Habari za Punde

Sekta Binafsi Kuendelea Kushirikiana na Serikali Katika Kukuza Sekta ya Biashara.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akihutubia katika wa Ufunguzi wa jengo jipya ka maduka ya kisasa la Thabit Kombo Kisonge Michezaji Jijini Zanzibar ,wakati wa hafla hiyo iliofanyika katika viwanja vya Mapinduzi Square Michezani na (kulia kwa Rais) Mgombea Urais wa Zabzibar kwa Tiketi ya CCM Mhe.Dk. Hussein Mwinyi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dkt. Abdulhamid Yahya Mzee.
 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein ametoa wito kwa sekta binafsi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kukuza sekta ya biashara, ambayo hivi sasa inaendeshwa kupitia sekta hiyo (binafsi).

Dk. Shein ametowa wito huo katika hafla ya ufunguzi wa Jengo la Sheikh Thabit Kombo (Thabit Kombo Building), lililojengwa kwa ushirikiano kati  Chama cha Mapinduzi Zanzibar (CCM) na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF).

Amesema katika kufanikisha dhamira hiyo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuimarisha mazingira ya kuendesha shughuli za kibiashara pamoja na kukuza Uwekezaji.

Aliwataka wananachi kufanya kazi kwa bidii na kujiamini, kwa kuelewa kuwa mafanikio yataweza kupatikana kupitia wananchi wenyewe.

Alisema Ilani ya CCM ya Uchaguzi mkuu wa 2015 – 2020 pamoja na Ilani mpya ya 2020- 2025 zimesisitiza na kutilia maanani suala la uimarishaji wa sekta ya Utalii, biashara na Usafirishaji, masuala ambayo yameshughulikiwa kwa jitihada kubwa na kupata mafanikio katika utekelezaji wa Ilani iliyopita.

Aidha, Rais Dk. Shein alisema amefarijika kuona ufunguzi wa maduka katika eneo la Michenzani na kuunasibisha ujenzi wa jengo hilo na dhana iliyoelezwa na Mwekezaji wa Kimarekani Tom Freston, inayosema ‘ubunifu ni kuchukua vitu viwili vilivyopo na kuviweka pamoja kwa njia mpya’.

Alisema ZSSF imefanikiwa kutumia ardhi ndogo ya mahala hapo iliyokuwa ikitumika kwa shughuli tofauti , ikiwemo biashara na kujenga jengo moja kubwa la ghorofa linalopendeza ambalo ndani yake kuna maduka ya kisasa ya biashara.

Alisema hatua hiyo pia imeipatia maskani Kaka ya Kisonge sehemu za Ofisi zenye haiba, akibainisha kuwa huo ni ubunifu unaolingana na wakati.

Alisema ni veyma masuala ya maendeleo yakazingatia wakati ili kufikia mafanikio na kuwanasihi wananchi wanaopata fursa katika nyanja za Uwekezaji (ikiwemo ujenzi) kuwa tayari kutoa maeneo yao ili waweze kufaidika na vitu vizuri na vilivyo bora, ikiwemo rasilimali za majengo, sambamba na kuwaasa kuacha kukataa mambo mapya yenye tija.

Aliwataka wananchi na wanachama wa CCM kuielewa na kuiunga mkono kwa uzalendo mkubwa dhamira ya chama hicho katika kuleta maendeleo kwa wananchi wake.

Alisema Serikali inalenga kuendelea kuliimarisha eneo la Michenzani kibiashara kwa kujenga eneo la kuegesha magari (parking) na hivyo kuongeza idadi ya wafanyabiashara, hatua itakayotoa majibu sahihi dhidi ya wale wote waliokuwa wakidhihaki azma ya ujenzi huo.

Aidha, aliwakumbusha viongozi na watendaji wa serikali kutumia vyema busara badala ya nguvu, akinasibisha kauli hiyo na busara zilizotumiwa na serikali katika kuielekeza ZSSF kuwekeza katika miradi mbali mbali ya maendeleo, jambo ambalo kabla lilikuwa gumu kufanyika.

Alisisitiza umuhimu wa kudumisha na kuimarisha usafi , akibainisha gharama kubwa zinazotumika katika ujenzi wa majengo ya namna hiyo pamoja na kuweka usafi katika maeneo mbali mbali ya mji, ikiwa ni hatua ya utekelezaji wa sheria ya Zanzibar kuwa jiji.

“Lazima jengo hili na lijalo tulitunze, ili liendelee kudumu kwa miaka mingi ijayo”, alisema.

Dk. Shein alieleza kuwa Serikali ina mipango madhubuti ya kubadili ng’ambo ya mji, na kufafanua kuwa mpango huo umeanza kutekelezwa kwa ujenzi wa nyumba ambpo hatimae zitaunganika na eneo la Michenzani, sambamba na ujenzi katika maeneo miji mbali mbali Unguja na Pemba.

Akigusia historia ya eneo la Michenzani, Dk. Shein alisema kabla ya Mapinduzi ya Zanzibar  1964, ilikuwa ni sehemu iliyohusisha shughuli mbali mbali, ikiwemo burudani za klabu mbali mbali za Dansi, mojawapo ni ‘African Dancing Club’.

