Habari za Punde

WAZIRI MKUU AONGOZA MAPOKEZI YA MWILI WA MZEE MKAPA MASASI

 
Mwili wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin William Mkapa ukitelemshwa  kutoka kwenye helkopta  ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wakati  ulipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Masasi kutoka Dar es salaam Julai 28, 2020 na baadae kupelekwa  kijijini  Lupaso  wilayani Masasi kwa mazishi yanayotarajiwa kufanyika kesho.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Sif Ali Idd (wa pili kushoto) wakizungumza kwenye uwanja wa ndege wa Masasi wakati wakisubiri helkopta ilyobeba mwili wa  Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin William Mkapa, Julai 28, 2020. Wa  pili kulia ni Mke wa Waziri Mkuu, Mama Mary Majaliwa na kulia ni Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mama Asha. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)


WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amewaongoza wananchi wa wilaya ya Masasi na maeneo mengine katika kuupokea mwili wa aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin William Mkapa katika uwanja wa Ndege wa Masasi, Mtwara ukitokea jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu aliwasili katika uwanja wa Ndege wa Nachingwea akiwa ameongozana na  mjane wa marehemu Mama Anna Mkapa, Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Mke wa Waziri Mkuu Mama Mary, Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mama Asha, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama.

Mheshimiwa Majaliwa pamoja na viongozi alioongozana nao waliondoka Nachingwea na kuelekea wilayani Masasi kwa ajili ya kuupokea mwili wa Mzee Mkapa ambao uliwasili katika uwanja wa Ndege wa Masasi leo (Jumanne, Julai 28, 2020) saa 8.50 mchana baada ya kumalizika kwa zoezi la kumuaga Kitaifa lililofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam na kuongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli.

Baada ya mwili huo kuwasili uwanjani hapo saa 9.00 alasiri ulishushwa kwenye helikopta na kuingizwa kwenye gari maalumu, msafara uliondoka kuelekea kijijini Lupaso ambapo vilio, majonzi na simanzi vilitawala kwa wananchi waliokuwa wamesimama pembeni mwa barabara kwa ajili ya kutoa heshima za mwisho.

Mwili wa aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu Mzee Mkapa uliwasili katika Kanisa Katoliki Parokia ya Lupaso jimbo la Tunduru-Masasi saa 10.10 jioni na kuanza kwa ibada takatifu ilianza. Ibada hiyo iliongozwa na Askofu wa Jimbo la Masasi-Tunduru, Askofu Filbert Mhasi.

Kwa upande wake, Askofu Mhasi ametumia fursa hiyo kuwahamasisha wananchi wapende kufanya mambo mema kwa kuwa ndiyo yatakayowaenzi na kuwafanya waendelee  kukumbukwa mioyoni mwa watu. “Mzee wetu Mkapa alikuwa mtu mwema mwenye mahusiano mazuri na jamii bila kujali jinsia, kabila wala dini.”

Amesema kuwa marehemu Mzee Mkapa atabaki kuwa kielelezo kwa wananchi wa Lupaso Jimbo la  Tunduru - Masasi na Taifa kwa ujumla kwa kuwa alikuwa ni mtu mnyeyekevu na mtii. Askofu Mhasi ametoa pole kwa Watanzania wote, mjane wa marehemu Mama Anna Mkapa na familia.

Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Mhe. Benjamini William Mkapa amefariki dunia usiku wa kuamkia Ijumaa, Julai 24, 2020 hospitalini jijini Dar es Salaam ambako alikuwa akipatiwa matibabu na anatarajiwa kuzikwa kesho Jumatano, Julai 29 kijijini kwao Lupaso wilayani Masasi, Mtwara.


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, JULAI 28, 2020.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.