Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akiwahutubia Wananchi na WanaCCM Pemba wakati wa mkutano wa mapokezi na kumtambulisha Mgombea Urais wa Zanzibar CCM Mhe.Dkt. Hussein Mwinyi, mkutano uliofanyika Uwanja wa Tibirinzi Chakechake Pemba leo.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein ambaye pia, Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ametoa pongezi
kwa wanaCCM na wananchi kisiwani Pemba kwa mapokezi makubwa waliyomfanyia
mgombea wa Urais kwa tiketi ya CCM Dk. Hussein Ali Hassan Mwinyi.
Dk. Shein aliyasema hayo leo katika hafla ya kumtambulisha
Mgombea nafasi ya Urais kwa tiketi ya CCM Dk. Hussein Ali Hassan Mwinyi kwa
wanaCCM na wananchi wa mikoa miwili ya
Pemba, hafla iliyofanyika katika uwanja wa kufurahishia watoto Tibirinzi Chake
chake Mkoa wa kusini Pemba.
Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwapongeza
wanaCCM na wananchi pamoja na kuzipongeza Kamati zote za maandalizi kwa kuandaa
mapokezi hayo ambayo yametia fora kisiwani humo pamoja na yale yaliyofanyika
hivi karibuni kisiwani Unguja.
Aidha, Rais Dk Shein alisisitiza
kuwa ushindi kwa CCM ni lazima kama inavyoeleza Katiba ya chama hicho kifungu
cha Tano kuwa ushindi ni lazima kwa Tanzania Bara na Zanzibar.
Pamoja na hayo, Rais Dk.
Shein ambaye pia ni Makamo Mwenyekiti wa CCM aliwataka viongozi katika Majimbo
kwenye uchaguzi unaotarajiwa kuanza kesho kuwachagua viongozi makini, wenye
uwezo na bila ya kufanya upendeleo.
Aliwataka viongozi hao
kutowachagua wababaishaji wenye tamaa na badala yake wawachague viongozi
watakaokiimarisha chama hicho.
Alieleza kuwa CCM ni
chama kikubwa sana kina viongozi mbali mbali wenye sifa hivyo wasing’ang’aniwe
viongozi waliokuwa hawana sifa hao kwa hao kila siku na kusisitiza kuwa ni
vyema wakawachagua viongozi wenye sifa ambao wakisimama wanasikilizwa na
wanamvuto kwa wapiga kura.
Alisema kuwa viongozi
wanaotakiwa wawe na sifa nzuri ambazo wataweza kufanya kazi na Dk. Hussein Ali
Hassan Mwinyi “Wajadilini kama tulivyowajadili wale 31 waliogombania nafasi ya
Urais kupitia chama chetu, wajadilini nje ndani ndani nje”, alisisitiza Makamo
huyo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar.
Alieleza kuwa CCM ina
sifa kumi na mbili ambazo mtu ama
mgombea hutakiwa kuwa nazo, ambapo kwa mgombea wa urais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi ni miongoni mwa viongozi wenye sifa zote
hizo.
Makamo Mwenyekiti huyo
wa CCM Zanzibar alimuelezea mgombea huyo kuwa ana heshima kubwa kwenye Serikali
pamoja na ndani ya CCM.
Nae Mgombea wa Nafasi
hiyo ameahidi kusimamia maslahi ya Zanzibar katika Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar pamoja na kusimaamia maslahi ya Zanzibar katika Jumuiya ya Afrika Mashariki
pamoja na Jumuiya za Kimataifa kwa ajili ya kuleta maendeleo.
Mgombea huyo alisisitiza
haja ya kupata ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa mwaka huu na kueleza kuwa
ushindi wa mwaka uwe ushindi mkubwa na usiwe ushindi mwembamba ambao utaleta
malalamiko na kueleza kwamba kutokana na mapokezi hayo hana wasi wasi kuwa
ushindi utakuwa wa kishindo.
Alisema kuwa ushindi
huo utapelekea kuunda Serikali itakayokuwa na maslahi kwa wananchi wote huku
akiwahakikishia kuwa Serikali atakayoiunda itawatumikia wananchi wote.
“Yajayo yanafurahisha
naahidi kwamba tutaboresha maisha ya Wazanzibari....hisani hulipwa kwa hisani
na hivyo na mimi naahidi hisani ya kuwatumikia wananchi ”,alisema Dk. Hussein
Mwinyi.
Aidha, alipongeza
risala na kusema kuwa salamu amezipokea huku akitoa shukurani na pongezi kwa
mapokezi aliyoyapata kisiwani humo.
Alisisitiza haja ya
kuwachagua viongozi bora katika chaguzi za chama hicho zinazoanza kesho
zikiwemo nafasi za Ubunge, Uwakilishi na Udiwani ili iwe rahisi kuyatekeleza yale
yanayoahidiwa na Chama hicho.
Dk. Hussein Mwinyi
aliwathibitishia wananchi kwamba yeye hajamtuma mtu hata mmoja ili agombee
katika chama hicho kwa azma ya kuja kumteuwa kuwa Waziri na kusisitiza kwamba
kila mmoja apambane na hali yake.
