Habari za Punde

Taasisi na Mashirika Yapongezwa Kwa Misaada Yao.

Na Hamida Kamchalla, TANGA.
WAZIRI wa Afya, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu amezipongeza Taasisi na Mashirika mbalimbali mkoani Tanga kwa kujitolea misaada na kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali ya awamu ya tano.

Aliyasema hayo wakati akiweka jiwe la msingi na kuzindua majengo ya vyumba vya madarasa katika shule ya sekondari ya Mnyanjani iliyoko jijini Tanga.

Mhe. Mwalimu alibainisha kwamba zipo Taasisi na Mashirika yanayostahili kupongwezwa kwa juhudi za kupambana na kuisaidia serikali kwani yanatoa hamasa hata kwa wananchi kuweza kujitolea michango yao pamoja na nguvu kazi kwa kushiriki shughuli za maendeleo ya jamii.

"Nipende kuwapongeza wafadhili wanaojitolea kuunga mkono juhudi za serikali yetu ya awamu ya tano chini ya Dkt. John Pombe Magufuli na vilevile niyaombe Mashirika mengine na taasisi kuiga mifano ya wengine katika kuchangia maendeleo ya wananchi wa Tanga na Tanzania kwa ujumla" alisema Mhe.Mwalimu.

Ujenzi wa madarasa hayo umejengwa kwa ufadhili wa Taasisi ya Nailkant chini ya Mkurugenzi wake Rashid Hamud (Liemba) ambapo pia umekwenda sambamba na ujenzi wa majengo mengine ya kutolea huduma muhimu za elimu ambao umefadhiliwa na African Evangelistic Enterprises kwa kushirikiana na Umoja wa Makanisa jijini Tanga.

Awali akisoma risala mbele ya Waziri huyo, Mkuu wa shule hiyo Ndg.Said a Mahadhi alisema kuwa shule hiyo ilikuwa na uhaba wa matundu ya vyoo vya wanafunzi pamoja na nyumba ya Mwalimu ambapo Taasisi mbili zimejitolea kujenga.

"Vyoo vya wanafunzi vimejengwa na kanisa la Tanzania Assembles of God (TAG) la mjini hapa, nyumba ya Mwalimu imejengwa kupitia mpango wa maendeleo ya elimu za sekondari (MMES) lakini pia tuna vyumba vingine viwili vya madarasa vimejengwa na mradi wa Education Performance for Results (EP4R)" alisema Mahadhi.

Aidha alisema kuwa vyumba vingine viwili vya madarasa vimejengwa kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri ya jiji la Tanga kwa kushirikiana na nguvu za wananchi huku vyumba nane vikijengwa kwa ruzuku kutoka serikali kuu.

Hata hivyo Mahadhi aliwashukuru wafadhili kwa misaada yao na kuongeza kuwa kwasasa wanafunzi hasa wa kike wamekuwa wakisoma kwa uhuru kutokana na ongezeko la matundu ya vyoo ambayo awali walikuwa wakilazimika kutoka shuleni hapo na kwenda kujisaidia kwenye nyumba za jirani.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.