Habari za Punde

KATIBU MKUU VIWANDA ATAKA UJENZI WA KIWANDA KIPYA CHA VIATU CHA KARANGA KUKAMILIKA KWA WAKATI


Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Prof. Riziki Shemdoe (wa pili kulia) akizungumza na Mhandisi Mkuu wa ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza bidhaa za ngozi cha Karanga  Mhandisi Emmanuel Mwangalaba (SP) alipotembelea kiwandani hapo kuangalia Maendeleo ya ujenzi. 


Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Prof. Riziki Shemdoe akikagua ujenzi unaondelea katika kiwanda cha kuzalisha bidhaa za ngozi Karanga Mkoa wa Kilimanjaro


Baadhi ya vifaa vinavyosubiri kufungwa katika kiwanda cha Karanga.



Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Prof. Riziki Shemdoe ameitaka kampuni ya Tanelec - Arusha kuharakisha utengenezaji wa vifaa  vya umeme ikiwemo  (switch gears ) ambazo zinasubiriwa kufungwa kwenye kiwanda cha kuzalisha bidhaa za ngozi  cha Karanga kilichopo Mkoani Kilimanjaro.

Prof. Shmdoe aliyasema hayo alipofanya ziara kwenye kiwanda cha Karanga ambacho kinajengwa na Shirika la Uzalishaji la Magereza. Lengo la ziara hiyo ni kuangalia maendeleo ya ujenzi wa kiwanda hicho kipya ambacho kinajengwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi Bilioni tisa.

Katika ziara hiyo Prof.Shemdoe alikagua ujenzi ambao kwa sehemu kubwa umekamilika na kinachosubiriwa ni ufungaji wa (switch gears) ambazo zinatengenezwa na Kampuni ya TANELEC ya Mkoani Arusha.

Prof. Shemode alisisitiza kazi hiyo ifanyike kwa haraka ili wataalamu wa kufunga vifaa hivyo watakapofika wasiwe na sababu ya  kushindwa kujaribu mitambo kwa ajili ya kukosa umeme.



”Ombi langu kwa Tanelec  mhakikishe mnatengeneza kwa wakati  vifaa vya umeme ili vifungwe na kufanyiwa majaribio ili wataalam wa kufunga mashine wakija kusiwe na kikwazo”.

Aidha aliwasihi wasimamizi wa ujenzi  kuhakikisha wanamalizia kazi zilizobakia kwa haraka kwenye ujenzi wa majengo ya awamu ya kwanza.

"Nategema baada ya kukamilika kwa majengo haya uzalishaji utaongezeka mara dufu".

Kwa upande wake msimamizi wa ujenzi huo Mhandisi Mwangalamba (SP)  alimueleza Katibu Mkuu kuwa ujenzi huo ungekuwa umekamilika ila changamoto yao ni utengenezaji wa vifaa  vya umeme kutoka Kampuni ya Tanelec kuchukua muda mrefu hivyo baadhi ya vifaa haviwezi kufungwa mpaka hapo (switch gears)  zitakapofungwa.

Ujenzi wa majengo ya kiwanda  cha Karanga unatekelezwa  na shirika la Uzalishaji la Magereza tangu Juni, 2019 na unatarajiwa kukamilika mwaka huu.


Kiwanda Cha Karanga kitakapokamilika kinatarajia kutoa ajira 5000 za moja kwa moja na zisizokuwa rasmi 4000 kutokana na shughuli mbalimbali katika eneo hilo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.