Habari za Punde

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali azungumza na watendaji wa Wizara kisiwani Pemba

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Simai Mohammed Said akizungumza na wafanyakazi wa Wizara ya Elimu wa kisiwani Pemba hapo skuli ya Maandalizi ya Madungu
Baadhi ya wafanyakazi na watendaji wa Wizara ya Elimu na mafunzo ya Amali wakisikiliza kwa makini hotuba ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali hapo skuli ya Maandalizi ya Madungu kisiwani Pemba

 Baadhi ya wafanyakazi na watendaji wa Wizara ya Elimu na mafunzo ya Amali wakisikiliza kwa makini hotuba ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali hapo skuli ya Maandalizi ya Madungu kisiwani Pemba

Na mwandishi wetu

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Simai Mohammed Said ameagiza kuwa kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi kufanya usafi wa nguvu katika maeneo yote ya majengo ya Taasisi za Elimu kwa Unguja na Pemba.
Pia ametoa agizo la kila Jumamosi ya wiki katika maeneo ya dakhalia zote kufanya usafi maalum kutokana na kuonekana kuwa katika hali mbaya.
Mhe Simai ametoa agizo hilo wakati akizungumza na baadhi ya watendaji wa sekta ya Elimu katika ukumbi wa Skuli ya Maandalizi Madungu na kuwataka waratibu wote kuhakikisha wanapanga utaratibu ili kuhakikisha agizo hilo linatekelezwa.
Mhe Simai pamoja na agizo hilo amewafafanulia wafanyakazi hao maagizo 13 waliyotakiwa kuyatekeleza Mawaziri wote wakati walipoapishwa na Mhe Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi dk Hussein Ali Hassan Mwinyi Siku chache zilizopita.
Miongoni mwa maagizo hayo ya Mhe Rais ambayo Mh. Simai ameyataja ni pamoja na uwajibikaji wa watendaji, kutoa haki za watu kwa uadilifu na kwa wakati, usimamizi wa mapato na matumizi pamoja na kuwa wabunifu.
Aidha amewataka watendaji wa Wizara hiyo kuhakikisha wanasimamia na kutekeleza majukumu yao na hatokuwa tayari kuwanyamazia watendaji wazembe ambao hawako tayari kufuata matakwa ya Serikali.
Pia amewataka waratibu hao kuwa wabunifu katika utendaji wa kazi zao na kuwa tayari kubadilika katika kazi zao ili kuhakikisha sekta ya Elimu inakuwa na kutoa wataalamu wengi zaidi nchini.
Mapema Afisa Mdhamin Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali mwalim Mohammed Nassor Salim amesema Wizara ya Elimu ina jumla ya Wafanyakazi 368 ambapo 217 ni wanawake na 151 ni wanaume ambao wanasimamia Wanafunzi 37200 wa Skuli za Sekondari.
Malim Moh’d amesema katika kudhibiti changamoto ya maadili ofisi yake imewapangia Skuli 3 kila Afisa ambazo anazisimamia kama mlezi, mkakati ambao umeleta mafanikio makubwa kimaadili na kitaaluma.
Wakati huo huo, Mhe Simai amefika Skuli ya Sekondari Fidel castro kwa lengo la kukichukua kitabu cha kusaini wageni wanaofika hapo ambacho kipo tokea mwaka 1963 hadi leo.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa kitabu hicho, Mhe Simai Amesema lengo kukihifadhi na kukiweka katika kumbukumbu za kihistoria kwani zimo saini za Marais waliopita akiwemo Rais wa kwanza baada ya Mapinduzi matukufu ya Zanziar Sheikh Abeid Amani Karume pamoja na viongozi mashuhuri.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.