Habari za Punde

Wawakilishi CCM wachangia Mil 50 kusaidia vita dhidi ya Virusi vya Corona nchini

 Kamati ya Uongozi wa Baraza la Wawakilishi ya CCM ikimkabidhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mchango wa Shilingi Milioni 50,000,000/- kwa ajili ya kusaidia vita dhidi ya mapambano ya kukabiliana na Virusi vya Corona Nchini. Kati kati ni Spika wa Baraza la Wawakilishi Mh.Zubeir Ali Maulid, Mnadhimu wa Baraza hilo Mh. Ali Salul Haji, Mwakilishi Viti Maalum Kusini Unguja Mh. Salma Mussa Bilal na Mwakilioshi wa Jimbo la Kikwajuni Mh. Salum Jazira.
 Spika wa Baraza la Wawakilishi Mh. Zubeir Ali Malid aitoa ufafanuzi juu ya uamuzi wa Kamati ya Uongozi ya Baraza la Wawakilishi kupitia CCM ilivyoamua kumega fedha kwa ajili ya kusaidia mapambano dhidi ya Corona
  Mnadhimu wa Baraza la Wawakilishi ambae pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Kwahani Mh. Ali Salum Haji akitoa maelezo ya fedha walizokwishaingiza katika Akauti ya Mchango wa Corona.
.
Wa kwanza kutoka Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Abdullah Hassan Mitawi, Mkurugenzi Uratibu, Nd. Khalid Bakari Amran, Naibu Katibu wa Makamu wa Pili Bibi Sharifa abeid na Afisa Uhusiano Ofisi ya Makamu wa Pili Nd. Famau Lali Mfamau.

Picha na OMPR

Na Othman Khamis , OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewaomba Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutumia nguvu zao za ziada katika kutoa Elimu kwa Wananchi juu ya mapambano dhidi ya Virusi vya Corona vinavyoendelea kuitikisha Dunia. 
Alisema ipo ishara na dalili kubwa zilizo wazi zinazoonyesha kwamba Wananchi walio wengi hasa wale wa Vijijini bado hawajafikiwa na Elimu ya mapambano dhidi ya Corona jambo ambalo ni hatari kwa Afya na maisha yao ya kila siku.
Balozi Seif alitoa ombi hilo hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanziar wakati akipokea Mchango wa Shilingi Milioni 50,000,000/- uliotolewa na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa Chama cha Mapinduzi, fedha zilizotoka ndani ya Mfuko wao ulioanzishwa kuhudumia harakati za Chama.
Hata hivyo Balozi Seif alishauri kwamba Elimu ya kupambana na Virusi hivyo ni vyema ikaendelezwa hata itakapofikia hatua ya kumalizika kwa mapambano ya Virusi hivyo ili kuijengea mazingira ya uhakika ya Afya Jamii yote Nchini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwashukuru na kuwapongeza Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa CCM kupitia Kamati yao ya Uongozi kwa wazo lao la kufikiria kuungana na Serikali Kuu katika kuchangia nguvu kwenye mapambano hayo.
“ Uamuzi wa Kamati ya Uongozi ya Baraza la Wawakilishi  ni wa busara kwa vile umezingatia Zaidi Afya za Wananchi wa Taifa hili”. Alisema Balozi Seif.
Aliendelea kuwakumbusha Wananchi wote kuzingatia Taarifa na Elimu inayotolewa na Wataalamu wa Afya juu ya kupiga vita virusi vya Corona vyenye kuonyesha dalili ya kubadilika mfumo wa mashambulizi dhidi ya Mwanaadamu.
Alisema tafiti za Wataalamu zinazidi kuonyesha kwamba Virusi vya Corona vina uwezo wa kushambulia moja kwa moja mapafu bila ya kuonyesha zile dalili zilizozoeleka zinazompa ishara Mtu anapoanza kubaini maumivu.
Akikabidhi Mchango huo wa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa Chama cha Mapinduzi  wa shilingi Milioni Hamsini Mnadhimu wa Baraza hilo Mh. Ali Salum Haji kwa niaba ya Wajumbe wake amezipongeza Serikali zote mbili Tanzania kwa jitihada zinazoendelea kuchukuwa za mapambano dhidi ya Corona.
Mh. Ali alisema Jitihada hizo ndizo zilizowapa hamasa za kuamua kuungana na Serikai katika kuchangia nguvu za mapambano hayo yanayohitaji ushirikiano wa pamoja na ngazi zote.
Mapema Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mheshimiwa Zubeir Ali Maulidi alisema Kamati ya Uongozi wa Wajumbe wa Baraza hilo ya Chama cha Mapinduzi ililazimika kutumia fedha za Mfuko huo ili kusaidiana na Serikali katika Vita hivyo vikubwa.
Mh.Zubeir alisema yapo matumaini makubwa ya jitihada zinazochukuliwa na kila Taasisi na Sekta katika kusaidia mapambano dhidi ya Virusi vya Corona vinavyosababisha Homa kali, kikohozi pamoja na matatizo ya mapafu.No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.