Habari za Punde

Taa za Solar kuondoa kero kijiji cha Makadara shehia ya Mbuyuni, Mkoani kisiwani Pemba

 MAFUNDI kutoka kampuni ya Salim Constraction LtD, wakifunga taa za mkono mmoja zinazotumia nishati ya umeme wa jua, katika barabara kuu ya kuelekea shehia ya Mbuyuni Wilaya ya Mkoani.(PICHA NA ABDI SULEIMAN)
MAFUNDI kutoka kampuni ya Salim Constraction LtD, wakifunga taa za mkono mmkoja zinazotumia nishati ya umeme wa jua, katika barabara kuu ya kuelekea shehia ya Mbuyuni Wilaya ya Mkoani.(PICHA NA ABDI SULEIMAN)
MOJA ya Taa zinazotumia nishati ya umeme wa jua, ikiwa katika njia ya kuingilia ndani ya kijiji cha Makadara, taa hizo zimeweza kuwakimbiza wapiga chabo usiku pale zinapowaka..(PICHA NA ABDI SULEIMAN)
NA ABDI SULEIMAN.
KABLA ya Januari mwaka huu, ilikuwa ni shida kupita katika barabara ya kuingia  Kijiji cha Makadara muda wa usiku unapofika...hofu ya kunyanganywa pesa vijana na watoto ilikuwa ikiwaumiza kichwa wazazi wengi.
Khamis Juma Kombo anasema baada ya kufungwa kwa taa za mkono mmoja za nishati ya jua, zimebadilisha maisha ya kijiji hicho  katika maeno ya barabarani.
Kuwekwa kwa taa za umeme jua zimeweza kuwakimbiza kundi la vijana, waliokuwa wameziweka roho za wakaazi wakijiji hicho juu. 
Licha ya baadhi ya nyumba nyingi za kijiji hicho kuunganishwa na huduma ya umeme wa Gridi, ndoto zaidi ziliweza kutimia baada ya Taa za umeme wa jua kuanza kungara katika barabara ya kuingia kijiji hapo.
Ni umbali wa dakika tatu kutoka Ofisi za Baraza la Mji Mkoani, kufika katika eneo ambalo  vijana wanaokaba na kunyanganya fedha na kuwadhalilisha watoto, eneo ambalo sasa hili limewekewa taa na kuwafanya vijana hao kukimbia.
Jua hilo linazama, sasa hivi kijiji kitakuwa kama asubuhi, hizi taa ni moja ya lulu ambayo tukiihitaji sasa imeanza kung’aa na tumeipokea kwa nia njema,” Awena Khamis  alimwambia mwandishi wa habari hizi.
Awena anasena hakuna hata mananchi mmoja aliyefikiria, ipo siku Makadara itaweza kungaa kama ilivyo sasa, muda wote unaweza kuwatuma watoto dukani, hata katika ngazi za kuteremkia skuli ya ng’ombeni sasa hazitishi tena kwa wanafunzi.
Ili ufike kijiji cha Makadara chenye wakaazi 464  wanawake wakiwa 245 katika shehia ya Mbuyuni,  unapaswa kusafiri umbali wa kilomita 29, kutoka Wilaya Chake Chake, jambo ambalo linahitaji ujasiri na mipango ya ahali ya juu.
Vijiji vyengine vinavyozunguka kijiji hicho ni Mbuyuni chenye wakaazi 739, Mjini Mkoani (699) na Kikwajuni Bondeni chenye wakaazi (298.)
HATUKUWAHI KUFIKIRIA KAMA TUTAKUWA NA TAA HIZI ZA KISASA
Juma Khamis Ali (38) anasema taa za umeme wa jua zimesaidia usalama wa watoto wao, mali, majumbani mwao, hata wapiga bodi (Chabo) wameweza kukimbia kufuatia uwepo wa taa hizo.
 “Sasa unaweza kuacha nguo zako nje usiku wala haziibiwi, hizi taa zimekuwa ni mlinzi katika kijiji chetu, wapiga bodi walikuwa wengi, mtu halali kwa raha usiku na wasiwasi wa kuchunguliwa (Chabo), sasa kuwepo kwa taa wapiga bodi wamekimbia kabisa,”amesema Khamis.
