Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe Balozi Seif Ali Iddi Azungumza na Mahujja Waliotarajiwa Kwenda Macca Mwaka Huu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Mahujaji Watarajiwa wakiokwama kutokana na mripuko wa Virusi vya Corona hapo Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil.
Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi Dr. Hussein Ali Mwinyi akisisitiza umuhimu wa kutunza Amani wakati Taifa linaingia kwenye Uchaguzi.
Waziri wa Katiba na Sheria wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanmzibar Mh. Khamis Juma Mwalimu akitoa maelezo kutokana na mwenendo mzima wa Ibada ya Hijja unaosimamiwa na Taasisi mbali mbali chini ya Uratibu wa Kamisheni ya Wakfu.
Mahujaji Watarajiwa wakisikiliza maelezo ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Tanzania Dr. Hussein Ali Mwinyi hayupo pichani alipowanasihi kusaidia Mitaani jamii ilinde Amani ya Nchi.
Mahujaji Watarajiwa wakisikiliza maelezo ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Tanzania Dr. Hussein Ali Mwinyi hayupo pichani alipowanasihi kusaidia Mitaani jamii ilinde Amani ya Nchi.

Mahujaji Watarajiwa wakiitikia Dua ya pamoja kuiombnea Nchi salama na Amani ndani ya kipindi cha mpito cha Uchaguzi na baada ya uchaguzi hapo Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil.

Na.Othman Khamis.OMPR.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewapongeza Waumini wa Dini ya Kiislamu waliokosa kwenda kutekeleza Ibada ya Hijja katika Mji Mtukufu wa Maka Nchini  Saudi Arabia Mwaka jana kwa kubakia na nia yao hadi pale wakati utakaporuhusu licha ya mripuko wa Virusi vya Corona vilivyoikumba Dunia.

Alisema zipo baadhi ya Nchi Duniani hadi sasa zinaendelea kuzuia Raia wao kusafiri nje ya Mataifa yao na kutoruhusu Wageni kuingia kwenye Nchi hizo kutokana na janga hilo thakili lililogharimu Maisha ya Watu wengi na kuacha taharuki.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa pongezi hizo wakati akizungumza na Mahujaji watarajiwa hao kwenye ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakili Kikwajuni Kikao alichokitumia kuwaaga Rasmi akikamilisha muda wake wa Utumishi wa  Serikali katika nafasi ya Umakamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ndani ya Kipindi cha Miaka Kumi.

Aliwataka Mahujaji Watarajiwa hao kutoona machungu kutokana na matukio hayo ya kuzuka kwa Ugonjwa unaosababishwa na Virusi vya Corona kwani Dunia bado haijakaa salama kutokana na Janga hilo na wanapaswa kuondoa fikra  za kudhania kuwa Karantini ni sehemu ya Jela.

“ Hata Mimi Mwenyewe hayo yamenikuta wakati nikirejea kutoka kwenye Uchunguzi wa Afya Nchini Cuba pale nakaribia kuwasili Nyumbani nikiwa njiani Napata taarifa kwamba nitakapofika na Timu yangu nitalazimika kukaa Karantini kwa kipindi cha siku 14. Kwa kujiridhisha nikalazimika kuongeza siku saba”. Alisisitiza Balozi Seif.  

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kupitia kundi hilo la Mahujaji Watarajiwa wa Zanzibar aliwakumbusha Wananchi kuzingatia umuhimu wa kutekeleza masharti yote yaliyowekwa na Wataalamu wa Afya katika mapambano dhidi ya Virusi vya Corona ili visirejee tena katika Ardhi ya Tanzania.

Akitoa salamu kwa Mahujaji Watarajiwa hao Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ambae pia ni Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi Dr. Hussein Ali Mwinyi aliwaomba Wachamungu hao pamoja na Wananchi wote waendelee kuliombea Dua Taifa ili livuke salama ndani ya kipindi hichi cha mpito cha kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu.

Alisema Wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla wanachokihitaji kabla na baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu ni kuona maisha yao yanaendelea kama kawaida bila ya wasi wasi katika muelekeo wa misingi ya Amani na Utulivu waliouzoea.

Dr. Hussein alisema endapo atapata ridhaa ya kuwatumikia Wananchi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar atakayoiongoza itahakikisha kwamba changamoto zitakazowakabili Waumini hao katika kwenda kutekeleza Ibada yao ya Hija itaangalia njia ya kusaidia mapungufu yatakayojitokeza.  

Mapema akitoa maelezo ya mtiririko mzima wa Mwenendo wa Mahujaji hao Watarajiwa Waziri wa Katiba na Sheria Zanzibar Mh. Khamis Juma Maalim alisema Zanzibar imesajili Taasisi 23 zinazosimamia kusafirisha Mahujaji kwenda kutekeleza Ibada ya Hijja Maka Nchini Saudi Arabia.

Mh. Khamis alisema Mahujaji Watarajiwa 1,600 walijiandikisha Mwaka Jana katika Taasisi 19 ambapo jumla ya Mahujaji Watarajiwa 933 wamewahi kukamilisha gharama za malipo kwa ajili ya safari hiyo ya Kidini.

Akitoa shukrani katika hitimisho la Mkutano huo Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana Zanzibar Sheikh Abdullah Talib Abdullah alimshukuru na kumpongeza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa jitihada zake zilizosaidia Uratibu mzuri katika usimamizi wa Ibada ya Hija.

Sheikh Talib alisema jitihada hizo ndizo zilizosaidia kuibuliwa kwa wazo la kuanzishwa kwa Mfuko wa Hija Zanzibar  ambao tayari Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesharidhia jambo hilo muhimu kwa mustakabala wa Ibada ya Hija ambayo ni nguzo ya Mwisho ya Uislamu inayomuwajibikia kila Muumini mwenye uwezo kuitekeleza.

Ibada ya Hijja Mwaka uliopita imetekelezwa kwa kuwahusisha Waumini wa Dini ya Kiislamu wa Saudi Arabia pekee kutokana na mripuko wa Homa kali ya mapafu inayosababisha na Virusi vya Corona. {Covid -19} iliyopelekea Serikali ya Nchi hiyo kuzuia Waumini wa nje ya Taifa hilo.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.