Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Uongozi wa Wizara ya Biashara na Viwanda Zanzibar, katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya
Saba imepata mafanikio makubwa katika kuendeleza na kuimarisha sekta ya viwanda
na biashara hapa nchini.
Hayo aliyasema leo, Ikulu mjini Zanzibar
alipokutana na uongozi wa Wizara ya Biashara na Viwanda wakati ilipowasilisha
utekelezaji wa Mpango Kazi wa Mwaka 2019/2020, na Mpango Kazi wa mwaka 2020/2021.
Rais Dk. Shein alisema kuwa katika kipindi hicho
juhudi kubwa zimefanywa katika kuimarisha Sheria, Sera na miongozo mbali mbali
sambamba na kuimarisha miundombinu muhimu kwa ukuaji wa sekta ya biashara na
viwanda.
Aidha, Rais Dk. Shein alisisitiza kwamba misingi
hiyo iliyojengwa ni vyema ikaendelezwa ili Serikali ijayo ya Awamu ya Nane
iweze kuanza utekelezaji wa mipango yake kwa kasi zaidi.
Rais Dk. Shein alisema kuwa Wizara hiyo imepata
mafanikio makubwa hasa katika kipindi hichi cha miaka mitano chini ya uongozi
wa Waziri wa Wizara hiyo hivi sasa Balozi Amina Salum Ali.
Alisema kuwa misingi ya biashara iliyoanzishwa
imesaidia sana kukua na kuimarika kwa biashara huria Zanzibar sambama na
kuvifufua na kuviendeleza viwanda mbali mbali kikiwemo kiwanda cha Sukari,
Mahonda pamoja na ongezeko la uzalishaji wa bidhaa mbali mbali ambazo umesaidia
upatikaji wa huduma na usalama wa chakula.
Pia, aliwasifu wawekezaji wa ndani kwa kujenga
ujasiri wa kuekeza katika maeneo mapya ya biashara ndani na nje ya nchi katika
sekta mbali mbali.
Katika maelezo yake, Rais Dk. Shein alipongeza
hatua zilizochukuliwa na Wizara hiyo za kuimarisha na kuanzisha viwanda hapa
Zanzibar huku akipongeza mashirikiano yaliopo ambayo yamepelekea kupata
mafanikio hayo.
Rais Dk. Shein alieleza matumaini yake makubwa ya
kuwa zao la karafuu litaendelea kuimarika pamoja na bei yake ili nchi pamoja na
wananchi wake waendelee kupata tija na mafanikio zaidi.
Rais Dk. Shein alitoa pongezi kwa uongozi wa
Wizara hiyo kwa kutimiza vyema wajibu wao na kuitumikia ipasavyo Serikali yao
na kueleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepata mafanikio makubwa na
hivi sasa tayari imeshaingia katika nchi zenye uchumi wa kati kwani ina nguvu
za kiuchumi.
Akizungumzia vikao vya kutathmini utekelezaji wa
mpango kazi ambavyo vimekuwa vikifanyika katika kipindi chote cha uongozi wake,
Rais Dk. Shein alisema kuwa vikao hivyo (bango kitita) ambavyo ni vya mwisho
katika muda wa uongozi wake, vimemsaidia kwa kiasi kikubwa kufuatilia
utekelezaji wa mipango ya Serikali katika Wizara zake.
Nae Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee aliupongeza uwasilishwaji Mpango Kazi huo
iliyofanywa na Wizara hiyo na kusema kuwa miaka mitano ya uongozi wa Balozi
Amina Salum Ali Wizara hiyo imekuwa na mabadiliko makubwa.
Alisema kuwa mikutano hiyo ya (Bango Kitita) imekuwa
na msaada mkubwa katika Wizara za Serikali na kueleza haja ya kuendelezwa huku
akisisitiza haja kwa viongozi na wafanyakazi wa Wizara hiyo kuendelea kuchapa
kazi hasa katika kipindi hichi cha kuelekea uchaguzi mkuu ujao wa mwezi Oktoba
mwaka huu.
Mapema Waziri wa Biashara na Viwanda Balozi Amina
Salum Ali alieleza kuwa Wizara katika mwaka 2020/2021 inatarajia kuyaendeleza
na kuyapima maeneo ya viwanda ambapo Wizara hiyo inaandaa Mpango wa matumizi na
upembuzi yakinifu kwa eneo la Dunga.
Aidha, alisema kuwa Wizara inakusudia kuliandaa eneo
la Nyamanzi na kuandaa Matamasha mbalimbali ambapo Wizara inakusudia kuliandaa
kwa ajili ya ubia eneo hilo kwa hatua za awali kufanya tathmini ya kimazingira
na kijamii (ESIA) pamoja na kulisafisha.
Kwa upande wa Shirika la Taifa la Biashara (ZSTC),
Shirika hilo limefanikiwa kuzindua mtambo mpya wa uzalishaji wa mafuta ya
Mikaratusi katika kiwanda cha mafuta ya
Makonyo na Arki za mimea huko Wawi Pemba.
Alisema kuwa Wizara kupitia Shirika hilo la (ZSTC)
inatarajia kuanzisha kiwanda cha kusarifu mwani katika eneo la Chamanangwe
Pemba kwa kushirikiana na wawekezaji kutoka Indonesia.
Nao uongozi wa Wizara hiyo ulimpongeza Rais Dk.
Shein kwa uongozi wake bora uliotukuka ambao umewawezesha kufanya kazi zao kwa
ufanisi mkubwa kutokana na busara, hekima na maelekezo mazuri waliyoyapata
kutoka kwa Rais Dk. Shein sambamba na kuimarika kwa sekta ya biashara na
viwanda.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment