Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk Hussein Ali Mwinyi Awakaribisha Wawekezaji Kutoka Jumuiya ya Madhehebu ya Bohora

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Ujumbe wa Jumuiya ya Mabohora Tanzania, ukiongozwa na Mwenyekiti wa Dawoodi Bohra Jamaat Dar es Salaam Sheikh.Tayabali Hamza Bhai Patanwalla, Ndg. Murtaza Ali Bhai na Nuruddin Bhai , walipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo na kumpongeza. 
 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dk. Hussein Ali Mwinyi amewakaribisha wawekezaji kutoka Jumuiya ya Madhehebu ya Bohora kuja kuekeza Zanzibar kutokana na fursa mbali mbali zilizopo hapa nchini.

Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi aliyasema hayo leo Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipokutana na Wajumbe wa Jumuiya ya Madhehebu ya Bohora kutoka Zanzibar na Tanzania Bara wakiongozwa na kiongozi wao Sheikh Tayabali Hamza Bhai Patanwalla ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya mwenye makao makuu yake Jijini Dar es Salaam.

Rais Dk. Hussein aliueleza Ujumbe huo wa Jumuiya ya Madhehebu ya Bohora kutoka Zanzibar na Dar-es Salaam kwamba milango ya Zanzibar iko wazi hivyo, anawakaribisha kuja kuekeza Zanzibar hasa ikizingatiwa kwamba walio wengi katika Jumuiya hiyo ni wafanyabiashara.

Alisema kuwa Zanzibar ina fursa nyingi za kuekeza katika sekta mbali mbali za maendeleo zikiwemo viwanda hivyo, aliwataka kuitumia fursa hiyo na kusisitiza kwamba iwapo  itazitumia fursa hiyo vyema itasaidia katika kutoa ajira kwa vijana.

Aliongeza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane itaendelea kushirikiana na Madhehebu hayo pamoja na yale mengine yote hapa nchini katika kuhakikisha kunakuwepo mashirikiano ya pamoja kwa azma ya kuendeleza na kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo.

Rais  Dk. Hussein Mwinyi aliipongeza Jumuiya hiyo kwa kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha na kuendeleza sekta mbali mbali za kijamii, kiuchumi na kimaendeleo zikiwemo huduma za afya, elimu na nyenginezo.

Aidha, Rais Dk. Hussein Mwinyi alitoa shukurani kwa Kiongozi wa Madhehebu ya Bohora duniani Dk. Syedna Mufaddal Saifuddin kutokana na salamu zake za pongezi alizomletea ambazo ziliwasilishwa na viongozi hao katika mkutano wao huo hivi leo.

Akitoa shukurani kutokana na salamu hizo, Rais Dk. Mwinyi aliipongeza Jumuiya hiyo kwa kuendeleza uhusiano na ushirikiano uliopo na kuahidi kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  itaendelea kushirikiana na Jumuiya hiyo bega kwa bega.

Mapema viongozi wa Jumuiya ya Madhehebu ya Bohora walimkabidhi Rais Dk. Hussein Mwinyi salamu za pongezi zilizotolewa na Kiongozi wa Madhehebu ya Bohora duniani Dk. Syedna Mufaddal Saifuddin kwa ushindi mkubwa alioupata na kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Akisoma salamu hizo kutoka kwa kiongozi huyo, Bwana Murtaza Zakirhussein AliBhai ambaye ni Mjumbe wa Jumuiya hiyo alieleza kuwa Kiongozi wa Madhehebu ya Bohora duniani Dk. Syedna Mufaddal Saifuddin anatoa pongezi kwa Rais Dk. Hussein na kusema kwamba wananchi wa Zanzibar wana matumaini makubwa na uongozi wake.

Salamu hizo zilieleza kwamba kiongozi huyo ana matumaini makubwa kwamba Zanzibar itaendelea kupata mafanikio makubwa katika kuendeleza kujiletea maendeleo yake kiuchumi, kijamii na  kiutamaduni.

“Hongera kwa ushindi mkubwa ulioupata katika uchaguzi uliopita, watu wa Zanzibar wamekuchagua wewe wakiwa na matumaini makubwa ya maendeleo kwa kutambua kwamba wewe utaiongoza Zanzibar kwa amani, umoja na mshikamano utakaodumu leo na siku zijazo”, ilieleza sehemu ya salamu hizo za pongezi kutoka kwa Dk. Saifuddin.

Sambamba na hayo, kiongozi huyo wa Mabohora duniani alimuombea dua Rais Dk. Mwinyi kwa Mwenyezi Mungu yeye na familia yake pamoja na wananchi wote wa Zanzibar ili wazidi kupata maendeleo zaidi na Allah aendelee kuwa mlinzi wao.

Kwa upande wao viongozi hao waliofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa pamoja waliipongeza hotuba aliyoitoa Rais Dk. Hussein Mwinyi siku aliyowaapisha Mawaziri katika viwanja vya Ikulu na kusema kwamba imewatia moyo na kuwapa matumaini makubwa ya mafanikio na maendeleo kwa Zanzibar na kuamini kwamba yajayo ni neema tupu.

Viongozi hao walimuahidi Rais Dk. Hussein Mwinyi kwamba watahakikisha Jumuiya yao inalichukua kwa mikono miwili suala la uwekezaji katika sekta mbali mbali za maendeleo ikiwemo viwanda na sekta nyenginezo na kuahidi kulifanyia kazi kwani limo ndani ya uwezo wao, huku wakiahidi kiongozi wao kufika Zanzibar pale atakapofanya ziara tena hapa nchini kwani mnamo Agosti 17,2020 alifanya ziara nchini  Tanzania.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.