Habari za Punde

Zoezi la Kukabidhi Vitambulisho Kwa Wapiga Kura Kufanyika Leo Unguja Katika Vituo 272.

Na JaalaMakame Haji- ZEC
Wapiga Kura wanaokwenda kuchukua wameshauriwa kufuata njia sahihi ikiwemo kuwasiliana na Maafisa Uchaguzi wa Wilaya katika kupata ufafanuzi endapo watakabiliana na changamoto katika vituo vya kuchukulia vitambulisho vya kupigia kura.

Mkurugenzi wa Uchaguzi Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ZEC Ndg.Thabiti Idarous Faina  alitoa ushauri huo wakati akizungumza na Waandishi wa habari huko Ofisini kwake Maisara Jijini  Zanzibar.

Mkurugenzi Faina alisema, Tume tayari imetoa mafunzo kwa watendaji walioteuliwa kusimamia zoezi la ugawaji wa vitambulisho katika vituo kwa lengo la kurahisha zoezi hilo ili kila mpiga kura apate haki yake bila usumbufu huo.

Ndugu Faina aliendelea kusema kuwa, katika mafunzo hayo, Tume iliwaasa watendaji hao kutumia lugha nzuri kwa Wananchi ili kuondosha minong’ono itakayoashiria vurugu na kumfanya mpiga kura kuridhika na mwenendo wa utoaji wa vitambulisho hivyo.

Katika mazungumzo yake, Mkurugenzi alisisitiza kuwa, Tume itahakikisha kila Mpiga Kura anapata kitambulisho chake cha kupigia kura ambapo aliwaomba wapiga kura hao kujitokeza kwa wingi katika vituo ili kupata haki yao hiyo.

Hata hivyo, alisema kwamba, zoezi hilo litaendelea kufanyika katika Ofisi za Uchaguzi za Wilaya baada ya kukamilika siku mbili za utoaji wa vitambulisho ambazo zilipangwa katika vituo vilivyotumika kwa zoezi la uandikishaji na uhakiki wa taarifa za Wapiga Kura

Aidha, aliongeza kusema kuwa, wakati wa zoezi hilo likendelea katika vituo Tume, haitosita kumchulia hatua mtendaji yeyote atakayebainika kukiuka maelekezo aliyopatiwa na Maafisa wa Tume ikiwa pamoja na kutumia lugha mbaya wakati anapotoa huduma kwa Mpiga Kura.

“Tumewaelekeza watendaji wetu vituoni kutumia lugha nzuri kwa wateja ambao ni Wapiga kura kwa hiyo hatutosita kumchulia hatua mtendaji atakaye kiuka maelekezo tuliyompatia” alisema.

Mkurugenzi Faina aliwaomba waandishi wa habari kuwaelimisha wananchi katika kutumia huduma iliyoanzishwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ya kutumia mtandao wa Zantel kwa kupiga namba *152*29# ili kujua kitambulisho chako kilipo na namba ya box la kitambulisho hicho.

Zoezi la uchukua wa vitambulisho vya kupiga kura linatarajiwa kuanza tarehe 25 hadi 26 mwezi huu katika vituo 272 vya Wilaya zote za Unguja ambapo zoezi kama hilo lilifanyika tarehe 18 hadi 19 mwezi huu kwa upande wa vituo 135 vya Wilaya zote za Pemba.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.