Aidha, alinukuu kauli ya Marehemu mzee Abeid Amani Karume, inayoelezea uzuri wa mji kuwa ni majengo yenye kupendeza na kuinasibisha hali hiyo na ukuaji wa miji katika nchi za Dubai na Singapore, ambazo zimekuwa na majengo marefu (sky scrapers) na yenye haiba kubwa.

Katika hatua nyengine,  Dk. Shein aliwashukuru wafanyabiashara na wawekezaji kwa kulipa kodi zao kwa wakati na kusema ndizo zinazofanikisha utekelezaji wa miradi mbali mbali ya maendeleo.

Aliwataka wadau hao pamoja na wale wenye mamlaka ya kukusanya kodi nchini kutimiza vyema wajibu wao ili kufanikisha malengo ya serikali.

Alisema kukamilika kwa mradi huo ni kielelezo cha ushirikiano na mshikamano kuelekea kazi ya kuijenga Zanzibar pamoja na CCM kuongoza nchi kwa mafanikio.

Aidha, alisema hatua hiyo ni uendelezaji wa historia ya Zanzibar kiuchumi na kijamii inayofahamisha wapi ilikotoka na hatua mbali mbali ilizopita hadi kupatikana mafanikio makubwa ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa jengo hilo.

Akielezea sababu za jengo hilo kuitwa jina la Sheikh Thabit Kombo, Dk. Shein alisema inatokana na mchango mkubwa alioutowa  kiongozi huyo katika siasa za ASP na CCM, ikiwemo kuwaunganisha Wazanzibari pamoja na kuzaliwa kwa CCM.

Vile vile, Dk. Shein alirudia kauli yake ya kuvitaka vyama vya siasa na wananchi kuendelea kufanya kampeni zao kwa njia za kistaarabu, pamoja na kujenga imani na Tume ya Uchaguzi, akibainisha hatua hiyo ni kuiunga mkono serikali kwani ndio inayojenga amani.

Aliwataka Wazanzibar kuwa watulivu kwa kigezo kuwa ndio njia pekee ya kupata viongozi bora pamoja na kusema serikali haitakuwa tayari kuona kunatokea vurugu, akibainisha watu mbali mbali duniani wanaipenda Zanzibar kutokana na utulivu na amani iliopo.

Alisema Uchaguzi ni tukio linalodumu kwa muda mfupi sana na kueleza kuwepo kwa maisha ya baada ya zoezi hilo, hivyo akasisitiza umuhimu wa  kudumisha amani nchini.

Mapema, Waziri wa Fedha na Mipango, Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa alisema wajibu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (ZSSF) hauko kwa wanachama wake pekee, bali ni kwa jamii yote ya Wazanzibar.

Alisema  hatua ya ZSSF kuingia ubia na CCM ni jambo zuri kwa kuzingatia CCM ni chama chenye nguvu na kinachoaminika muda wote, sambamba na  kufanya mambo yenye manufaa kwa wananchi wake.

Nae, Makamo Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini wa CCM, Pandu Ameir Kificho, akitoa salamu za ushirikiano wa ujenzi huo, alisema jengo hilo ni sehemu ya mradi wa CCM na kusema moja kati ya majukumu ya Baraza hilo ni kusimamia miradi iliopo na miradi  mipya inayoibuliwa kwa lengo la kukiongezea mapato na kuondokana na utegemezi wa ruzuku toka serikalini.

Alisema suala la kujitegemea ni kipaumbele cha CCM kwani kinakipa uwezo chama hicho kuweza kufanya shughuli zake bila utegemezi wowote.

Alisema ni lazima CCM tutafute mbinu mbali mbali ili kuendeleza miradi mikubwa kama hiyo na kusema Baraza la wadhamini wa CCM limeridhishwa  an ujenzi huo kuwa umekamilika kwa kiwango cha juu na hivyo kumpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, kwa fikra za kufanyika mradi huo wa ushirikiano.

Alisema kukamilika kwa jengo hilo, kunaifanya Maskani kaaka ya Kisonge kuwa ndio yenye jengo zuri zaidi Tanzania, na kubainisha kuwa ujenzi huo ni chachu kwa mgombe wa Urasi kupitia tiketi ya  CCM Dk. Ali Hussein Mwinyi kuibuka na ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu baaade mwaka huu.

Aidha, akitoa taarifa ya ujenzi wa Jengo hilo, Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango Khamis Mussa alisema ujenzi wa jengo hilo la ghorofa tano katika eneo la Muembe Kisonge, unaohusisha maduka 48, Ofisi pamoja na maskani ya Kisonge yenye vyumba 13 na Ukumbi wa mikutano, umefanywa na Kampuni ya Group Six International kwa gharama ya shilingi Bilioni tisa hadi kukamilika kwake.

Alisema kukamilika kwake kunaashiria utekelezaji wa ahadi ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein baada ya maskani hiyo kuhujumiwa kwa kutiwa moto Oktoba 18, 2012.

Nae, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Dk. Abdalla Juma Sadalla ‘Mabodi’ alimpongeza Rais Dk. Shein kwa msimamo wa dhati na kuibuwa rai ya ujenzi huo na kuisimamia.

Hafla ya ufunguzi wa jingo hilo umehudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Serikali, akiwemo makamo wa Pili wa Rais na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Balozi Seif Ali Idd na Mgombea wa Kiti cha Urais kupitia CCM Dk. Hussein Ali Mwinyi.

Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 

 E-mail: abdya062@gmail.com

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.