Habari za Punde

Balozi Seif Aendelea na Ziara Yake Mkoani Shinyanga leo.

Mlezi wa Mkoa wa Shinyanga Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Wajumbe wa Halmashauri ya CCM Wilaya ya Kishapu akikamilisha ziara yake ya siku Tatu Mkoani Shinyanga.
Baadhi ya Wajumbe wa Halmashauri ya CCM Wilaya ya Kishapu wakimsikiliza Mlezi wao Balozi Seif Ali Iddi  hayupo pichani alipozungumza nao hapo Kishapu Mkoani Shinyanga.
Mbunge wa Jimbo la Kishapu Suleiman Masoud Nchambi akielezea mafanikio makubwa yaliyopatikana ndani ya Jimbo la Kishapu, Mkoa wa Shinyanga na Taifa kwa ujumla kutokana na jitihada kubwa za Serikali.
Balozi Seif na Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi wakipokea zawadi mbali mbali ikiwemo Nafaka na Mifugo kutoka  kwa Wanashinyanga  ikiwa Heshima kutokana na uLezi wao ndani ya Mkoa huo mwa Miaka Mitano.
Kikundi cha Utamaduni cha Majembe  Mwangano cha Wilaya ya Kishapu kilichopata fursa ya kutoa Burdani katika Mkutano wa Mlezi wa Mkoa wa Shinyanga Balozi Seif Ali Iddi alipozungumza na Wajumbe wa Halmashauri ya CCM Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema ushirikiano wa pamoja  wa Wabunge wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania wa Majimbo yaliyomo ndani ya Mkoa wa Shinyanga chini ya usimamizi wa Serikali umesaidia kupaisha kwa kasi kubwa Mkoa huo Kimaendeleo ndani ya kipindi kifupi.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akizungumza na Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Kishapu akimalizia ziara yake ya Siku Tatu Mkoani Shinyanga akiwa Mlezi wa Mkoa huo kuangalia umaliziaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2015-2020 ndani ya Mkoa huo.
Alisema Waheshimiwa Wabunge wa Majimbo hayo wakiwa Watumishi wa Wananchi walionyesha ukomavu mkubwa uliopelekea  kuhamasishana katika kuona changamoto zinazowakabili Wananchi katika Majimbo yao zinapata ufumbuzi wa kudumu.
Hata hivyo Balozi Seif akiwa pia Mjumbe wa Kamati Kuu ya Hamashauri Kuu ya Taifa ya CCM alionyesha kuchukizwa kwake na tabia ya baadhi ya Wabunge wa Majimbo kuwachukia wenzao wa Viti Maalum wa Mikoa pale wanaposhiriki katika kuunga mkono Wananchi kwenye Miradi yao ya Maendeleo.
“ Wale Wabunge wa Majimbo na Viti Maalum ni vyema wakaendeleza Utamaduni wa kufanya kazi kwa pamoja ili kubeba dhima ya kuendelea kuwatumikia Wananchi kwa maslahi ya Taifa ”. Alisema Mlezi huyo wa Mkoa wa Shinyanga.
Hata hivyo Balozi Seif alisisitiza kwamba itapendeza na kufurahisha pale Mbunge wa Viti Maalum ambae yeye ni Mtumishi wa Wananchi wa Majimbo ya Mkoa mzina napoamua kupeleka maendeleo ni vizuri kumuarifu Mbunge Muhusika wa Jimbo ili kazi zao ziwe na maingikliano ya pamoja.
Akizungumzia muelekeo wa Taifa katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Mwezi Oktoba Mwaka huu Balozi Seif aliwakumbusha Wananchi wa Mkoa wa Shinyanga kuelewa kwamba wao ndio waamuzi wa kumchagua Kiongozi atakayepaswa kuwaongoza ndani ya Miaka Mitano ijayo.
