Habari za Punde

Balozi Seif aufungua rasmi mradi wa maji safi na salama Fujoni

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiufungua rasmi Mradi wa Maji safi na salama  uliotekelezwa kwa nguvu za Wananchi wenyewe wa Kijiji cha Fujoni Wilaya ya Kaskazini “B”.
  Haiba ya Mradi wa Maji safi na salama unavyoonekana baada ya kukamilika kwake utakaohudumia Zaidi ya Wananchi Mia Tatu wa Kijiji cha Fujoni uliobuniwa na Wananchi wenyewe.
 Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini B Nd. Rajab Ali Rajab akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa Mradi wa Maji safi na salama wa Kijiji cha Fujoni Wilaya ya Kaskazini B.
 Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi akitoa salamu kwenye hafla ya ufunguzi wa Mradi wa Maji safi na salama wa Kijiji cha Fujoni Wilaya ya Kaskazini B.
Balozi Seif Ali Iddi akipokea zawadi ya Madafu ya Kitamli kutoka kwa Wananchi wa Kijiji cha Fujoni mara baada ya kuufungua Mradi wa Maji safi na salama wa Kijiji hicho.
Picha na – OMPR – ZNZ

Na Othman Ame, OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Viongozi wanaochaguliwa katika Majimbo pamoja na Wadi wana wajibu wa kuhakikisha kero zinazowakabili Wananchi za kila siku katika maeneo yao zinapatiwa ufumbuzi unaostahiki.
Alisema wajibu huo unakuwa dhima kwao kwa vile Viongozi hao hutafakari, kujipima na hatimae uwezo walionao nao huwashawishi kufikia hatua ya kuamua kutekeleza jukumu hilo la kuwatumikia Wananchi.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akiufungua rasmi Mradi wa Maji Safi na Salama uliotekelezwa kwa nguvu za Wananchi wenyewe wa Kijiji cha Fujoni Wilaya ya Kaskazini “B” utakaokuwa na uwezo wa kuhudumia Zaidi ya Wananchi Mia Tatu.
Alisema Fedha za Mifuko ya Maendeleo ya Majimbo zinatotolewa na Serikali zote Mbili Tanzania kupitia Bunge la Jamuhuru ya Muungano wa Tanzania na Baraza la Wawakilishi Zanzibar ni msaada unaoongeza nguvu katika miradi iliyoanzishwa na Wananchi ambayo hukwama katika utekelezaji wake na sio kuanzishia Miradi mipya.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Mwakilishi anayemaliza muda wake wa Uwakilishi Jimbo la Mahonda alisema pale zinapojichomoza changamoto kwenye Miradi ya Kijamii si vyema Viongozi na Wananchi wenyewe wakajenga fikra za kuzisubiri Taasisi husika.
Alieleza kwamba itapendeza iwapo Wananchi na Viongozi husika wakaongeza jitihada kwa kutafuta mbinu za kupata ufumbuzi wa changamoto hizo jambo ambalo inakuwa rahisi kwa zile taasisi husika kuunga nguvu za pamoja katika kukamilisha Miradi husika.
Balozi Seif  aliwaomba Wananchi katika Majimbo yao kuwa tayari kuwapokea Wabunge, Wawakilishi na Madiwani Wapya watakaopewa jukumu la kuwatumikia wakati utakapowadia baada ya kumalilika kwa Uchaguzi Mkuu kipindi kifupi kijacho.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimshukuru na kumpongeza Mwananchi wa Kijiji cha Fujoni aliyejikubalisha kutumia Umeme wa Nyumba yake kuhudumia upandishaji wa Maji katika Matangi Matatu ya Kisima cha Mradi huo wa Kijiji cha Fujoni.
Mapema Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini “B” Nd. Rajab Ali Rajab alisema Viongozi wa  majimbo kwa kushirikiana na Wananchi mara kadhaa wamekuwa wakiwekeza katika miradi ya Kijamiii hasa ile ya Huduma za Maji na Afya kutokana na changamoto zinazoikumba Jamii katika maeneo yao.
Hata hivyo Nd. Rajab aliwashauri Wananchi pamoja na Kamati za Maendeleo za Majimbo, Wadi na Shehia kuzishirikisha Taasisi zinazohusika na Miradi wanayoianzisha ili kuepuka mapema matatizo yanayoweza kuviza maendeleo ya Miradi hiyo.
Mkuu huyo wa Wilaya ya Kaskazini “B” alimpongeza Balozi Seif Ali Iddi anayemaliza muda wake wa Uwakilishi katika Jimbo la Mahonda kwa kufanikiwa vyema Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi kwa Zaidi ya asilimia Mia Moja ndani ya kipindi chake cha Miaka Mitano.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa Kaskazini Unguja Nd. Iddi Ali Ame aliwatahadharisha Viongozi wanaopewa jukumu la kuwahudumia Wananchi waepuke sababu zisizo na msingi zinazoweza kupelekea kuwavunja moyo Wananchi wanaowasimamia.
Alisema Mwananchi wakati wote wa harakati zake za Kimaisha anahitaji kupata huduma za lazima na za msingi na pale  inapotokea tatizo ndani ya Miradi  inayoanzishwa lazima ushirikiano wa pamoja upewe nafasi ya kipekee.
Mwenyekiti huyo wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unaguja alionya kwamba Mbunge, Mwakilishi au Diwani ye yote atakayeshindwa  kusimamia jukumu lake alilokabidhiwa Chama hakitositra kumuwajibisha hata kabla ya kumalizika kwa kipindi chake cha Utumishi wa Miaka Mitano.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.