Amesema watoto sasa unaweza kuwatuma muda wowote bila ya hofu, tofauti na hapo zamani kabla ya uwepo wa taa hizo, japo kuwa zinamuwangaza mkali sana.
Taa hizi zimeongeza usalama majumbani, zimesaidia kwa kiasi kupunguza vitendo vya unyanganyaji wa  fedha na unyanyasji wa watoto usiku wanaokwenda madukani,  pamoja na kukimbiza kundi la vijana wahuni njiani.
Asha Othama Kassim (27) amesema ilikuwa mtoto usiku kutoka njie ni mtihani, sasa hivi wanakwenda mpaka dukani wala hakuna vuna vijana wakorofi, hizi taa zimesaidia sana hapa kijijini petu.
“Ilikuwa hata kuwatuma watoto dukani basi mtu anaogopa, anapokonywa fedha au hata kubakwa, sasa taa zimesaidia ukitembea mwangaza unamurika sana na watoto wanacheza bila hofu,,” alisema Asha.
Omar Yakub Ali (38) amesema taa ni usalama katika kijiji Makadara, sababu kilikuwa kiza sana, sasa wameepukana na matatizo mengi watoto wetu kukabwa.
Kwa mujibu wa Taarifa ya utekelezaji wa mradi (ZUSP), imesema mradi huo ambao unatekelezwa kwa Wilaya ya Mkoani utakuwa na taa 50 za mikono miwili na taa 100 za mkono mmoja.
Wilaya ya Chake Chake yenyewe itakuwa na taa 164 za mikono miwili na taa 51 za mkono mmoja, Wilaya ya Wete taa 115 za mikono miwili na taa 104 za mkono mmoja, huku mradi ukiwa na gharama ya Bilioni 6.3 ikiwa ni mkopo kutoka Benki ya Dunia.
VIJANA NAO HAWAKUWA NYUMA
Kombo Omar Othman (19) anasema vijana nao wamenufaika na taa hizo, kwa kuongeza usalama wao wakati wa kwenda katika masomo ya ziada muda wa Magharibi hadi saa mbili usiku.
anasema Kombo huku akionyesha namna ngazi hizo zilivyokuwa zikitisha usiku kabla ya taa hizo.Taa hizo zimeongeza usalama kwa watoto wa shule na sasa wanawahi kwenda shule kwa kuwa hawahofii tena usalama wao kama hapo awali kabla ya kuwekwa taa hizo.
“Hapa katika hizi ngazi tulikuwa tukiogopa hata kupita, vijana wahuni wakikikaa na kutusubiri turudi watuhangaishe kwa kututisha , kwa kweli ilikuwa ni mtihani mkubwa kwetu wakati mwengine huwaita wazazi wetu,”amesema
Kulthum Khamis Mussa (22),  anasema sasa huwezi kusikia mtoto au mwanafunzi amepokonywa vitu vyake, tulikuwa wazazi katika hali mbali kwa vijana wetu wakati mwengine tukawafuate vyuoni huko.
             WAFANYA BISHARA SASA NI HADI USIKU
Uwepo wa taa hizo siyo tu zimeongeza usalama bali ni nuru pia kwa wafanyabiashara wameanza kuona ongezeko la faida kutokana na kufanya biashara zao hadi usiku,” Khalid nasema.
Khalid Omar Juma anasema taa hizo muda wa usiku zimewasaidia sana, mapato yameanza kuongezeka kulingana na biashara ya mtu menyewe.
“Kwa sasa mambo mazuri usiku wateja wanapatikana mmoja mmoja, zamani ukijuta kufanya bishara usiku sasa hivi, natarajia kuongeza hata bidhaa za watoto hapa gengeni pangu,”alisema Khalid.
Yussuf Shaame Haji amesema hizi taa zimewaondoshea hata gharama za ununuzi wa mafuta ya taa, kuingiza katika taa za kandili kwa siku tatu hutumia lita moja ya mafuta shilingi 1162 kuanzia saa 12 jioni hadi saa mbili usiku.
