Habari za Punde

Jamii Bado Inatakiwa Kuchukua Tahathari ya Kuendelea Kujikinga na Maambukizi ya Virusi Vya Corona.-Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Balozi Seif Ali Iddi akikabidhi Vifaa vya Kinga dhidi ya Virusi vya Corona kwa Skuli 12 zilizomo ndani ya Jimbo la Mahonda, akimkabidhi Afisa wa Elimu  wa Wilaya ya Kaskazini "B " Unguja Mwalimu Othman Ussi Mchano, hafla hiyo imefanyika katika Skuli ya Sekondari Kitope.
Na.Othman Khamis. OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Jamii bado inapaswa kuchukuwa tahadhari ya kuendelea kujikinga na maambukizi ya Virusi hatari vya Corona  vilivyoleta fadhaa ndani ya Jamii Kitaifa sambamba na Jumuiya ya Kimataifa.
Alisema Corona ilileta hofu, wasi wasi na simanzi Dunia nzima  hali iliyopelekea baadhi ya Mila na Taratibu za Wanaadamu kama vile kupeana mikono kuachwa kwa muda ili kuepuka maambukizi ya janga hilo thakili.
Balozi Seif Ali Iddi akiwa pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda anayemaliza Muda wake alisema hayo wakati wa hafla fupi ya kukabidhi Vifaa vya kinga dhidi ya Virusi vya Corona  kwa matumizi ya Walimu na Wanafunzi wa Skuli  12 zilizomo ndani ya Jimbo hilo hafla iliyofanyika katika Skuli ya Sekondari Kitope.     
Alieleza kwamba Jamii kuendelea kujikinga na Maambukizi ya Virusi vya Corona bado itakuwa ni suala la lazima katika kipindi hichi cha mpito kwa vile maradhi yanayotokana na Virusi hivyo yanaendelea kuitesa Dunia katika baadhi ya Mataifa zikiwemo Nchi za Bara la Afrika.
Hata hivyo Serikali ililazimika kupunguza masharti Kumi yaliyoainishwa kupunguza Maambukizi ya Vurusi hivyo baada ya jihitada kubwa iliyochukuliwa na Taifa kwa kushirikiana na Wananchi pamoja na Taasisi za Kitaifa na zile za Kimataifa.
“ Hatua za kunawa Mikono kwa maji ya kutiririka, vitakasa Mikono na uvaaji wa Maski katika maeneo ya msongamano ni vyema ikaendelea kuzingatiwa na kufanywa kama suala la kawaida katika Jamii”. Alisisitiza Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwashukuru na kuwapongeza Wananchi wote Nchini kwa usikivu wao uliopelekea kufuata maelekezo ya Serikali Kuu pamoja na Wataalamu wa Sekta ya Afya na hatimae Taifa kuendelea kubakia salama.
“ Tuna mfano wa Majirani wenzetu wa Mataifa ya Madagaska na Botswana waliofanikiwa kudhibiti kuendea kwa maambukizi ya Virusi vya Corona na kuamua kulegea vikwazo kwa hatua kubwa ambayo sasa inawagharimu kutokana na kasi kubwa ya kurejea upya kwa Maambukizi ya Virusi hivyo”. Alitanabahisha Balozi Seif.
Alisisitiza umuhimu wa Wanafunzi na Walimu Maskulini kuendelea kuvitumia Vifaa vya Kinga kutokana na maeneo yao makubwa kuendelea kuwa na msongamano mkubwa wa Watu.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaomba Wananchi hao kwa vile yeye anapumzika Utumishi wa Jimbo washirikiane na Viongozi wao wa Mahonda Mpya iliyokuja baada ya marekebisho ya Mipaka iliyofanywa hivi karibuni na Tume ya Uchaguzi Zanzibar {ZEC}.
Mapema Katibu Tawala wa Wilaya ya Kaskazini “B” Nd.  Makame Machano Haji kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo Nd. Rajab Ali Rajab alimshukuru Balozi Seif kwa kukamilisha ahadi alizotoa wakati wa Utumishi wake unaomalizika hivi karibuni.
Nd. Makame alisema Uongozi wa Wilaya hiyo tayari umeshajitolea kubeba dhima  ya kuhakikisha vifaa vyote vilivyotolewa na Viongozi wa Serikali na Jimbo kwa ajili ya kuwahudumia Wananchi vinasimamiwa kwa faida na maendeleo ya Wananchi wote.
Akitoa shukrani kwa niaba ya Walimu Wakuu wa Skuli zilizokabidhiwa Vifaa hivyo vya Kujikinga ya Virusi vya Corona Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Sekondari Kitope Mwalimu Simai Haji Hamad alisema wao kama wasimamizi wa Wanafunzi wa Skuli hizo wako tayari kuona vifaa walivyokabidhiwa vinatumika kwa lengo husika.
Mwalimu Simai alimuomba Mwakilishi huyo wa Jimbo la Mahonda anayemaliza muda wake wa Utumishi asiwe mbali nao kwa kuendelea kutoa ushauri wake pale atakapohitajika kufanya hivyo ili ile kiu ya Wananchi wa Jimbo la Mahonda Mpya ifikie kileleni.
Vifaa vilivyotolewa na Balozi Seif Ali Iddi vyenye thamani ya Shilingi Milioni 44,000,000/- ni pamoja na Sabuni, Ndoo, Vitakasa Mikono pamoja na vifaa vya kuhifadhia Pua na mdomo { Maski}
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Walimu Wakuu wa Skuli 12 ziliko  katika Jimbo la Mahonda waliofika Skuli ya Kitope kupokea Vifaa vya kinga dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Corona.
Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Sekondari ya Kitope Mwalimu  Simai Haji Hamad akitoa shukrani kwa niaba ya Walimu Wakuu wenzake kwenye hafla maalum ya kupokea Vifaa vya kinga dhidi ya Virusi vya Corona.
Baadhi  ya Waalimu Wakuu wa Skuli 12 zilizomo ndani ya Jimbo la Mahonda wakifuatilia nasaha za Mwakilishi wa Jimbo  la Mahonda Balozi Seif hayupo pichani kwenye makabidhiano ya Vifaa vya kinga dhidi ya Corona.
Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Sekondari ya Fujoni Mwalim Abdi akisoma dua mara baada ya kukamilika kwa hafla maalum ya kupokea Vifaa vya kinga dhidi ya Virusi vya Corona hapo Skuli ya Sekondari ya Kitope.
Picha na – OMPR – ZNZ.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.