Katika
hatua nyingine, Mgombe huyo wa urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, alisema
kama atapata ridhaa ya kuiongoza Zanzibar, atafanyakazi kwa maslahi ya watu
wote na kamwe hatowavumilia wala rushwa, wazembe na wasiowajibika.
Alisema
kama wapo watendaji wa aina hiyo na hawamjui yeye utendaji wake, basi watamjua
muda mfupi tu baada ya kuwa rais wa Zanzibar, baada ya uchaguzi unaotarajiwa
kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.
“Nitafanya
kazi kwa maslahi ya watu wote, nitahakikisha watu wote wanafanya kazi ipasavyo,
kwa dhamira ya kuwatumikia Wazanzibari wote na sio vyenginevyo tena bila ya
ubaguzi”, alisema.
Akizungumzia
suala la amani na utulivu wa nchi, Dk. Mwinyi alisema kuwa atahakikisha amani
iliyopo Zanzibar itaendelea kudumu hivyo, aliwataka wananchi kudumisha umoja
huku akiamini kuwa ndio silaha pekee ya kuwaletea maendeleo.
“Umoja
wetu tutauenzi, tutaudumisha na hata katika masuala ya ajira nitahakikisha
kwamba hakutakuwa na ubaguzi…..,”alisema.
Nae
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdalla Mabodi alieleza hatua
zilizochukuliwa na chama hicho kuwapata wagombea Urais na hatimae kumpata
kinara wa kupeperusha bendera kwa tiketi ya CCM huku akiwapongeza wanaCCM na
wananchi wa Pemba kwa mapokezi makubwa.
Nao wanaCCM, waliokuwa
wagombea nafasi ya Urais kwa tiketi ya CCM na kuingia tano bora walitoa maneno
yao ya shukurani huku wakimuahidi Dk. Hussein Mwinyi kuwa watakuwa nae bega kwa
bega na kuwataka wanaCCM na wananchi kuendelea kumuunga mkono pamoja na
kukiunga mkono chama hicho.
Katika salamu za
WanaCCM wa Mikoa miwili ya Pemba kwa mgombea Urais wa Zanzibar Dk. Hussein
Mwinyi walieleza kuwa chama hicho kimepata nahodha mweliedi, mahiri, mzoefu,
mchapa kazi na asiyechoka wala kuogopa anaeelewa mazingira ya pepo zote za
bahari asiyechoka wala kukata tamaa.
Waliongeza kuwa
wanaamini kuwa mgombea huyo atawavusha salama kwa malezi aliyolelewa yeye ni
mtoto mwema na atawapeleka wanakotaka kwenye maendeleo endelevu ya nchi.
“Karibu Pemba kwa
WanaCCM wenzako tunakukubali, tunakupenda, tunakuthamini, tunakutaka,
tumekuchagua na tunakuahidi tutakupa kura za kutosha ili uiongoze nchi yetu,
Mhe. Mgombea ondoa hofu Pemba ya jana sio ya leo” walieleza wana CCM hao.
Aidha, walitumia fursa
hiyo kumpongeza Mwenyekiti wa CCM Taifa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
John Pombe Magufuli na Makamo Mwenyekiti wa chama hicho kwa upande wa Zanzibar
Dk. Ali Mohamed Shein kwa kuongoza vyema mchakato wa kumpata mgombea Urais wa
Tanzania na Rais wa Zanzibar.
Nao waliokuwa
wanachama wa vyama vya upinzani waliojiunga na CCM, walieleza azma yao ya
kumuunga mkono Dk. Mwinyi pamoja na kuiunga mkono CCM ili ishinde uchaguzi ujao
kwa kishindo.
Mapema ndege ya Shirika la ndege la “Pression Air”
ilituwa katika kiwanja cha ndege cha Pemba, mnamo majira ya saa 4:11 asubuhi ambayo
ilimchukua mgombea huyo ambaye alipokelewa kwa vifijo na nderemo kutoka kwa
Wanachama na wapenzi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) pamoja na wananchi mbali
mbali waliokuwa na shauku kubwa ya kumpokea Mgombea wao wa Urais wa Zanzibar
kupitia Chama hicho Dk. Hussein Ali Mwinyi.
Mamia ya wanaCCM walifurika katika kiwanja hicho
kwa ajili ya kumpokea Mgombea huyo akitokea Unguja , huku rangi na kijani
kibichi na njano kavu ikitawala ambayo ni sare ya Chama hicho kiwanjani hapo.
Bendi ya Chipukizi pamoja na ngoma nyengine za kienyeji
zilitowa burudani ya muruwa katika Kiwanja hicho, ikiwa ni ishara ya furaha ya
mapokezi ya mgombea Urais wa Zanzibar
kwa tiketi ya CCM Dk. Hussein Mwinyi.
Pamoja na mapokezi hayo, katika kiwanja cha Ndege
cha Karume Pemba wananchi wakiwemo wanachama , wapenzi wa Chama hicho walipata
fursa ya kujipanga kando kando ya bara bara kwa ajili ya kumpokea mgombea huyo
baada ya kufika Kisiwani Pemba kwa utambulisho.
Wananchi na WanaCCM hao walijipanga barabarani
kutoka kiwanja cha ndege hadi Kiwanja cha kufurahishia watoto Tibirinzi nje
kidogo ya mji wa Chake Chake Pemba.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment