RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, ambaye pia ni Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar leo alikuwa ni miongoni mwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu waliopiga Kura ya Maoni kumchagua Mbunge na Mwakilishi wa Jimbo la Tunguu.
Zoezi hilo limefanyika leo huko katika ukumbi wa
Dk. Ali Mohamed Shein uliopo Kampasi ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar
(SUZA), huko Tunguu Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.
Makamo Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar akiwa
miongoni mwa Wajumbe hao alishiriki kikamilifu katika zoezi hilo la kuwachagua
viongozi hao wa Jimbo la Tunguu akiwa ni miongoni mwa Wajumbe 160 waliohudhuria
kati ya Wajumbe wote 176 wa Jimbo hilo.
Zoezi hilo lilikuwa na jumla ya wagombea wa nafasi
ya Ubunge ambao jumla yao walikuwa kumi na wagombea nafasi ya Uwakilishi jumla
yao walikuwa ni 14 ambao mapema walipata fursa ya kujielezea na kunadi sera zao
mbele ya Wajumbe hao wa Mkutano Mkuu wa Jimbo hilo.
Mapema Mwenyekiti wa CCM Jimbo la Tunguu Ramadhan
Khatib Ramadhan aliwasihi Wajumbe wa Mkutano Mkuu huo kuwa zoezi hilo ni
utaratimu maalum uliowekwa na Chama Cha Mapinduzi kwa kila ifikapo miaka mitano
ya uchaguzi.
Alisema kuwa utaratibu huo ni kwa mujibu wa sheria
na Katiba ya CCM ambao unakiongoza chama hicho.
Aidha, aliwataka wagombea wote wa nafasi hizo
kukubali na kuridhika na matokeo watakayoyapata kwani waliogombea nafasi hizo
ni wengi lakini wanaohitajika ni mmoja kwa nafasi ya Uwakilishi na mmoja kwa
nafasi ya Ubunge wa Jimbo hilo.
Mwenyekiti huyo wa CCM Jimbo alisisitiza haja ya
kuwachagua viongozi wenye sifa na walio na uwezo wa kukitetea chama hicho na
kukitumikia kwa moyo wao wote kutokana na chama hicho kuimarika kwa muda mrefu
na kuweza kuasisiwa tokea Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964.
Pamoja na hayo, kiongozi huyo aliwaeleza Wajumbe
na wagombea nafasi hizo kwamba uchaguzi huo utakuwa wa huru na haki kwa kufuata
miongozo yote ya Chama hicho cha CCM sambamba na Katiba, sheria na kanuni zake.
Hapo jana wakati akimtambulisha Mgombea nafasi ya
Urais kwa tiketi ya CCM Dk. Hussein Ali Hassan Mwinyi kwa wanaCCM na wananchi wa mikoa miwili ya Pemba, hafla iliyofanyika
katika uwanja wa kufurahishia watoto Tibirinzi Chake Chake Mkoa wa kusini Pemba,
Rais Dk. Shein aliwataka viongozi katika Majimbo yote nchini kuwachagua viongozi
makini, wenye uwezo na tena bila ya kufanya upendeleo.
Rais Dk. Shein aliwataka
viongozi hao katika uchaguzi unaofanyika hivi leo kutowachagua wababaishaji
wenye tamaa na badala yake wawachague viongozi watakaokiimarisha chama hicho.
Makamo Mwenyekiti huyo
alieleza kuwa CCM ni chama kikubwa sana kina viongozi mbali mbali wenye sifa
hivyo wasing’ang’aniwe viongozi waliokuwa hawana sifa hao kwa hao kila siku na
kusisitiza kuwa ni vyema wakawachagua viongozi wenye sifa ambao wakisimama
wanasikilizwa na wanamvuto kwa wapiga kura.
Alisisistiza kuwa
viongozi wanatakiwa wawe na sifa nzuri ambazo wataweza kufanya kazi na Dk.
Hussein Ali Hassan Mwinyi “Wajadilini kama tulivyowajadili wale 31
waliogombania nafasi ya Urais kupitia chama chetu, wajadilini nje ndani ndani
nje”, alisisitiza Makamo huyo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment