuu wa kukumbwa na
janga hilo la Virusi vya Corona ikilinganishwa na Mataifa mengine Duniani
yakiwemo pia hata yake jirani ya Afrika Mashariki.
No comments:
Post a Comment