Habari za Punde

TAMWA Zanzibar Watoa Elimu kwa Wanamtandao Kupiga Vita Vitendo vya Udhalilishaji

Mwanamtandao wa kupinga Udhalilishaji Bi.Asha Juma Omar akiwasilisha ripoti ya ufuatiliaji na utoaji wa elimu kwa jamii  kuhusiana na vitendo vya uzalilishaji Zanzibar , wakati wa mkutano huo wa mafunzo yaliofanyika Kisiwani Pemba.
Afisa wa Tathimini na ufuatiliaji wa TAMWA Zanzibar Ndg. Mohammed Khatib akizungumza wakati wa mkutano huo na Wanamtandao 
Mwanamtandao Ndg.Seif Sharif Makame, akichangia  mada wakati wa mkutano huo wa Wanamtandao uliofanyika Pemba.  
Wanamtandao wakishiriki kikao cha kupokea na kujsdili ripoti ya utekelezaji wa majukumu yao.

Na Gaspary Charles – TAMWA PEMBA

MTANDAO wa kupinga udhalilishaji Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba umefanikiwa kutoa elimu kwa wanajamii 2,667 kwa Mwezi wa Agosti na Septemba, ambapo watu 1,452 sawa na asilimia 54 kati yao wakiwa ni wanawake na wanaume 1,215 sawa na asilimia  46 ya wote waliofikiwa katika kipindi hicho.

Hayo yamebainishwa na wanamtandao huo wakati wa kikao cha kujadili maendeleo ya kazi za kutoa elimu, kufuatilia na kuibua kesi hizo kilichofanyika katika Ofisi za TAMWA Pemba.

Seif Sharif Makame miongoni mwa wanamtandao huo alisema katika kipindi hicho pia wamefanikiwa kuibua na kufuatilia kesi Nane ambapo kati ya kesi hizo Nne zinahusiana na matukio ya ubakaji.

“Katika juhudi za kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ya jamii tulifanikiwa kuibua kesi Nane huku kesi Nne zote zikiwa ni kesi za ubakaji,” alisema.

Kwa upande wake Asha Juma Omar, alisema wazazi wanatakiwa kuwajibika ipasavyo kwa kuwafuatilia watoto wao  kwani  kufanya hivyo itasaidia kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vya udhalilishaji.

Alisema kupitia utoaji wa elimu na ufuatiliaji wa kesi hizo katika jamii wamebaini kuwepo kwa mashirikiano madogo katika kuripoti matukio ya ushalilishaji jambo linalopelekea kuongezeka kwa viutendo hivyo katika jamii.

Katika hatua nyingine alibainisha kuwa uwepo wa mikutano ya kampeni umeathiri kwa kiasi kikubwa jihudi za ufikiaji wa jamii nyingi kutokana na wengi wao kushindwa kuhudhuria katika mikutano yao.

“Mikutano ya kampeni imekuwa ni changamoto kubwa  kwetu katika harakati hizi za ufikishaji wa elimu kwa jamii kwani sehemu nyingi tulizokuwa tunatembelea  wengi wao sasa wanajikita zaidi katika mikutano ya kisiasa,” aliongeza.

Mapema akizungumza katika kikao hicho, Afisa Tathimini na ufuatiliaji wa TAMWA Zanzibar, Mohamed Khatib Mohamed aliwasisitiza wanamtandao hao kuendelea kuzifuatilia kwa ukaribu kesi zilizoibuliwa ili kuhakikisha wanawasaidia wahanga wa matukio hayo kupata haki zao katika vyombo husika.

Alisema, “lengo na jukumu la uwepo wa mitandao ya kupinga udhalilishaji katika jamii sio tu kuibua kesi na matukio hayo bali ni kuhakikisha tunaziibua na kuzifuatilia kuanzia hatua ya mwanzo hadi mwisho.

Nae Mratibu wa TAMWA Ofisi ya Pemba, Fat-hiya Mussa Said aliwataka wanamtandao huo kuongeza kuvu zaidi za kufuatilia kesi ambazo tayari zimeibuliwa ili ziweze kufikishwa katika ngazi husika za kisheria.

Aidha aliiomba jamii kuendelea kutoa mashirikiano kwa wanamtandao huo na kuacha tabia za kuficha matukio ya udhalilishaji ili wahusika wa vitendo hivyo waweze kuchukuliwa hatua kisheria.

Kikao hicho ni mwendelezo wa utekelezaji wa mradi wa kuongeza nguvu kwenye juhudi za mapambano dhidi ya vitendo vya udhalilishaji Zanzibar unaotekelezwa na Chama cha Waandishi wa Habari -TAMWA Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.