Habari za Punde

Endepo Atapewa Ridhaa Dk. Mwinyi ya Kuiongoza Zanzibar Ataendeleza Kasi ya Maendeleo Kuanzia Pale Alipoishia Mtangulizi.

 

MAKAMU Mwenyekiti wa CCM ambae pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein akihutubia katika mkutano wa kampeni ya CCM ya Mgombea Urais wa Zanzibar Mhe.Dk.Hussein Mwinyi uliofanyika katika uwanja wa Micheweni Wilaya Micheweni.  

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza  la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewataka wananchi wa Wilaya Micheweni na Wazanzibari kwa ujumla, kuwachagua wagombea kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM), ili kuleta mustakbali mwema wa uhai na maendeleo ya Taifa.

Dk. Shein ambae pia ni Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ametoa wito huo  Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba katika muendelezo wa Kampeni za chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu baadae mwezi huu.

Amesema ili Micheweni iweze kusonga mbele, kupata heshima , kupiga hatua za kimaendeleo pamoja na kukabiliana vilivyo na umasikini, ni vyema kwa wananchi wa Wilaya hiyo kumchagua mgombea wa Chama hicho katika nafasi ya Urais Dk. Hussein Mwinyi pamoja na wagombea wengine katika nafasi za Ubunge, Uwakilishi na Udiwani.

Alisema Dk. Hussein Mwinyi ni kiongozi mwenye uwezo mkubwa wa kiutendaji, kimaadili, kufikiri pamoja na kubuni mambo mapya, akibainisha uthibitisho wa mambo hayo katika utumishi wake uliotuka ndani ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia nadhifa mbali mbali.

Alisema Dk. Mwinyi ni msomi mbobezi, Daktari bingwa wa Binadamu hususan katika maradhi ya moyo, mwalimu wa madaktari, akiwa na uwezo mkubwa  wa kufikiri mambo mazuri yenye faida kwa Taifa.

Alisema endapo Dk. Mwinyi atapewa ridhaa ya kuiongoza Zanzibar ataendeleza kasi ya maendeleo kuanzia pale alipoishia mtangulizi wake, hivyo akawataka   wanachi kumtengenezea nfasi nzuri ya kuingia Ikulu.

“Lazima tuhakikishe wana CCM wote Unguja na Pemba tunampigia kura Dk. Hussein Mwinyi , tuzingatieni ukweli wa mtu……. msiridhike na vya kale, vyengine vya kale havifai”, alisema.        

Alieleza kuwa Dk. Mwinyi anaufahamu vyema Muungano wa Tanzania, na kusema kuwa sio mwanagenzi wa siasa za CCM, ambapo kwa nyakati tofauti amekuwa kiongozi.

Aidha, alisema Muungano ni ngao ya Wazanzibari na kuusifia Muungano huo kwa kuwa mfano mzuri wa kuigwa katika Afrika kutokana na baadhi ya mataifa kujaribu kuunganisha nchi zao bila mafanikio.

“Tuwape watu nafasi ya kuitumikia nchi yetu wenye uwezo, sio wanaotaka kujikweza……… na wale wenye uwezo wako CCM”, Alisema.

Pia, Rais Dk. Shein alisisitiza umuhimu wa kudumisha amani,umoja na mshikamano miongoni mwa Wazanzibar, na kusema mambo hayo ni muhimu kwao, hivyo ni vyema wakaipa nguvu CCM ili iweze kuongoza Dola.

Alisema Zanzibar inahitaji mihimili mitatu yenye nguvu kuelekea mafanikio.

Nae, Mgombea wa kiti cha Urais kupitia CCM, Dk. Hussein Mwinyi aliipongeza Serikali ya awamu ya saba, chini ya Uongozi wa Dk. Ali Mohamed Shein kwa utekelezaji mwema wa Ilani ya Uchaguzi ya 2015-2020.

Alisema Serikali ilifanikiwa kuimarisha sekta ya Afya na Ustawi wa Jamii katika nyanja mbali mbali, ikiwemo uimarishaji wa miundombinu, uapatikanaji wa dawa pamoja na vifaa tiba.

Alisema katika kipindi hicho sekta ya elimu nayo imepata mafanikio makubwa Wilayani humo, ambapo skuli mbili za kisasa za Ghorofa zenye viwango katika maeneo ya Wingwi na Micheweni zilijengwa zikiwa na viwango vinavyohitajika, kama vile maabara na maktaba.

Dk. Mwinyi alieleza mamabo yanayotarajiwa kukamilishwa endapo atapata ridhaa ya kuongoza nchi, ikiwemo kurasimishwa kwa Bandari ya Shumba ambayo itajengewa gati na soko la samaki.

Aidha, aliahidi kupandishwa hadhi Hospitali ya Micheweni, kuendeleza miundombinu ya Afya, ikiwemo ujenzi wa nyumba za wafanyakazi, kupatiwa vifaa tiba pamoja na kuajiriwa madaktari Bingwa.

Alisema Serikali ijayo inalenga kuwapatia Boti za kisasa wavuvi Wilayani humo ili waweze kuvua amaki katika maji makubwa zaidi na kupata tija kutokana na shughuli zao.

Vile vile alisema Serikali itasimamia ujenzi wa barabara za ndani katika maeneo tofauti Wilayani humo ili ziweze kupitika muda wote, sambamba na kulipatia ufumbuzi tatizo la uvamizi wa maji chumvi katika maeneo ya kilimo.

Mapema, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Aballa Juma Sadalla alisema CCM itaendelea kusimamia sera na Ilani yake inayotekelezeka pamoja na wagombea wanaouzika, kupitia  kampeni za kisayansi.

Katika mkutano huo Viongozi mbali mbali wa kitaifa walihudhuria, akiwemo Rais Mstaafu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Ali Hassan Mwinyi, Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali idd, Waziri Kiongozi Mstaafu Vuai Shamsi Nahoda, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Abdalla Juma Sadalla pamoja na wake wa viongozi wakuu.

Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 

 E-mail: abdya062@gmail.com

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.