Habari za Punde

VIJANA JIJINI TANGA WAIOMBA SERIKALI KUWAWEZESHA KUPATA AJIRA

Na Hamida Kamchalla, TANGA.
VIJANA wa Jiji la Tanga wameiomba serikali mkoani hapa kuwawezesha katika upatikanaji wa ajira ikiwa ni pamoja na kujiajiri wenyewe kwa lengo la kujikwamua kiuchumi na kuondokana na fikra za kujiingiza katika makundi yasiyofaa.

Rai hiyo imetolewa jana na vijana hao wakati wa maadhimisho ya siku ya vijana duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Tangamano ambapo vijana kutoka maeneo mbalimbali walihudhuria na kushiriki katika michezo mbalimbali.

Vijana hao walisema kuwa changamoto kubwa kwao ni ajira jambo ambalo wamekuwa wakilipigania kwa juhudi kubwa huku wakitafuta fursa mbalimbali kwa wadau wa maendeleo ikiwa ni pamoja na kuchukua mikopo katika Taasisi mbalimbali jijini hapa ili kujiendeleza kimaisha na kuondokana na hali ya kuwa tegemezi.

"Bado vijana tuna changamoto katika kujitafutia ajira, hatuna fursa za mafunzo katika biashara zetu tunazofanya baada ya kuchukua mikopo na vilevile kuna tatizo la riba kuwa kubwa kwa taasisi za mikopo hivyo kufanya vijana wengi kushindwa kuendesha biashara zao" alisema Asha Ngonyani, mwanafunzi wa Chuo cha Utalii Maasai.

Ngonyani aliongeza kuwa endapo changamoto zinazowakabili zikikosa utatuzi kuna hatari ya vijana wengi jijini hapa kujiingiza katika vitendo vibaya na kuishia katika unywaji pombe na ufugaji madawa ya kulevya pamoja na vijana wa kike kuishia kubeba mimba wasizozitarajia na hatimaye kukatisha ndoto zao.

Kwa upande wake Proches Milambo alisema kuwa pamoja na changamoto ya ukosefu wa ajira waliyonayo vijana hao wameendelea kutumia fursa mbalimbali zilizopo ndani ya Jiji na kuzifanyia kazi ili kupambana na umasikini ili kujiletea kipato.

Hata hivyo alibainisha kwamba pamoja na kupambana na hali hiyo bado wanapata nafasi kutoka halmshauri kwa kupatiwa mikopo wa vijana wa asilimia 4 huku halmashauri hiyo ikipambana kutafuta wadau mbalimbali wa maendeleo na kuhakikisha wanawashirikisha vijana katika kupatiwa mikopo ya nje.

"Pamoja na vijana kupambana na fursa zilizopo ndani ya Jiji kujiletea maendeleo pia tunamshukuru mkurugenzi wetu wa halmashauri kuendelea kutafuta wadau mbalimbali wa maendeleo na kupata fursa mbalimbali kwa vijana ili kupambana na changamoto tulizonazo" alieleza Milambo.

Katika maadhimisho hayo mgeni rasmi alikuwa mkuu wa Wilaya ya Tanga, Thobiasi Mwilapwa ambaye aliwataka vijana hao kutumia fursa mbalimbali zinazotolewa ndani ya jiji kwa kufanya malengo yaliyokusudiwa ili kujiletea tija katika kujikwamua kiuchumi na kusaidia kujenga Taifa lenye nguvu na bora.

"Nitafurahi sana baada ya shuhuli ya siku ya leo vijana wengi wanaenda kutekeleza yale mliyojifunza hapa, hii siyo sherehe tuu bali ni sherehe na mafunzo pia, nendeni mkapambane mlete mabadiliko na muendelee mbele kuliko mlivyokuwa awali" alisema Mwilapwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.