Habari za Punde

Wananchi wa Mkoa wa Kusini Watakiwa Kutoa Ushirikiano na Jeshi la ;Polisi Kutoa Taarifa za Wahalifu.

NA MWAJUMA JUMA
WANANCHI wa Mkoa wa Kusini Unguja wamesema kuwa kushindwa kukamatwa.kwa watuhumiwa wa makosa ya mauaji ndani ya Mkoa huo sio Kama  kunachangiwa na wao kutotoa ushirikiano kwa Polisi.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi walisema kuwa sio kweli kuwa wanakataa kutoa ushirikiano isipokuwa Jeshi lenyewe ndio linakuwa kikwazo.

Walisema kuwa wakati mwengine wanakuwa wanawaita Polisi kumetokea uhalifu lakini mwisho wa siku wanatokea muda ambao tayari wahalifu washaondoka.

"Mbona likitokea tukio la mzungu kuibiwa wanakuja na kufatilia kwa sababu wanaona Kuna pesa wasiseme Kama hatutoi ushirikiano sio kweli wao ndio wanashirikiana na wahalifu", alisema mmoja wa wananchi ambae jina lake limehifandhiwa.

Hivyo alilishauri Jeshi la Polisi kujipanga upya kwani hakuna mwananchi hata mmoja ambae anataka katika mtaa wake kuwepo na uhalifu.

Wananchi hao waliyasema hayo kufatia Jeshi  la Polisi Mkoani humo  kuendelea kulalamika juu ya kukosa mashirikisho kutoka kwa wananchi katika upatikanaji na kuwakamata wahalifu hasa wa mauaji.

Kamanda wa Polisi Mkoani humo Suleiman Hassan Suleiman  akizungumza na mwandishi wa habari hizi huko ofisini kwake Tunguu alisema kuwa mnamo Febuari 26 mwaka huu, huko Peje kulitokea tukio la mauaji kwa kijana kumuuwa mpenzi wake lakini mpaka Sasa muuaji huyo hajapatikana .

Tukio hilo la mauaji lilihusisha wivu wa mapenzi ambapo kijana Haji Haja Issa alimuuwa mpenzi wake Hajra Abdalla Abdalla kwa kumchoma kwa kitu chenye ncha Kali na kumsababishia kifo.

Alisema kuwa baada ya kufanya tukio hilo mtuhumiwa huyo alikimbia na Jeshi la Polisi linaendelea kumtafuta.

Hata hivyo kwa mujibu wa uchunguzi umebaini kuwa mtuhumiwa huyo  amekuwa akionekana mtaani hapo lakini watu wameshindwa kumfikisha Polisi mtuhumiwa huyo.

Alieleza kuwa tukio hilo linafanana na lile la mauaji yaliyotokea Ndagaa la kuuliwa kwa mwanamke ambae aliuliwa mchana kweupe lakini wananchi walishindwa kutoa ushirikiano kwa Polisi.

Hata hivyo alisema pamoja na hilo alisema kuwa wanaendelea na jitihada za kumtafuta muhalifu wa tukio la mauaji la Hajra Abdalla Abdalla ili aweze kuchukuliwa hatua.

Katika hatua nyengine amesema kuwa mtuhumiwa wa kosa la mauaji ya Anna Joseph Msema (25) mkaazi Mwera Pongwe Sammuel Matius Chilalu (26), mkaazi wa Mwera Pongwe alifariki nae katika.hospitali ya mnazimmoja alipofikishwa kupatiwa matibabu.

Mtuhumiwa huyo ambae ni familia moja na Anna ambao ni watoto wa mjomba kwa shangazi alifanya kosa hilo Machi 11 mwaka huu huko Mwera Pongwe saa 5:00 usiku kwa kumpiga rungu na kumkata kwa panga na kimsababishia kifo.

Chanzo Cha tukio hilo kunadaiwa ni wivu wa mapenzi ambapo baada ya kufanya hivyo na yeye alidaiwa kunywa sumu ya kuulia magugu na kukimbia.

Kamanda Hassan alisema kuwa baada ya kutokea tukoo hilo msako ulianza na kumkamata na kumkuta yupo katika hali mbaya na kumpeleka hospitali kwa matibabu ambapo usiku wa.saa mbili alifariki.

Hata hivyo alisema kuwa matukio ya udhalilishaji wa jinsia kwa wanawake na watoto yamepunguwa kwa kiasi kikubwa katika Mkoa wake na yaliyojitokeza na mauaji ya wivu wa mapenzi.

Hivyo aliwashauri vijana ambao watakutwa na matatizo katika mahusiano yao wajaribu kukaa na watu wazima ili waweze kufikia muafaka badala ya kuchukuwa hatua mikononi mwao.

Alisema kuwa kitendo cha kutopeleka kesi kwa familia zao kunapelekea muhusika kuwa na msongo mkubwa wa mawazo na baadae kujikuta anafanya maamuzi ya kuuwa.


Tangu kuanza kwa mwaka huu matukio mawili ya mauaji yamejitokeza ambapo moja mtuhumiwa wake hajapatikana na moja mtuhumiwa wake alifariki kwa kujiuwa pia.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.