Habari za Punde

Watangaza Nia ya Urais Anayetakiwa ni Mmoja Tu Aungwe Mkono na Makundi Yote Waliosimamia Waomba Nafasi Hiyo Kwa Upande wa Zanzibar.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif ALI Iddi akizungumza na Wajumbe wa Halmashauri ya CCM Mkoa na wale wa Mabaraza ya Jumuiya za CCM  Mkoa  Kaskazini Pemba hapo katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Micheweni. 
Wajumbe wa Halmashauri ya CCM Mkoa na wale wa Mabaraza ya Jumuiya za CCM  Mkoa  Kaskazini Pemba wakihamasika na kushangiria Hotuba ya Mjumbe wa Kamati Kuu Balozi Seif.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis. OMPR.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi alisema mgombea atakayekabidhiwa Bendera ya CCM kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba Mwaka huu atapaswa kuungwa mkono kwa asilimia kubwa  na Wanachama wote ili apate nguvu zitakazoiwezesha CCM iendelee kuongoza Dola Bara na Zanzibar.
Alisema watangaza nia ya Urais wa Zanzibar kupitia CCM anayetakiwa ni Mmoja na akishapatikana kupitia mchakato wa upembuzi utakaofanywa na Viongozi wa ngazi tofauti za Chama lazima aungwe mkono na makundi yote yaliyosimamia waomba nafasi hiyo kwa upande wa Zanzibar.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na Wajumbe wa Halmashauri ya CCM ya Mkoa pamoja na Wajumbe wa Mabaraza ya Jumuiya za CCM wa Mkoa  Kaskazini Pemba hapo katika Ukumbi wa Chama uliopo Micheweni Kaskazini Pemba.
Alisema katika kumpata Mwana CCM mahiri na Mzalendo anayeuzika kwa Wananchi Viongozi watakaohusika katika uteuzi huo waelewe kwamba wanabeba dhima kuhakikisha Yule watakayemteuwa bila shaka anauzika  hasa kwa upande wa Zanzibar kwa vile Jamuhuri ya Muungano anaendelea kubeba jukumu hilo.
“ Mgombea atakayefanikiwa kupata ridhaa ya Wananchi waliowengi atakuwa na kazi ya kubeba dhima ya kusimamia maendeleo ya Taifa na kustawisha Maisha ya Umma”. Alisema Balozi Seif.
Kwa upandwe wa nafasi ya Ubunge, Uwakilishi na Udiwani Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM Taifa alisema Viongozi na Wananchi wa Majimbo wao ndio wanaowaelewa kwa kina Watu wenye sifa za kujitolea katika kuwatumikia kwa kipindi cha Miaka Mitano.
Balozi Seif  alifahamisha kwamba Wanachama wanaobahatika kupewa jukumu la kuwatumikia Wananchi na baadae kuhamia kimaisha katika maeneo mengine hawafai na wapiga kura lazima wajitahadhari na watu wenye tabia hiyo ambao wengine tayari wameshaonyesha tabia hiyo chafu katika Utumishi wa Umma.
Alieleza kwamba Viongozi wanaokabidhiwa dhama ya kuwatumia Wananchi lazima wajielewe kwamba wao ni Watumishi wa Umma na sio Watawala kama baadhi yao wanavyofikiria katika akili zao kwa vile walitumia rushwa katika kupata nafafsi hizo.
“ Kiongozi  hatakiwi kwa fedha zake bali apewe dhamana kwa mujibu wa Uzalendo wake unaompa nguvu za kuwatumikia Wananchi katika eneo lake la Utumishi”. Alisisitiza Balozi Seif.
Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM Taifa akiwa pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza Viongozi na Wananchi Kisiwani Pemba kwa umahiri wao uliowezesha Kisiwa hicho kuwa salama na wimbi la Maambukizo ya Virusi vya Corona vilivyotawala Dunia.
Balozi Seif alisema kitendo cha Viongozi na Wananchi wanaowaongoza kufuata miongozi ya Wataalamu wa Afya pamoja na kauli za Viongozi wa Kitaifa ndicho kilichowapunguzia hofu na kujikuta wakiendelea na harakati zao za kimaisha bila ya wasi wasi wowote.
Aliwakumbusha Wananchi na Viongozi hao licha ya kupungua kuenea kwa Virusi vya Corona Nchini lakini bado wanapaswa kuendelea kuchukuwa tahadhari za kujikinga na janga hilo kwa kunawa mikono kila mara kwa maji ya kutiririka sambamba na kutumia vitakasa mikono.
Alifafanua kwamba kufanya hivyo licha ya Wataalamu kueleza kwamba Virusi vya Corona vitaendelea kuwepo miongozi mwa Jamii lakini wakifanya hivyo watajihakikishia kuishi salama.
Akigusia zoezi la mchakato wa Uchaguzi ndani ya Chama Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Balozi Seif  alisisitiza umuhimu wa Wanachama na wagombe nafasi tofauti za Uongozi  kuzingatia maadili na kanuni za uchaguzi ili mchakato huo umalizike kwa mafanikio.
Alisema wapo baadhi ya Wanachama kwa kushirikiana na waliotia nia ya kugombe nafasi za Uongozi wameanza Kampeni kwa kuwatumia Mawakala kumwaga fedha jambo litaloweza kuwaponza katika safari  yao ya baadae kwenye mchakato mzima.
Aliendelea kukumbusha kwamba kitendo cha kumchagua Kiongozi kwa kutumia rushwa hatima yake ni kumpata Kiongozi asiyezingatia maadili katika kusimamia Ilani ya Uchaguzi dhambi ambayo Uongozi wa CCM hautakuwa tayari ifanyike kwa maslahi na maendeleo ya Taifa.
Akitoa Taarifa fupi ya Chama cha Mapinduzi ndani ya Mkoa wa Kaskazini Pemba Katibu wa CCM wa Mkoa huo Bibi Khadija Nassor Abdi alisema Uongozi wa Mkoa huo umefanikiwa vyema kusimamia Ilani ya Uchaguzi ndani ya Miaka Mitano inayomalizika Mwezi Oktoba Mwaka huu.
Bibi Khadija alisema ipo Miradi ya Maendeleo iliyopata kukwamuka katika utekelezaji wake ambacho ilikuwa changamoto kubwa vipindi vilivyopita akitolea mfano Miundombinu ya Mawasiliano ya Bara bara, Maji safi na salama, Elimu na huduma za Afya.
Mapema Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi kupitia Mkoa wa Kaskazini Pemba Nd. Omar Zubeir  akimkaimu Mwenyekiti wa CCM Mkoa huo alisema Uongozi wowote ule huambatana na nguvu ya Mungu. Hivyo Wanachama hawana haja ya kulumbata katika mchakato wowote ule.
Alisema kinachohitajika ni kwao kuzingatia Sheria, Kanuni, Miongozo na taratibu zilizowekwa mfumo ambao hupatikana Yule wanayemkusudia kwa njia ya Amani, Upendo na Umoja ukiambatana na nguvu hizo za Mungu.
Nd. Omar Zubeir alisema hata Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Taifa ambae pia ni Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli amekuwa akisisitiza umuhimu wa Viongozi, Wanachama na Wananchi kuheshimu nguvu za Mungu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.