Habari za Punde

Balozi Seif Ali Iddi Atembelea Mradi wa Ujenzi Mtaro wa Maji Machafu Mfenesini

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi  wa kwanza kutoka Kulia ajionyesha kupata faraja kutokana na jitihada za Wahandisi za kulitafutia ufumbuzi wa tatizo la kutapakaa kwa maji ya Mvua katika eneo la Makaazi ya Wananchi Mfenesini Meli Kumi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Balozi Seif Ali Iddi akimsikiliza Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar Nd. Mustafa Aboud Jumbe akimuonyesha Mchoro wa Ujenzi wa Msingi wa kupitishia Maji ya Mvua katika eneo la Mfenesini Meli Kumi Wilaya ya Magharibibi "A " Unguja leo
Balozi Seif Ali Iddi akiwakumbusha Wahandisi wanaopewa miradi ya Ujenzi kuhakikisha wazingatia ubora wa Miundombinu wanayoisimamia ili kuepuka hasara hapo Mfenesini Meli Kumi alipofanya ziara fupi.
Msingi wa kupitisha Maji ya Mvua unaojengwa katika eneo la Mfenesini Meli Kumi utakaosaidia kupunguza marufiko ya maji ya mavua hasa kipindi cha msimu wa masika.
Na.Othman Khamis.OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewakumbusha Wahandisi wanaopewa miradi ya Ujenzi kuhakikisha wazingatia ubora wa Miundombinu wanayoisimamia ili kuepuka hasara au maafa wakati wa matumizi wa miradi husika.
Balozi Seif  Ali Iddi alitoa kumbusho hilo wakati akizungumza na Uongozi wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji pamoja na Wahandisi wa ujenzi wa msingi wa kupitishia Maji ya Mvua katika eneo la Mfenesini Meli Kumi  alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya Ujenzi wa Mradi huo.
Alisema ipo miradi tofauti inayoanzishwa kwa nia ya kuwaondoshea shida na usumbufu Wananchi lakini matokeo yake ndani ya muda mfupi baadhi ya miradi  huleta athari na kutokidhi mahitaji halisi kutokana na kukosa kiwango kinachokusudiwa kitaalamu.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaomba Wahandisi wa Ujenzi wa Mradi huo kujitahidi kutafuta mbinu za ziada katika kuona changamoto inayowakabili Wananchi wa eneo hilo ya kufurika kwa Maji ya Mvua hasa wakati wa msimu wa Masika inaondoka au kupungu.
Alisema Mfenesini ni miongoni mwa maeneo yanayokumbwa na mafuriko ya maji ya mvua za masika na hali hiyo imeongezeka mara dufu Mwaka huu kufuatia Mradi wa ujenzi mkubwa wa Bara bara ya Bububu hadi Mkokotoni.
Balozi Seif aliwapongeza Wahandisi wa Wizara ya Ujenzi na wale wa Kampuni za Kimataifa kwa jitihada kubwa wanazoendelea kuzichukuwa za kuimarisha miundombinu ya Ujenzi wa Miradi mbali mbali ya Kiaifa ambayo imesaidia kuleta Ukombozi na Ustawi wa Jamii.
Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar Nd. Mustafa Aboud Jumbe alisema Msingi huo wenye urefu wa Mita Mia 425 unatarajiwa kumwaga maji ya mvua katika eneo la bondeni.
Alisema wahandisi wamelazimika kubadilisha mfumo wa Bomba ili kutoa fursa ya mtiririko wa kasi ya maji ya Mvua sambamba na unyanyuliwaji wa Bara  bara kwa lengo la kuepuka kutuama kwa mchanga kunakosababisha Maji kuanza kusambaa   maeneo ya Mitaani.
Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji alibainisha kwamba Maji ni adui mkubwa wa Bara bara. Hivyo lazima uwepo utaratibu muwafaka wa kuhakikisha yanapatia njia ya kupita bila ya kuathiri upande wowote ule.
Eneo la Mfenesini Meli Kumi limekuwa na changamoto ya kufurika kwa maji ya mvua za Masika na Mwaka huu familia zaidi zililazimika kuyahama na kuyaacha makaazi yao kutokana na ongezeko kubwa la mvua hizo zilizoleta athari kubwa ya mali zao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.