Habari za Punde

Balozi Seif azindua tamasha la Utamaduni wa Mzanzibari

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwapungia mikono Wananchi waliohudhuria kwenye uzinduzi wa Tamasha la Utamaduni wa Mzanzibar hapo Mnara wa Kumbukumbu ya Mapinduzi Michenzani.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akipiga Ngoma kuashiria kulizindua rasmi Tamasha ya 25 la Utamaduni wa Mzanzibari hapo Mnara wa kumbukumbu ya Mapinduzi Kisonge.
 Balozi Seif akifanya mzaha na mmoja wa Wasanii na Wanautamaduni wa Vikundi vya wajasiri amali walioshiriki maonyesho ya Tamasha la Utamaduni wa Mzanzibari hapo Michenzani
 Balozi Seif Ali Iddi akiangalia kazi za Wasanii wa fani ya ufinyanzi wa vyungu kwenye Maonyesho Maalum ya uzinduzi wa Tamasha la Utamaduni la Mzanzibari.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiangalia na kufurahia kazi za Wajasiri amali wa vipodozi pamoja na dawa za asili kwenye amaonyesho ya Tamasha la Utamaduni wa Mzanzibar.
 Wasanii wa Kikosi cha Mafunzo Zanzibar wakitoa burdani safi ya Ngoma ya Tukulanga kwenye hafla ya uzinduzi wa Tamasha la Utamaduni wa Mzanzibar Zanzibar hapo Kisonge Michenzani Mjini Zanzibar.
  Umma wa Wananchi waliohudhuria uzinduzi wa Tamasha la Utamaduni wa Mzanzibari wakifuatilia matukio mbali mbali yaliyojiri katika uwanja wa kumbukumbu ya Mapinduzi Michenzani.
 Waziri wa Vijana,Utamaduni, Sanaa na Michezo Balozi Ali Abeid Karume akijiandaa kumkaribisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kulizindua Tamasha la Utamaduni la Mzanzibari hapo Mnara wa kumbukumbu ya Mapinduzi Kisonge.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimkabidhi tuzo Maalum Msanii Maarufu Nchini ambae pia ni Mshauri wa Rais wa masuala ya Utamaduni Bwana Chimbeni Kheir kwenye uzinduzi wa Tamasha la Utamaduni la Mzanzibari.
 Kikosi cha wana habari wakichukuwa matukio mbali mbali yaliyokuwa yakifanyika kwenye uzinduzi wa Tamasha la Utamaduni la Mzanzibari hapo Mnara wa kumbukumbu ya Mapinduzi Kisonge
Balozi Seif akimkabidhi Tuzo Maalum Mama mzazi wa Msanii maarufu nchini wa maigizxo na Vichekesho Marehemu Khamis Haji Maarufu Halikuniki Mbuzi ngumu aliyefariuki dunia miaka michache iliyopita.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Wananchi wanapaswa kuzitumia fursa zinazopatikana kupitia Utamaduni wao kama nyenzo muhimu ya Biashara, Ajira na Uchumi wakiendelea kulinda Mila na Ahlaki njema zinazotokana na Utamaduni huo.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kulinda na kuendeleza misingi na maelekezo ya kiutekelezaji yanayotokana na miongozo mbali mbali katika kuhakikisha Utamaduni wa Taifa unaenziwa wakati wote.
Akilifungua Tamasha la 25 la Utamaduni wa Mzanzibari hapo Mnara wa Kumbukumbu ya Mapinduzi Michenzani Square Balozi Seif Ali Iddi alisema mchango wa Tasnia ya sanaa na ubunifu katika Uchumi wa Zanzibar inakisiwa kuwa asilimia 4.3%  kutoka Mwaka 2010 hadi 2018.
Balozi Seif alieleza kwamba hiyo ni hatua nzuri iliyofikiwa na Tasnia hii katika kuchangia Uchumi wa Taifa huku akizitaka Taasisi zinazohusika na Maendeleo ya Utamaduni na Sanaa kuendelea kujenga mazingira bora zaidi kwa Wazalishaji wa Kazi na bidhaa za Sanaa ili waweze kuyafikia malengo na matarajio ya Taifa.
“ Taasisi husika hazina budi kuwa na takwimu sahihi ya vianzio vya Utamaduni ili kutambua mchango unaopatikana katika Tasnia hii kwa maendeleo ya Kijamii na Taifa kwa jumla”. Alisisita Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitoa wito kwa Jamii ikubaliane na mabadiliko hayo na kutambua kwamba sanaa na utamaduni ni kazi kama zilivyo kazi nyengine katika mfumo wa Kibiashara ambazo zinalindwa kwa misingi ya utaratibu wa Kisheria.
“ Ni vyema kwa Wananchi wakajikita zaidi katika kuzitumia fursa zinazopatikana kupitia Utamaduni wao kama nyenzo muhimu ya Biashara, Ajira na uchumi huku wakiendelea kulinda na kudumisha mila na ahlaki njema zilizopo”. Alisema Balozi Seif.
Alifahamisha kwamba Matamasha ya Kiutamaduni yana umuhimu mkubwa Ulimwenguni  kwa vile ni moja ya bidhaa adhimu zinayosaidia ukuaji wa Sekta ya Utalii inayochangia pamoja na kuimarisha kukuwa kwa Uchumi wa Taifa lolote.
Balozi Seif alieleza kwamba kumekuwa na mabadiliko makubwa ya Kisera katika Mataifa mbali mbali Barani Afrika katika Miaka ya hivi karibuni yanayohusiana na mipango ya Maendeleo na uwiano wake katika Nyanja za Kiutamaduni.
