Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein Ametowa Salamu za Rambirambi ya Kifo Cha Rais wa Awamu ya Tatu wa Tanzania Benjamin William Mkapa.


KIFO cha Marehemu Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bejamin William Mkapa kimeacha pengo kubwa katika uongozi na maendeleo ya Tanzania, Afrika na duniani kote kwa mchango wake uliooendelea kuhitajika ndani na nje ya mipaka yaTanzania.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, aliyasema hayo leo  katika risala aliyoitoa kupitia vyombo vya habari kufuatia kifo cha Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bejamin William Mkapa, kilichotoke usiku wa kuamkia Ijumaa ya tarehe 24 Julai, 2020.

Katika risala yake hiyo Rais Dk. Shein alisema kuwa Marehemu Mzee Mkapa alikuwa na uwezo mkubwa wa kubuni mambo mapya ya maendeleo ambapo miongoni mwa mambo makubwa ambayo aliyaanzisha katika kipindi chake cha uongozi ni kuunda Mamlaka ya Kodi ya Mapato Tanzania (TRA).

Alisema kuwa aliunda (TRA) ili kuimarisha ukuaji wa uchumi, kuongeza ukusanyaji wa mapato na kuiwezesha Tanzania kujitegemea ambapo jitihada zake hizo zilipelekea Tanzania kukua kwa uchumi wake.

“Tulianza kulipa madeni ambapo baadae nchi yetu ilisamehewa madeni yake, tulianza kuaminiwa na tukawa tunakopesheka”, alisema Dk. Shein.

Aidha alieleza kuwa katika kipindi chake cha miaka kumi uchumi ulikuwa kutoka asilimia 3.6 hadi 6.7 sambamba na hatua hiyo, alichukua hatua za kubinafsisha  Mashirika ya Umaa ambayo yalikuwa yakiendeshwa kwa hasara na kuuletea mzigo mkubwa kwa Taifa.

Akimuelezea Marehemu Mkapa, Rais Dk. Shein alisema kuwa vilevile aliansha Mpango wa Kukuza Uchumi na Kupinguza Umasikini( MKUKUTA),(MKURABITA) na (TASAF), pamoja na kuanzisha Wakala kadhaa kama vile EWURA,SUMATRA kwa ajili ya kudhibiti na kutoa huduma bora kwa jamii.
Alieleza kuwa baada ya kustaafu kwake aliansiha Taasisi Isiyo ya Kiserikali  ya Benjamin Mkapa, ambayo inayoshughulikia masuala ya afya hasa mapambano dhidi ya UKIMWI.

Katika masuala ya kupiga vita rushwa na ufisadi, kiongozi huyo alianzisha Tume Maalum maaraufu kwa jina la Tume ya Warioba iliokuwa na lengo la kupendekeza njia bora za kuzuia mianya na vitendo vya rushwa.

Alisema kuwa matokeo ya jitihada hizo ni kuanzisha kwa taasisi ya kudhibiti na kuzuia rushwa Tanzania (TAKUKURU) na hatimae kupelekea kuundwa kwa Mahakama maalum ya wahujumu uchumi katika Awamu ya Tano ya Jamhuri ya Mungano wa Tanzania.

Kutokana na kauli mbiu yake ya “Uwazi na Ukweli”, Rais Mkapa alianzisha Wizara Maalum inayoshughulikia Utawala Bora, kadhalika alianzisha vitengo vya habari na Mawasiliano katika Wizara na Mashirika pamoja na kuanzisha utaratibu wa kuwahutubia wananchi kila mwezi.

Alisema kuwa hatua hizo zimewawezesha wananchi kuyafahamu matokeo muhimu ya Kitaifa na Kimataifa ambapo pamoja na suala hilo Marehemu Mzee Mkapa alitambua mapenzi ya Watanzania katika sekta ya michezo kwa hivyo, alihakikisha anawajengea wananchi kiwanja cha michezo cha kisasa chenye kiwango cha kimataifa.

