Habari za Punde

Kuboronga kwa makusudi kwa waamuzi wa soka ni utashi wao

Na Mwandishi wetuMKUFUNZI wa waamuzi katika wilaya ya Mjini Unguja Ramadhan Ibada Kibo amesema kuboronga kwa makusudi waamuzi katika michezo kunatokana na utashi wao na hautokani na kamati inayosimamia waamuzi hao.


Hayo aliyasema katika kikao cha pamoja na viongozi wa kamati tendaji ya Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) Wilaya ya Mjini kilichofanyika hoteli ya Amaan mjini hapa.


Alisema kuwa yapo makosa ambayo yanafanywa na waamuzi yanatokana na tatizo la ubindamu lakini sio kama anafanya kwa makusudi.


Alisema kuwa kamati kazi yake kubwa ni kusimamia waamuzi juu ya kuwafundisha namna ya kutafsiri sheria kazi ambayo amekuwa akiifanya kila siku.


Hivyo alisema kuwa kama kunatokea mwamuzi kuharibu mpira wakati mwengine watakuwa wanafanya kwa utashi wao na sio ionekane kamati ndio inachangia kufanya hivyo.


“Kuna makosa ya kibindamu yanakuwa yanafanyika katika mchezo na tunayaona lakini sio mwamuzi kaharibu na kutupiwa lawama kamati kama haisimamii”, alisema.


Hata hivyo alisema kuwa kabla ya ligi haijasimama kulikuwa na changamoto nyingi ikiwemo kutimia kwa waamuzi kwenye michezo hasa ya daraja la tatu kulikochangiwa na waamuzi kutumiwa katika michezo mengine pasipo na kupeana taarifa.


Hivyo aliwaomba viongozi wa chama hicho kujitahidi kuwa na ushirikiano na vyama vyengine ambavyo vinawatumia waamuzi wao ili kuona changamoto hiyo haijitokezi katika ligi itakayoendelea.


Katika kikao hicho Mwenyekiti wa chama hicho Iddi Juma aliwaambia wajumbe wa kamati hiyo kuwa wamepokea malalamiko kutoka kwa klabu kuhusu waamuzi kuharibu na kuitaka kamati kuwa makini wakati ligi itakapoendelea.


Alisema kuwa klabu nyingi zinaonekana kutoa lawama kwa waamuzi hao ambao wengi wao wanadai kuwa huharibu mechi pasipo na kuchukuliwa hatua.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.