Habari za Punde

Dkt. Abbasi: Kanuni za Kitaifa Anti Doping kuanza kutumika mapema mwakani

Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi akiwataka viongozi wote wa Vyama na Mashirikisho ya Michezo kuhakikisha kila mmoja anawajibika katika kutoa maoni, alipokuwa akifungua Warsha ya kutoa maoni katika Rasimu ya Kanuni zitakazoasiliwa kwa ajili ya kupinga mbinu haramu za matumizi ya madawa za  kusisimua misuli na kuongeza nguvu michezoni (Anti Doping) iliyofanyika Novemba 19, 2020 Jijini Dar es Salaam, (katikati) Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Yusuph Singo.

Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Yusuph Singo akiwasihi Wadau wa Michezo kulichukulia kwa uzito suala la Anti Doping na kuharakisha utoaji maoni, ili kuepusha taifa kufungiwa ushiriki wa michezo ya Kimataifa, Novemba 19, 2020, Jijini Dar es Salaam, katika ufunguzi wa Warsha ya kutoa maoni ya rasimu ya kanuni zitakazo asiliwa za kupinga mbinu haramu za matumizi ya dawa za kusisimua misuli na kuongeza nguvu michezoni.

Wadau wa Michezo wakifuatilia Warsha ya kutoa maoni ya Rasimu ya Kanuni zitakazoasiliwa za kupinga mbinu haramu za matumizi ya dawa za kusisimua misuli na kuongeza nguvu michezoni iliyofanyika leo Novemba 19, 2020 Jijini Dar es Salaam.

 Na Anitha Jonas – WHUSM, Dar es Salaam.

Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi amewataka viongozi wa Mashirikisho na Vyama vya Michezo kuwa wabunifu na kuandaa mikakati ya kukuza na kuendeleza michezo nchini.

Dkt. Abbasi ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam alipokuwa akifungua Warsha ya Wadau wa Michezo nchini  ya kutoa maoni ya katika rasimu ya Kanuni za Taifa za Kupinga mbinu haramu na matumizi ya dawa za kusisimua misuli na kuongeza nguvu  michezoni (Anti Doping).

Akizungumza katika Warsha hiyo Katibu Mkuu huyo na Msemaji Mkuu wa Serikali  alisisitiza kuwa kila kiongozi wa Chama na Mashirikisho ya Michezo atimize wajibu wake kwa kutoa maoni ili kujiepusha na kero ya wanamichezo kuja kufungiwa kushiriki michezo na kuliletea taifa aibu.

“Najua mnafahamu kuwa taasisi hii ya kupinga matumizi ya mbinu haramu na dawa za kuongeza nguvu michezoni namna ilivyo na nguvu hivyo ni vyema suala hili  mkalifanya kwa umakini, ili kuiepusha nchi kuwekewa vikwazo vya kushiriki michezo mbalimbali  kimataifa,” alisema Dkt.Abbasi.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo Michezo Tanzania Bw.Yusuph Singo alisema Kamati ya Anti Doping kwa sasa imefanya kazi ya kuandaa kanuni ambazo zitakazo asiliwa na kuwa za kitaifa na badae serikali itaunda sheria ya kusimamia masuala hayo ya kupinga mbinu haramu michezoni.

“Kenya walisitishiwa  kushiriki mashindano ya Kimataifa kwa kukosa “codes” ambazo zinaendana na mazingira ya nchi yao, ambazo ndiyo hizi kanuni tulizoandaa hivyo, ningependa suala hili tulichulie uzito na tulikamilishe haraka ili kuepusha taifa na chagamoto kama hii na tungependa kanuni hizi zianze kutumika mapema mwakani,” alisema Bw.Singo. 

Halikadhalika nae Katibu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania Bw.Philbert Bayi aliishukuru Serikali kwa kufanikisha kusainiwa kwa mkataba huo wa kupinga matumizi ya mbinu haramu michezoni mnamo mwaka 2017,  kwani Tanzania ilikuwa ni moja ya nchi chache zilizokuwa bado hazijasaini mkataba huo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.