Habari za Punde

Matukio ya Ajali ya Moto Gari la Kubeba Mafuta Yaendelea Kutikisha Barabarani.

Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wakiwa kwenye jitihada za kupambana na moto wa gari la kubebea Mafuta eneo la Kiegea Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro mapema tarehe 20, Septemba 2020. (Picha na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji) 

Na Mwandishi Wetu

Kumekuwa na muendelezo wa matukio ya ajali za magari ya kubebea Mafuta kuwaka moto na kulipuka yawapo barabarani yakisafirisha Mafuta na kuleta madhara kwa binadamu, uharibifu wa miundombinu na mali zipakiwazo katika magari hayo.

 

Mapema tarehe 20 Septemba, 2020 gari lenye namba za usajili T862 BZS lenye tela namba T814 DBZ lilishika moto eneo la Kiegea Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro likiwa njiani kuelekea Bujumbura Burundi kutokea Jijini Dar es Salaam.

 

Gari hilo mali ya kampuni ya INTERPETROL likiwa na Mafuta ya Dizeli na likiendeshwa na dereva aliyejitambulisha kwa jina la Hamidu Issa raia wa nchi jirani ya Burundi alisema hajui chanzo cha moto huo.

 

Kwa upande wake Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACF) Goodluck Zelote alisema, moto huo walifanikiwa kuudhibiti na kuokoa kiasi kikubwa cha Mafuta yaliyokuwemo na haukuleta madhara yoyote kwa binadamu, chanzo cha moto huo hakijajulikana.

 

Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linatoa rai kwa wananchi kutoa taarifa ya moto na majanga mengine kwa haraka zaidi kwa kupiga namba ya dharura 114. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.