Habari za Punde

Mtandao wa Elimu Tanzania Kusaidia Ujenzi wa Bweni la Wanafunzi Wilayani Chemba Dodoma.

Mratibu wa Taifa wa TEN/MET, Bw. Ochola Wayoga (katikati) akizungumza leo na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusiana na Maadhimisho ya Juma la Elimu ya mwaka huu, 2020 katika ofisi za mtandao huo zilizopo Mikocheni jijini Dar es Salaam. Wa kwanza kulia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi wa Juma la Elimu Tanzania, Anna Sawaki na Ofisa Utetezi wa TEN/MET, Nasra Kibukila.

Na Joachim Mushi, Dar es Salaam

MTANDAO wa Elimu Tanzania (TEN/MET) imeadhimia kutumia maadhimisho ya Juma la Elimu mwaka huu kujenga Bweni la wanafunzi Wilayani Chemba kusaidia wanafunzi toka familia za wafugaji na jamii nyingine eneo hilo.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Mratibu wa Taifa wa TEN/MET, Bw. Ochola Wayoga amesema bweni hilo lenye uwezo wa kubeba wastani wa wanafunzi 50 hadi 100 litajengwa katika Shule ya Sekondari Kwamtoro iliyopo Wilaya ya Chemba jijini Dodoma.

Akifafanua zaidi Bw. Wayoga amesema Bweni hilo linajengwa kwa ushirikiano wa wadau wa TEN/MET na jamii kwa utaratimu wa kuchangia gharama zake hadi kukamilika ili kuwasaidia jamii hiyo ya wafugaji dhidi ya changamoto ya miundombinu ya shule.

"Tunatoa wito kwa wadau mbalimbali wenye nia njema wapenda elimu kuungana nasi na Serikali ya Wilaya ya Chemba katika ujenzi wa bweni la wanafunzi ili kuongeza ulinzi kwa watoto na kuboresha mazingira ya kujifunzia. Ili kufanikisha tuma mchango wako kwa namba; 0743 001393," alisema Mratibu Wayoga.

Aidha alisema maadhimisho ya mwaka huu ambayo yamepangwa kufanyika kitaifa Wilayani Chemba, yamelenga kuhamasisha uelewa wa jamii juu ya haki ya kupata elimu, kuongeza uhamasishaji kwa jamii juu ya uwajibikaji wa pamoja wa elimu na kuhamasisha Serikali kuzingatia na watoto wenye uhitaji, ikiwemo miundombinu ya shule, vifaa vya mafunzo na mafunzo ya ualimu.

Amebainisha kuwa kutokana na uhitaji mkubwa wa masuala mbalimbali ya elimu, Serikali haipaswi kuachiwa kila kitu hivyo wadau awadabudi kujitokeza na kushiriki kichangia masuala anuai kusaidia kutatua baadhi ya changamoto kwenye sekta nzima ya elimu.

Pamoja na hayo, Bw. Wayoga ameeleza kuanzia Agosti 17 mwanzo wa maadhimisho ya juma hilo hadi Agosti 21 kutakuwa na mijadala mbalimbali, midahalo, ushiriki katika utoaji wa elimu kupitia vyombo vya habari juu ya masuala anuai ya elimu na changamoto zake kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.