Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe,Dk. Hussein Ali Mwinyi Ameutaka Uongozi wa Bandari na Mamlaka ya TRA Kulitubia Ghala Jipya la Kuhifadhia Mizigo Saateni Jijini Zanzibar.c la Bandari i

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameutaka uongozi wa Bandari pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhakikisha kazi za kulitumia ghala jipya la mizigo lililopo Saateni zinaaza mara moja ili kupunguza mlundikano wa makontena katika bandari ya Malindi.

Dk. Hussein aliyasema hayo leo huko Saateni Jijini Zanzibar mara baada ya kutembelea ghala jipya la mizigo lililojengwa na Kampuni ya Serikali.

Katika maelezo yake Dk. Hussein alisisitiza haja ya kutumika haraka ghala hilo kwani hatua hiyo itapunguza mlundikano wa makontena katika bandari ya Malindi huku akikea tabia ya kufanya kazi kwa mazoeza kutokana na Kampuni hiyo ya ujenzi kuchukua muda mrefu wa ukamilishaji wa ghala hilo.

Rais Dk. Hussein alisikitishwa na hali hiyo ya kuchelewa kukamilika kwa ghala hilo hasa ikizingatiwa kwamba wajenzi ni Kampuni ya Serikali ambayo watendaji wake wakuu ni askari wa Idara Maalum za SMZ.

Alisema kuwa utendaji kazi kwa mazoea ndio uliopelekea kulundikana kwa makontena katika bandari ya Malindi na kueleza kuwa fedha za Serikali zimepotea nyingi kutokana na ufanisi wa bandari kutoridhisha.

Hivyo, aliutaka uongozi wa Mamlaka ya Bandari kutoa kazi kwa muda maalum na fedha maalum kwani kutokufanya hivyo  kunapelekea uvunjifu  wa utaratibu wa Serikali kuilipa Kampuni fedha zote na matokea yake Kampuni hiyo kukaa miezi mitatu kwa kujenga waya wa umeme wa usalama uliozunguka kuta za ghala hilo.

Rais Dk. Hussein alisema kuwa jambo hilo halivumiliki kwani meli katika Bandari ya Zanzibar haziji na zinazokuja zinakawia kushusha mizigo hatua ambayo inatokana na uzembe na hatimae kusababisha upotezaji wa mapato.

Kutokana na hatua hiyo, Rais Dk. Mwinyi alisisitiza haja ya kuanza kazi mara moja ya kuweka mizigo katika ghala hilo huku akishanganzwa na maelezo ya Msimamizi wa Ujenzi huo Hassan Sarboko kutoka kikosi cha (KMKM) ya kumaliza ujenzi huo miezi mitatu iliyopita bila ya kulikabidhisha ghala hilo kwa wahusika.

Naibu kamishna wa TRA Zanzibar Mcha Hassan Mcha pamoja na Kaimu Mkurugenzi Ufundi Shirika la Bandari Salum Udi waliahidi kuanza kazi kesho ya kuweka mizigo katika ghala hilo baada ya kuhakikishiwa na Msimamizi huyo wa ujenzi kwamba ujenzi wa ghala hilo umekamilika.

Mapema Rais Dk. Hussein alikutana na uongozi wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji , Wizara ya Fedha na Shirika la Bandari pamoja na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi huko Ikulu Jijini Zanzibar na kueleza kwamba mkutano huo umefanyika kujadili hatua mbali mbali zitakazoleta jibu la kuwepo ufanisi uziorizisha katika Shirika la Bandari ya Zanzibar.

Kukutana na viongozi hao kunatokana na ziara yake aliyoifanya hapo jana katika bandari ya Malindi Zanzibar ambapo alipata maelezo juu ya ufanisi wa badari hiyo na ndipo alipoagiza kutaka kukutana na uongozi huo hivyo, alieleza kwamba kutokana na kuwa bandari ya Zanzibar ndio kitovu cha biashara hapa nchini hivyo ni lazima kufanyike utaratibu wa kuondosha changamoto hiyo kwa haraka.

Alisema kuwa ziara aliyoifanya jana lengo lake lilikuwa ni kujua ni tatizo gani linalofanya ufanisi kuwa mdogo jibu ambalo lilikuwa ni kujaa kwa makontena katika eneo la bandari na kupelekea kutopatikana ufanisi.

Katika maelezo yake Rais Dk. Hussein katika kikao hicho alieleza kuwa tatizo kubwa ni uhaba wa kuweka makontena jambo ambalo limepelekea meli nyingi kuacha kuja Zanzibar na kusababisha kushusha mizigo katika bandari za Mombasa na Dar-es Salaam kutokana na meli zinazokuja Zanzibar kukaa muda mrefu bila ya kushusha mizigo.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi aliwataka viongozi hao aliokutana nao kuhakikisha utaratibu wa haraka unapatikana katika kuondoa tatizo hilo lililopo Bandarini hapo na kukiri kwamba ZRB pmaoja na TRA wamekuwa wakikosa mapato kutokana na mlundikano wa makontena bandarini hapo.

Rais Hussein alisisitiza ufumbuzi wa haraka wa tatizo hilo hasa ikizingatiwa kwamba uchumi wa Zanzibar kwa asilimia kubwa unatokana na Bandari, hivyo viongozi hao kutokana na utaalamu wao ni vyema wakasaidia kwa kupatikana ufumbuzi huo.

Nao uongozi wa Bandari ulimuhakikishia Rais Dk. Hussein kwamba kupatikana kwa eneo la kuweka makontena (bandari kavu) litasaidia kwa kiasi kikubwa huku wakieleza jinsi walivyojipanga kwa kununua vifaa vya kazi hiyo zikiwemo gari za kubebea makontena.

Kwa upande wa Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Usafirishaji, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mustafa Aboud Jumbe alieleza hatua mbali mbali zilizochukuliwa na Wizara katika kukabiliana na tatizo hilo ikiwa ni pamoja na kuundwa kwa Kamati ya Mawaziri pamoja na kuwashirikisha wadau mbali mbali sambamba na kuongeza huduma zikiwemo za kibenki na ZRB.

Viongozi hao pia, walieleza kwamba tayari bandari hiyo imezidiwa na hiyo ni kutokana na kupitwa na wakati kutokana na udogo wake vile vile kuwa ya muda mrefu kwani tayari imeshafikisha takriban miaka 100 tangu kujengwa kwake.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.