Habari za Punde

WENYE ULEMAVU WA KUONA WAIOMBA TCRA KUWASAIDIA WAPATE MENU YA SAUTI KWENYE SIMU.

Na Hamida Kamchalla, TANGA.

WATU wenye ulemavu wa macho wameiomba mamlaka ya mawasiliano nchini (TCRA) kuangalia jinsi ya kuwasaidia katika huduma za kimtandao ya simu za mkononi katika kutengeneza menu maalumu ya sauti kwa ajili ya watu wasioona.

Rai hiyo imetolewa jana na mshiriki Bakari Hassan wakati alipokuwa akichangia mada kwenye mafunzo yaliyohusu mkataba wa huduma kwa mteja wa TCRA yalifanyika jijini Tanga na kuwashirikisha wasioona kutoka mikoa ya Dar es salaam na Tanga.

Hassan alisema alishawahi kupeleka ombi hilo kwenye kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom mwaka 2014 na alisikilzwa na kupewa ahadi lakini mpaka sasa hakuna kilichototendeka hivyo kuiomba mamlaka hiyo inayohusika na mawasiliano kuwasilisha ombi lao na kupatiwa ufumbuzi katika mitandao yote nchini. 

"Hili ni wazo langu ambalo nililipeleka kwenye kampuni moja ya simu za mkononi lakini halikufanyiwa kazi, niombe kwenu mtuwasilishie ombi hili kwa makampuni yote ya simu, watengeneze menyu kwa ajili ya sisi wenye changamoto ya kusoma, iwe katika mfumo wa sauti" alisema.

"Kuna simu nyingine hasa zile za smartphone zina mfumo ya sauti lakini sisi tusioona hatuwezi kutumia, tunatumia hizi za kubonyeza na haina mfumo wa sauti, nawaomba wadau walisikie hili na walifanyie kazi kwani pia itasaidia kuboresha biashara na huduma zao kwa ujumla" aliongeza.

Naye mkuu wa TCRA kanda ya kaskazini Imelda Salum alisema amelipokea ombi hilo na mamlaka italiwasilisha kwa wahusika wa mitandao kuangalia jinsi ya kulifanyia kazi.

Akitoa mada kuhusu mkataba huo mkuu wa kitengo cha kudhibiti ubora wa huduma za TCRA Haruni Lemanya alieleza kwamba mkataba umelenga kuboresha maisha ya watanzania kupitia udhibiti wenye ufanisi, unaochochea na kukuza ubunifu ambao unahakikisha kupatikana huduma bora na imara za mawasiliano ambazo zitatolewa kwa gharama nafuu.

Lemanya alisema kuwa mamlaka pia imejikita katika kuboresha ustawi wa watanzania kupitia utoaji wa huduma za udhibiti zenye ubora ambazo zitahakikisha upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa wote kwa kutekeleza mfumo wa ubora wa uendeshaji katika shughuli zote.

"TCRA inaboresha na kupitia upya malengo yake ya ubora mara kwa mara na kuwafahamisha wahusika wote ndani ya mamlaka, tunahakikisha tunawajibika katika kutekeleza majukumu yetu kwa haki, kujali na kwa kuzingatia dhana ya uwazi" alieleza.

Aidha alisema kuwa mamlaka inaamini katika wawezeshaji kwa wafanyakazi wake kwa kuwapa uwezo wa kupambana na changamoto, kutoa maamuzi ba kutekeleza kikamilifu wajibu wao katika sehemu zao za uwajibikaji.

Hata hivyo Lemanya alibainisha kwamba dhamira kuu ya mamlaka hiyo ni kusimamia huduma za mawasiliano ya posta na kielektroniki kwa ufanisi, kuboresha utendaji wa watoa huduma na kulinda maslahi ya watumishi wa huduma za mawasiliano.

"Tunafanya hata yote kwa lengo la kutoa mchango wetu kwa maendeleo ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na dira yetu ni kuwa mdhibiti wa mawasiliano ya posta na kielektroniki mwenye hadhi ya kimataifa" alisisitiza.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.