Alisema huo ndio muelekeo wa Kitaifa katika kuhakikisha Utamaduni na sanaa unapewa kipaumbele katika kuchangia Pato la Taifa, huku Tamasha likizingatiwa kuwa ni sehemu ya Mipango ya utekelezaji wa Sera na Majukumu yaliyowekwa katika kuendeleza Utamaduni na Sanaa.
Akizungumzia mmong’onyoko wa maadili ndani ya Jamii ambao bado ni tatizo kubwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Vijana ndio wahanga wa kuiga, kukumbatia na kufuata Utamaduni ambao kimfumo na mwenendo halisi sio silka ya Taifa.
Alisema kutokana na athari za Maendeleo ya Sayansi na Teknolojia Duniani, Jamii imekuwa ikishuhudia jinsi kundi kubwa la Vijana linavyoshawishika na kuvutika na Utamaduni wa Kigeni na hatimae kusahau  mfumo wa maisha yao kupitia kwenye mitindo.
Balozi Seif alitanabahisha kwamba ingawa wigo ni sehemu ya kujifunza na kujenga taswira ya Maendeleo mapya kwa upande Mmoja lakini haupaswi kuchafua misingi na taratibu za maisha zilizowekwa kwa muda mrefu katika mfumo mzima wa maisha ya Jamii.
Alisema kazi ya kufuatilia mienendo ya Watoto bado inapaswa kufanywa na Wazazi na Walezi wenyewe ili wapate nafasi ya kuwarekebisha hasa kwa vile wao ndio wahusika wa ununuzi wa TV na Simu zinazokuwa nafasi kubwa ya mambo yanayoigwa na Vijana hao.
Alisisitiza umuhimu wa kuimarishwa kwa somo la Uzalendo  kwa Vijana hatua kwa hatua kwa lengo la kuwawezesha kujitambua  na kuchukuwa hatua ya kuheshimu  mihimili halisi ya Taifa lao wakiwa tayari kulihami la kulitetea wakati wowote katika maisha yao ya kila siku.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alizipongeza jitihada zinazoendelea kuchukuliwa na Makundi mbali mbali ya Vijana katika kuhakikisha mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia yanalivusha salama Taifa.
Alieleza kwamba Taifa limeendelea kufarijika  kwa mabadiliko yalioanza kujitokeza chini ya usimamizi wa Mabaraza ya Vijana Zanzibar na Tanzania kwa ujumla katika utaratibu wao wa kukabiliana na hali hiyo huku wakiendeleza matunda yaliyoanza kupatikana.
Balozi Seif ameonyesha matumaini yake kutokana na Ujumbe Maalum wa Tamasha la Utamaduni wa Mzanzibar wa mwaka huu usemao “ Amani yetu ni matunda ya Utamaduni wetu uliokuja kipindi muwafaka ambacho Taifa limo katika matayarisho ya kuelekea kwenye uchaguzi Mkuu ifikapo Mwezi Oktoba Mwaka huu wa 2020.
Alisema Wasanii wana wajibu wa kutumia ubunifu wao kuhimiza juu ya kuwepo kwa maisha ya amani, umoja, upendo na utulivu mambo ambayo yamekuwa ni sehemu katika mwenendo wa maisha ya kawaida ndani ya Jamii.
Alifahamisha kwamba uzoefu unaonyesha hali ya amani ikitoweka katika jamii hakuna utaratibu wa maisha utakaonusurika na kuwa salama kwenye maisha ya kawaida ya kila siku.
Akitoa Taarifa ya Tamasha la 25 la Utamaduni wa Mzanzibari Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nd. Amour Khalim Bakar alisema harakati za Tamasha zilianza na Mwaka Kogwa Makunduchi na kufuatiwa na Fensi, mashindano ya Resi za Ngalawa.
Nd. Amour aliwaomba Wananchi kushiriki kwenye Tamasha hilo la Utamaduni la Mzanzibari ikiwa ni ishara ya kuunga mkono Utamaduni Wao uliopata umaarufu sio tuu Mwambao wa Afrika ya Mashariki bali pembe mbali mbali za Dunia.
Akimkaribisha Mgeni rasmi kulizindua Tamasha hilo Waziri wa Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo Balozi Ali Abeid Karume alisema Sekta ya Utamaduni imekuwa na manufaa makubwa kwa Kizazi cha sasa ambacho ndio tegemeo la Taifa hapo baadae.
Balozi Karume alisema aliwapongeza Wananchi, Viongozi na hasa Vijana waliohamasika kushiriki kikamilifu katika shamra shamra za maadhimisho ya Tamasha ra Utamaduni wa Mzanzanzibari lilioasisiwa karibu Miaka 25 sasa  na Rais Mstaafu wa Zanziobar wa Awmu ya Tano Dr. Salmin Amour Juma.
Katika uzinduzi huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alipata fursa ya kukabidhi Tuzo Maalum kwa Wasanii waliotoa mchango mkubwa katika kuitangaza sanaa ya Zanzibar.
Wasanii hapo ni pamoja na Mshauri wa Rais wa Zanziobar katika masuala ya Utamaduni Mheshimiwa  Chimbeni Kheir , Bwana Ali Mwalim Rashid, Bwana Omar Salum Kiwenge, Bibi Khadija Ali Mshamba, Juma Haji Maarufu Halikuniki, Bibi Mwanajuma  Ali Hassan na Bwana Khamis Nyange Maarufu Profesa Gogo.
Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alipata nafasi ya kukagua kazi za Wasanii wa fani mbali mbali ikiwa ni ishara kwa kudni hilo kushiriki vyema katika Tamasha la Utamaduni wa Mzanzibari.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.