Alisema kazi iko ndani ya mikono yao ya kutafakari wale waliowaongoza kipindi kinachomalizika kama watafaa kuendelea au kutafuta wengine wapya lakini cha kuzingatia kuepuka kosa linaloweza kufanywa katika mchakato huo wa Uchaguzi linaweza kuendelea kuwatesa kwa kipindi chote cha Miaka Mitano.
Akigusia Uchaguzi wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Balozi Seif alisema Dr. John Pombe Magufuli ameshaonyesha wazi moyo wake wa kukubali kuendelea kuwatumikia Watanzania Bara na Zanzibar katika kipindi chengine kijacho.
Aliwaagiza Viongozi wa ngazi zote ndani ya Mkoa wa Shinyanga kusimamia ipasavyo kampeni za kistaarabu zitakazomuwezesha Dr. Magufuli kwenye uchguzi ujao kuibuka kwa asilimia 100% ya kura zote ikilinganishwa na asilimia 68% ya Kura alizozipata kwenye uchaguzi wa Mwaka 2015.
Balozi Seif alibainisha wazi kwamba Zanzibar na Tanzania kwa ujumla lazima ziongozwe na Mzalendo anayekubali kujitolea  kwa moyo wake kuwatumikia Wananchi katika misingi ya amani na upendo.
Alifahamisha kwamba hayo yote yatafanyika na kukamilika katika mfumo wa Demokrasia endapo kila Mwananchi atazingatia umuhimu wa kusimamia pamoja na kudumisha Amani na Utulivu uliopo Nchini ukibakia kuwa kielelezo cha Tanzania kusifika kuwa Kisiwa cha Amani Duniani.
Alisema Watanzania ni vyema wakakumbuka kwamba Mtu au Kikundi chochote kitakachotishia Amani ya Taifa lazima waelewe kuwa Mtu au Kikundi hicho ni adui wa Taifa.
Wakielezea Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2015 – 2020 Wabunge wa  Majimbo yaliyomo ndani ya Mkoa wa Shinyanga pamoja na wale wa Viti Maalum wamempongeza na kumshukuru Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli kwa kasi kubwa anayoisimamia katika kuimarisha Uchumi wa Taifa.
Wabunge hao walisema kasi hiyo inayokwenda sambamba na Utekelezaji mzuri wa Ilani ya Uchaguzi  katika kipindi cha Miaka Mitano inayomalizika hivi sasa imekuwa ushahidi wa wazi wa rekodi aliyoweka ya Kuifanya Tanzania kupaisha Uchumi wake.
Walisema jitihada za Rais zimewarahsishia na wao kwa upande wa Majimbo kuiga mfano huo na hatimae changamoto kadhaa zilizokuwa zikiwasumbuwa Wananchi zimepatiwa ufumbuzi na zitabakia kuwa Historia kwa Miaka mingi ijayo.
Wakitoa shukrani zao Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Shinyanga wamemsifu Mlezi wao kwa hekina, busara na ushauri aliokuwa akiwapatia Viongozi na Wananchi wa Mkoa huo wakati wote wa Ulezi wake ndani ya Miaka Mitano.
Walisema Balozi Seif na Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi walikuwa walezi bora walioshiba upendo na kufananishwa na Mto unaotiririsha Maji yake yanayosambaa na kunufaisha Wananchi wa Mkoa wa Shinyanga.
Viongozi hao kupitia Mkutano huo wamemuomba Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kufikiria namna itakavyowezesha Mlezi huyo ambae licha ya kukaribia kumaliza jukumu lake lakini ajengewe mazingira ya kuendelea kuwatumikia Wananchi wa Mkoa huo hapo baadae.
Mlezi huyo wa Mkoa wa Shinyanga pamoja na mambo mengine alipata wasaa wa kukagua maendeleo ya Mradi wa Ujenzi wa Jengo Jipya la Ofisi ya CCM Wilaya ya Kishapu jengo ambalo tayari ameshajumuisha nguvu zake katika ziara zake zilizopita nyuma na kuridhika na hatua iliyofikiwa hivi sasa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.