Habari za Punde

Mradi wa Ujenzi wa Nyumba ya Makaazi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Pagali Chake kukamilika ndani ya wmezi mmoja

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wa kwanza kutoka Kulia akipata maelezo ya kiufundi kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nyumba Mhandisi Ramadhan Mussa Bakari wa Pili kutoka Kulia aliyenyanyua mikono kuhusu maendeleo ya Mradi wa Ujenzi wa Nyumba ya Makaazi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Pemba.

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nyumba Mhandisi Ramadhan Mussa Bakari Kushoto akimthibitishia Balozi Seif  ukamilishaji wa Mradi wa Ujenzi wa Nyumba ya Makaazi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Pagali Chake ndani ya kipindi kisichozidi Mwezi Mmoja na Nusu.
Picha na – OMPR – ZNZ.


Na Othman Khamis, OMPR

Wahandisi wa Mamlaka ya Maji Zanzibar {ZAWA} wanaosimamia usambazaji wa huduma ya Maji safi na salama katika Mtaa Mpya wa Pagali pembezoni mwa Mji wa Chake Chake Pemba wameagizwa kuandika maombi ya upatikanaji wa vifaa vilivyopungua katika kazi yao ili kuona mradi huo unamalizika kwa wakati uliopangwa.
Agizo hilo limetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofanya ziara fupi ya kukagua maendeleo ya Mradi wa Ujenzi wa  Nyumba ya Makaazi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar hapo Pagali Chake Chake Pemba ambao uko katika hatua nzuri ya kuridhisha.
Balozi Seif alisema itapendeza kuona kwamba vifaa vinavyotumika katika Mradi huo vinakuwa katika kiwango cha ubora unaokubalika ambavyo vitadumu kwa kipindi kirefu kinachopelekea kupunguza gharama kubwa za matengenezo ya mara kwa mara.
Alisema ipo tabia mbaya na ya muda mrefu katika miradi mingi ya huduma za Maji safi na salama inayotumiwa na baadhi ya Wahandisi wanapopewa jukumu la kusimamia kazi huamua kununua vifaa vilivyo chini ya kiwango na matokeo yake miradi husika hufanya kazi muda mfupi na baadae kuleta usumbufu kwa Wananchi.
Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Majengo Zanzibar Mhandisi  Ramadhan Mussa Bakari alisema wajenzi wa Mradi huo kwa sasa wanasubiri kukamilika kwa zoezi la uwekaji wa miundombinu ya Bustani ili wakamilishe kazi ndogo ndogo zilizobakia ikiwemo upakaji wa rangi.
Mhandisi Ramadhan Mussa Bakar alimueleza Balozi Seif  kwamba matengenezo yaliyobakia katika kipindi hichi yanatarajiwa kukamilika ndani ya muda wa Mwezi Mmoja na makabidhiano ya Mradi kamili yanakisiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu au mwanzoni mwa Mwezi wa Septemba Mwaka huu.
Alisema kinachozingatiwa ni jinsi ya kuwapata washauri na Wataalamu wa masuala ya Miti na Bustani kutoka Taasisi ya Misitu pamoja na Manispaa ili bustani itakayooteshwa ilingane na hadhi ya nyumba za Viongozi Wakuu wa Serikali.
Mradi wa Ujenzi wa Nyumba ya Makaazi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mtaa wa Pagali Chake Chake Kisiwani Pemba ulianza Mnamo Mwezi Juni Mwaka 2018.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.