Habari za Punde

SHULE ZA SEKONDARI ZA JUMUIYA YA WAZAZI CCM NA CHANGAMOTO YA MIUNDOMBINU

Na Hamida Kamchalla, TANGA.

IMEELEZWA kwamba miundombinu mibovu imechangia kwa kiasi kikubwa kuzorota kwa shule za sekondari za Jumuiya ya wazazi mkoani Tanga na kusababisha wanafunzi kutimkia kwenye shule za kata.

Hayo yalisema jana na mwanachama wa jumuiya ya wazazi mkoani hapa ambaye alikuwa mgombea ubunge viti maalum Makihiyo Ngwilizi kwenye kikao cha jumuiya hiyo na kusema kuwa kuna changamoto ya miundombinu katika shule zote sita ambazo zinasimamiwa na jumuiya hiyo mkoani hapa.

Ngwilizi alibainisha kwamba baada ya kufuatilia maendeleo ya shule hizo aligundua uchakavu wa majengo, kukosekana kwa maji pamoja na ubovu wa matundu ya vyoo kwa wanafunzi ambapo kuna baadhi ya shule vyoo vyao havina milango.

Alifafanua shule hizo kuwa ni pamoja na Boza iliyoko wilayani Pangani, Kidereko wilayani Handeni, Mombo ipo Korogwe mjini, Kwemvumo wilayani Lushoto, Mbaramo wilayani Muheza na Shemsanga ipo Korogwe vijijini ambapo alisema hazina wanafunzi kati ya hizo shule ya Mbaramo wilayani Muheza imefungiwa

“Changamoto kubwa ni miundombinu katika shule zetu, kila shule niliyopita kufanya ukaguzi nimekuta tatizo linajirudia, majengo yetu ni chakavu, hakuna maji, na kwengine unakuta hata vyoo havina milango, hivi ni mzazi gani atampeleka mtoto wake shule ambayo akiingia chooni anaonekana” alisema.

“Lakini pia niseme hizi shule za kata zimechangia wanafunzi wengi kutokujiunga na shule zetu nah ii inachangiwa na ubovu wa miundombinu yetu, ushauri wangu kwa ngazi ya Taifa, kufanyike utaratibu wa kuziangalia upya na kufuatilia kwa ukaribu shule zetu ili zirudi kwenye hali yake ya zamani” alisisitiza.

Kufuatia hali hiyo, jumuiya hiyo Taifa imetoa tamko kwa kilamkoa kusimamia shule zao na ikishindikana kuzisimamia basi zifungwe na majengoyatafutiwe mwekezaji atakayeweza kufanya shuhuli za maendeleo kuiingizia jumuiya kipato ili iweze kujikimu.

Tamko hilo limetolewa na Mwenyekiti wa jumuiya ya wazazi Taifa Edmund Mndolwa ambapo alisema changamoto zote ni lazima zifanyiwe kazi lakini pia alisisitiza jumuiya hiyo ijikite zaidi kwenye utekelezaji na usimamizi mzuri wa vyanzo vyao.

Mndolwa aliitaka jumuiya hiyo nchini kote kuangalia jinsi ya kuanzisha miradi kwenye shule zitakazoendelea kufanya kazi ikiwa ni pamoja na kutenga shule kila mkoa kwa ajili ya kusomesha wanafunzi wa kike masomo ya sayansi.

“Natoa tamko kwa kila mkoa wenye shule za wazazi zaidi ya tano ni lazima kutengwe shule moja kwa ajili ya kufundishia wanafunzi wa kike masomo ya sayansi,  lakini pia kila shule lazima iwe na mradi wa ufugaji wa nyuki, tujikite kwenye utekelezaji wa ilani yetu” alisema.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.