Habari za Punde

Dk.Hussein Mwinyi ni Kiongozi Mwenye Sifa Zote za Uongozi Ndani ya CCM na pamoja Kuwa Rais wa Zanzibar. -Dk. Shein.


Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akihutubia na kumtambulisha Mgombea Urais wa Zanzibar Mhe.Dk. Hussein Mwinyi, wakati wa Uzinduzi wa Kampeni za CCM Jijini Dodoma Uwanja wa Jamuhuri.

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa Dk. Hussein Ali Hassan Mwinyi ni kiongozi mwenye sifa zote za uongozi ndani ya CCM ikiwa ni pamoja na kuwa Rais wa Zanzibar.

Dk. Shein ameyasema hayo leo wakati akimtambulisha mgombea nafasi ya Rais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Dk. Hussein Ali Hassan Mwinyi katika uzinduzi wa Kampeni za Chama hicho zilizofanyika katika uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa chama hicho walioongozwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Rais Dk. John Pombe Magufuli.

Katika maelezo yake Rais Dk, Shein alisema kuwa Dk. Hussein Ali Hassan Mwinyi ana sifa zote za kuwa Rais wa Zanzibar na ndio maana akachaguliwa na Halmashauri Kuu ya Taifa tarehe 10, Julai mwaka huu ili CCM iendelee kuiongoza Zanzibar na yeye apeperushe bendera kwa tiketi ya chama hicho.

Alisema kuwa kuchaguliwa kwa Dk. Hussein Mwinyi kutalipelekea Dola la Tanzania liendelee kudumu, kuimarika kwa Muungano, umoja, usalama wa nchi pamoja na Mapinduzi ya Zanzibar.

Alisema kuwa Dk. Mwinyi ana uwezo mkubwa kwani ni msomi aliebobea kwani kwa fani yake ni daktari bingwa wa maradhi ya ndani ya mwanaadamu,  anaheshima kubwa na anaheshimika ndani na nje ya nchi na anatambulika kwa sifa zake binafsi kwani ndio sifa zilizokipelekea CCM imchague kugombea nafasi ya Urais kwa upande wa Zanzibar.

Alisema kuwa Dk. Mwinyi ni mzalendo halisi kwani kazi zote alizokabidhiwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amezifanya kwa ufanisi mkubwa, ikiwemo ya Naibu Waziri wa Afya, Waziri wa Afya, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Rais Mambo ya Muungano pamoja na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ambapo amefanya kwa miaka mingi nafasi ambayo bado anayo.

Alisema kua Dk. Mwinyi ataivusha Zanzibar ili CCM iibuke na ushindi na kuwaomba wanaCCM na wananchi kukumbuka kuendelea kuchagua viongozi wa CCM kwa Jamhuri ya Muungano akiwemo Rais Magufuli na Makamo wake Mama Samia Suluhu Hassan.

Hata hivyo alisisitiza haja ya kuwachagua Wabunge, Madiwani na Wawakilishi wa CCM na kuwataka kutowacha nafasi hata moja wazi na badala yake nafasi zote wapewe  viongozi wa CCM.

Akitoa salamu kwa watu wa Zanzibar, Rais Dk. Shein alisema kuwa wanasubiri kwa hamu wakamchague Dk. Hussein Ali Hassan Mwinyi kwa vishindo vikubwa sana na kueleza kuwa wanaCCM na wananchi wa Zanzibar watahakikisha Dk. Hussein anashinda kama alivyoshinda yeye katika chaguzi zilizopita.

Nae Dk. Hussein Mwinyi  alitoa salamu za wanaCCM wa Zanzibar ambao wameeleza kuwa wako tayari kuwachagua viongozi wote wa CCM wakiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamo wa Rais, Wabunge, Wawakilishi pamoja na Madiwani.

Alimpongeza Rais Dk. Shein kwa Utekelezaji Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa upande wa Zanzibar na kueleza kuwa hali hiyo itapelekea wagombea nafasi kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) watapita kirahisi.

Alisema kuwa atafanya kazi pale alipoishia Rais Dk. Shein juhudi kubwa katika kuimarisha sekta za maendeleo na uchumi zimefanyika chini ya Rais Shein na kusisitiza kua kwa upande wake ataendeleza kwa spidi na kasi kubwa.

Alisema kuwa kwa upande wa Tanzania Bara, Rais Magufuli amefanya mambo mengi katika kipindi chake cha miaka mitano ya mwanzo na iwapo atapewa miaka mitano mengine atafanya mambo makubwa zaidi.

Aliwataka wanaCCM kutobweteka na kusisitiza kuwa  siku ya uchaguzi ikifika basi waende kupiga kura na kuwachagua viongozi wote wa CCM waliwekwa katika maeneo yao na  kuahidi ushindi wa kishindo utapatikana.

Sambamba na hayo alisisitiza haja ya kulinda amani iliopo kwani bila ya amani hakuna maendeleo kwani alisema kuwa tayari kuna viashiria vilivyojitokeza ambavyo vinatokana na kauli za baadhi ya watu.

Aliwasisitiza wanaCCM na wananchi wasikubali kupelekwa katika jambo lolote litakalohatarisha amani ya nchi kwani hatua iliyofikiwa ya watu kufanya shughuli zao za maendeleo pamoja na ibada  ni kutokana na kuwepo kwa amani.

Aidha, alieleza kuwa amani ya nchi inaletwa na wananchi wake na kuwataka wananchi kuhakikisha amani inadumishwa huku akisema kuwa CCM itafanya vizuri zaidi mara hii kutokana na kutekelezwa vyema Ilani ya Uchaguzi kwa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.