“Sasa kutumia mafuta ya taa niameanza kusahau, mauzo pia yameanza kuongezeka kutoka shilingi elfu 40,000 au 60,000 kabla ya umeme, sasa nafikia 80,000 hadi 100,000 baada ya kuwepo umeme,”alisema Yussuf.
KWA UPANDE WAO VIONGOZI WA SERIKALI
Uongozi wa shehia ya Mbuyuni umesema uwekezaji wa taa za barabarani za umeme jua katika kijiji cha Makadara,  umekifanya kijiji hicho kuonekana kimekuwa shehia ya mjini kama ilivyo maeneo ya mji wa Chake Chake muda wa usiku unapofika.
Sheha wa shehia ya Mbuyuni Nassor Juma Kombo amesema shehi inawananchi 1, 902 wakiwemo wanawake 1,000, kwa sasa tokea kuanza kuwaka taa hizo matukio maovi yametoweka katika kijiji cha Makadara.
Mkurugenzi wa Baraza mji Mkoani Rashid Abdalla Rashid amesema uwekaji wa taa hizo katika maeneo ya mkoani ni utekelezaji wa malengo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwaletea wananchi wake maendeleo katika maeneo wanayoishi.
Kwa sasa mikakati ya baraza la Mji ni kuhakikisha huduma hiyo inafika katika vijiji vyote kama ilivyokuwa katika kijiji cha Makadara kwa kutumia fedha za makusanyo ya baraza, tayari baadhi ya maeneo yamesha ainishwa.
“Mradi wa taa umeelezwa bayana katika ilani ya uchaguzi ya mwaka 2015/2020 na sio jambo lakukurupuka,” alisema. 
Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015-2020, ibara ya 95 imeeleza kuwa sekta ya nishati, hususan umeme ni nyenzo muhimu katika kukuza uchumi na maendeleo ya jamii, pamoja na kurahisisha shughuli nyingi za kiuchumi, kuongeza kasi ya uzalishaji na kuwawezesha wananchi kujiajiri wenyewe.
Ibara hiyo ya 95 (e) imesema vyanzo vya nishati mbadala ya umeme ukiwemo umeme wa jua, mawimbi ya bahari, upepo na gesi asilia vimefanyiwa uhakiki.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Pemba Ahmed Khamis Mkaran, amesema kwa sasa wananchi wa kijiji cha makadara wanaishi kwa amani, kwani taa zimesaidia sana kukimbizi vijana waliokuwa wakifanya matukio hayo.
“Kwa sasa muda mrefu sijasikia kitu katika taarifa za kesi zinazofika ofisini kwangu kwa siku, uwepo wa taa hizi zimesaidia kwa kiasi kikubwa kutokomeza matukio na wananchi wanaishi kwa amani,” amesema kamanda Makaran
Kwa Upande wa Hotuba ya Waziri wa Ardhi, Maji, Nishari na Mazingira Zanzibar, Salama Aboud Talib iliyowasilishwa katika baraza la wawakilishi 2017/2018 imesema bado serikali inaendelea na azma yake katika kukamilisha mradi wa utafiti wa nishati mbadala, ili kujua uwezekano wa Zanzibar kupata umeme kwa njia mbadala.
Hutuba hiyo imesema kuwa takwimu za kuangalia mwenendo wa upepo na upatikanaji wa jua, zinazendelea kukusanywa tokea mwezi Agosti 2015 hadi 2018, ambapo takwimu zinaashiria uwezekano mzuri wa matumizi ya nshati mbadala kwa zanzibar.
Kwa mujibu wa sera ya Nishati ya Zanzibar ya Disemba 8 mwaka 2009, iliyotayarishwa na Wizara ya Maji, Ujenzi, Nishati na Arhdi, imesema lengo kuu ni kukidhi mahitaji ya nishati ya idadi ya watu wa Zanzibar kwa maendeleo ya kijamii na kiuchimi katika mazingira endelevu.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.