Habari za Punde

Rais wa Zanzibare na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein Azungumza na Balozi Mdogo wa Jamhuri ya Watu wa China Anayefania Kazi Zanzibar Mhe Xie Xiaowu.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein akidsalimiana na Balozi Mdogo wa Jamhuri ya Watu wa China anayefanyika Kazi zake Zanzibar Mhe Xie Xiaowu alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo na kuaga baada ya kumaliza muda wake wa Kazi,mazungumzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar. 

JAMHURI ya Watu wa China imepongezwa kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta za maendeleo hatua inayotokana na juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuwaletea maendeleo wananchi wake.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ametoa pongezi hizo Ikulu Jijini Zanzibar  wakati alipofanya mazungumzo na Balozi Mdogo wa Jamhuri ya Watu wa China anayefanya kazi zake hapa Zanzibar Xie Xiaowu aliyefika Ikulu kwa ajili ya kuaga baada ya kumaliza muda wake wa kazi hapa nchini.

Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein alieleza kuwa ni miaka 56 hivi sasa tokea Jamhuri  ya Watu wa China ianze kuiunga mkono Zanzibar  katika sekta mbali mbali za maendeleo pamoja na kuimarisha uhusiano na ushirikiano mara tu baada ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964.

Rais Dk. Shein alisema kuwa Jamhuri ya Watu wa China ina historia ya muda mrefu katika kushirikiana na Zanzibar  ambapo nchi hiyo imeweza kusaidia miradi kadhaa ikiwemo katika sekta ya afya, elimu, miundombinu, habari, kilimo, utamaduni, michezo,  viwanda na mengineyo.

Aidha, Rais Dk. Shein alieleza kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar ina furahishwa na juhudi za nchi hiyo za kuendeleza uhusiano na ushirikiano wake huo ambao umepelekea kuendeleza na kuimarisha sekta za maendeleo na kukuza udugu wa kihistoria.

Rais Dk. Shein, alitumia fursa hiyo kuipongeza China kupitia kiongozi wake Rais Xi Jinping ambaye ametekeleza ahadi zake kwa asilimia 90 kati ya zile alizomuahidi Dk. Shein wakati wa ziara yake mwaka 2013 nchini China aliyoifanya  kufuatia mwaliko wa kiongozi huyo.

Rais Dk. Shein alisema kuwa miradi mbali mbali imeweza kufanikiwa katika utekelezaji wa ahadi hizo alizozitoa kiongozi huyo ikiwemo ujenzi wa Hospitali ya Abdalla Mzee Pemba, ujenzi wa uwanja wa Mao Tse Dung na mengineyo.

Mazungumzo hayo pia yaligusia maendeleo na mafanikio yaliofikiwa katika ujenzi wa jengo jipya la uwanja wa ndege wa Abeid Amani Karume ambalo linatarajiwa kuzinduliwa Septemba 28 mwaka huu 2020, ambapo Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuipongeza Jamhuri ya Watu wa wa China kwa kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika ujenzi huo.

Kufuatia mafanikio hayo, Rais Dk. Shein alieleza haja kwa Jamhuri ya Watu wa China kupitia Shirika lake la ndege kufanya safari za moja kwa moja hadi Zanzibar kwani tayari mashirika kadhaa ya ndege yanafanya safari zake hapa Zanzibar na mengineyo yanatarajia kuanza mara tu baada ya kuzinduliwa uwanja huo.

Rais Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa kukamilika kwa ujenzi huo na kufunguliwa kwa jengo hilo kutaimarisha zaidi uchumi na maendeleo ya Zanzibar kwani kutafungua milango mbali mbali ya uchumi kama vile watalii sambamba na kuongezeka kwa soko la ajira. Rais Dk. Shein alimpongeza Balozi huyo kwa juhudi zake binafsi katika kuhakikisha miradi kadhaa ambayo Jamhuri ya Watu wa China inasaidia Zanzibar.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Shein pia, alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara kutoka China kuja kuekeza Zanzibar katika sekta ya uvuvi huku akiwapongeza waekezaji ambao wameshaonesha nia ya kuja kuekeza  hapa Zanzibar. Dk. Shein alieleza kuwa rafiki wa kweli ni yule anaekujali wakati wa shida ambapo Jamhuri ya Watu wa China ilikuwa ya mwanzo kuisadia Zanzibar katika kupambana na janga la COVID 19.

Pia, Rais Dk. Shein alieleza juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha uchumi wake huku akimueleza Balozi huyo kuwa Zanzibar itafuata nyayo za nchi hiyo katika kujiletea maendeleo sambamba na kukuza uchumi wake kwani tayari viashiria vimeshaonesha kuwa Zanzibar inakwenda kupaa kiuchumi.

Nae  Balozi mdogo wa China Xie Xiaowu alimueleza Rais Dk. Shein kuwa Jamhuri ya Watu wa China inathamini uhusiano na ushirikiano uliopo kati yake na Zanzibar na kuahidi kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuendeleza na kuimarisha sekta za maendeleo ikiwemo afya, elimu, miundombinu, kilimo, viwanda na sekta nyenginezo.

Balozi huyo anayemaliza muda wake wa kazi hapa Zanzibar alitoa pongezi za pekee kwa Rais Dk. Shein kwa uongozi wake uliotukuka ambao umeipelekea Zanzibar kuimarika kiuchumi sambamba na kuendelea kuiweka katika hali ya amani, utulivu na mshikamano mkubwa.

Katika maelezo yake, Balozi Xie Xiaowu alitumia fursa hiyo kuwapongeza viongozi wote wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na wananchi kwa kumpa mashirikiano makubwa katika utekelezaji wake wa kazi na kuahidi kuwa nchi yake itaendeleza uhusiano uliopo.

Balozi huyo  alimueleza Rais Dk. Shein kuwa miradi yote iliyokuwemo katika makubaliano kati ya Zanzibar na nchi yake itatekelezwa hatua kwa hatua huku akieleza kuwa baadhi yake ilikawia kukamilika kutokana na kutokea kwa janga la COVID 19.

Hata hivyo, Balozi huyo alitoa  pongezi kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kukamilisha ujenzi wa jengo jipya la uwanja wa Zanzibar na kueleza kuwa ahadi ya nchi yake ya kuunga mkono juhudi hizo zipo pale pale.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein akizungumza na Balozi Mdogo wa Jamhuri ya Watu wa China  anayefanyia Kazi Zanzibar Mhe. Xie Xiaowu alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo na kuaga baada ya kumaliza muda wake wa Kazi Zanzibar hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein akiwa na mgeni wake Balozi Mdogo wa Jamhuri ya Watu wa China anayefanyika kazi zake Zanzibar, wakitoka katika ukumbi baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliofanyika Ikulu Zanzibar.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.