Katika uwanja wa siasa, Rais Dk. Shein alisema kuwa Marehemu Mkapa alikuwa ni mfano wa wanasiasa bora walioweka mbele maslahi ya Taifa na kuongoza kwa mifano.

Alisema kwua kwa uhodari mkubwa aliokuwa nao Marehemu Rais Mkapa, aliweza kuendesha siasa za vyama vingi kwa haki na demokrasia ambapo uongozi wake wa miaka kumi akiwa Rais, uliipatia Tanzania heshima kubwa katika Jumuiya ya Kimataifa na ndani ya Taifa hili.

“Alipenda mashirikiano na kuheshimu mawazo ya kila mmoja na wakati wote alikuwa mchangamfu na mwenye tabasam….alikuwa na uwezo mkubwa wa kuhimili changamoto za uwongo kila zinapotokea”, alisema Dk. Shein.

Aidha, aliongeza kuwa Rais Mkapa alikuwa kiongozi asiyependa fitina na majungu na siku zote huwapongeza wanaofanya vizuri pamoja na kuwasamehe wale wanaotubu makosa yao kwake kwa dhati.

Rais Dk. Shein alisema kuwa Rais Dk. Shein alikuwa mstari wa mbele katika kutetetea na kuzienzi tunu za Taifa zikiwemo umoja wa Watanzania, Mapinduzi ya Zanzibar na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Katika kuamini kwake umuhimu wa kuendeleza umoja na mshikamano miongoni mwa mataifa ya Afrika Marehemu Mzee Mkapa alitoa mchango mkubwa katika kuanzishwa upya kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kuumarisha mtengemano wa nchi na wananchi wa nchi za Afrika Mashariki.

Rais Dk. Shein alisema kuwa Marehemu Mkapa alikuwa muumini wa dhati wa amani ya nchi ambapo katika kutilia mkazo umuhimu wa kutunza amani kwa maendeleo ya Taifa katika moja ya hutoba zake alisisitiza umuhimu huo kwa kusema

“Nchi hii ni nchi yetu sote ni ya watoto wetu na vizazi vyetu vijavyo. Ikiwa na amani ni amani ya Watanzania wote ikiwa ya vurugu ni vurugu itakayowaathiri Watanzania wote. Tukivurugana MwenyeziMungu hatotupa ardhi nyengine,tuamue basi kuijenga Tanzania ya demokrasia ya kweli, Tanzania inayoheshimu haki za binaadamu, Tanzania inayopiga haraka hatua za maendeleo, Tanzania ya amani, upendo, umoja na mshikamano”.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein, alisema kuwa Marehemu Mzee Mkapa alikuwa na sifa ya kuibua vipaji vya viongozi wachanga, kuwajenga na kuwakuza na hatimae viongozi hao kutoa mchango mkubwa katika Taifa.

Rais Dk. Shein alisema kuwa yeye mwenyewe binafsi alijifunza mambo mengi sana na kupata mashirikiano ya hali ya juu kutoka kwa Marehemu Rais Mkapa kwa kiasi cha kupata weledi mkubwa wa kuyatekeleza majukumu yake katika uongozi.

Vile vile, Rais Dk. Shein aliwasihi Watanzania kuendelea kuwa wamoja, kuyaenzi na kuyadumisha yale yote aliyoyaacha Mzee Mkapa huku akisisitiza kuwa ni vyema kuzingatia fikra na mawazo yake kupitia hotuba zake mbali mbali pamoja na yale yaliomo katika kitabu chake cha “My Life My Purpose” (Maisha yangu Kusudi langu).

Rais Dk. Shein aliongeza kuwa kwa niaba ya Wananchi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar anaungana na wanafamilia, ndugu, marafiki na Watanzania wote katika kipindi hichi kigumu cha majonzi na huzuni.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.