Habari za Punde

Mhe Hemed: Watendaji wa Taasisi za Umma wana wajibu wa kutekeleza majukumu licha ya changamoto wanazopambana nazo

Katibu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Bibi Raya Issa Mselem akimpatia maelezo juu ya marekebisho yanayofanywa ndani ya Ukumbi wa Baraza hilo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman alipofanya ziara ya kutembelea Taasisi zilizo chini ya Ofisi yake.
 Mheshimiwa akipatiwa maelezo na Mmoja wa Watendaji wa Vitengo vya Mawasiliano ndani ya Jengo la Baraza la Wawakilishi hapo Chukwani nje kidogo ya Mjini wa Zanzibar.
 Msimamizi wa Maktaba ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar Nd. Haji akimfahamisha Mheshimiwa Hemed jinsi Maktaba hiyo inavyotoa huduma kwa Wahishimwa, Wafanyakazi na hata Wageni wanaofika kwenye Jengo hilo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla aKati kati akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Afisi ya Baraza la Wawakilishi wakiongozwa na Katibu wao Bibi Raya Issa Mselem.
Mheshimiwa Hemed Suleiman akiridhika na uwajibikaji wa Watendaji wa Tume ta Ukimwi Zanzibar iliyopo Shangani licha ya mazingira magumu ya eneo la kazi alipofanya ziara Maalum kujionea changamoto zao.Kulia ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed ni Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Ukimwi Zanzibar Dr. Ahmed Mohammed Khatib.

 Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Ukimwi Zanzibar Dr. Ahmed Mohammed Khatib kati kati akimtembeza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar katika vitengo mbali mbali vya Jengo la Ofisi ya Tume hiyo liliopo Shangani.

                                                 Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis , OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla alisema Watendaji wa Taasisi za Umma bado wana wajibu wa kuendelea kutekeleza majukumu yao ya kila siku licha ya changamoto wanazopambana nazo katika maeneo yao ya kazi.

Alisema ufinyu wa vitendea Kazi, ubobu wa maeneo ya kazi kwa baadhi ya Ofisi pamoja na Bajeti ndogo wanazopata katika uendeshaji wa  Afisi katika Taasisi hizo isiwe kikwazo cha kuwapunguzia uwajibikaji wao katika majukumu waliyopangiwa na Taifa.

Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla alitoa kauli hiyo wakati akiwa kwenye ziara za kutembelea Taasisi zilizo chini ya Ofisi yake kwa kukaguwa uwajibikaji na changamoto za Watendaji hapo Ofisi ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar iliyopo Chukwani pamoja na Tume ya Ukimwi Zanzibar iliyopo Shangani Mji Mkongwe wa Zanzibar.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeamua kupunguza matumizi yasiyo na msingi ili kile kinachokusanywa kifanikishe miradi mengine yenye umuhimu wa kuhudumia Jamii kama ilivyoahidi wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu zilizopita.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwakumbusha Watendaji wanaosimamia manunuzi ya vifaa na huduma za Kiofisi lazima wawe na hadhari ya kuepuka mitego ya Baadhi ya Wafanyabiashara wenye tabia ya kuuza Vifaa vibovu visivyo na hadhi ya Kiofisi.

Alisema wapo baadhi ya Watendaji kwa kushirikiana na Wafanyabiashara wajanya huingia kwenye Mikataba mibovu ya manunuzi ya Vifaa na zana za Maofisi na matokeo yake fedha nyingi zinazotengwa na kutolewa na Serikali kwa Kazi hiyo zinaingia mifukoni mwa wajanja hao.

Mheshimiwa Hemed alibainisha kwamba yapo matumizi mabaya ya fedha ndani ya baadhi ya Taasisi za Serikali na kusababisha mazingira yasiyokubalika ya ukusanyaji wa mapato jambo ambalo Serikali halitalifumbia macho na italazimika kuchukuwa hatua zinazofaa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza Viongozi na Watendaji wa Ofisi ya Baraza la Wawakilishi pamoja na wale wa  Tume ya Ukimwi Zanzibar kwa uchapakazi wao wa Kizalendo bila ya kujali ufinyu wa Ofisi zao kulingana na majukumu yao.

Alisema Serikali inatafakari kuwa na azma ya kujenga Jengo kubwa litakalokidhi mahitaji ya Taasisi na Idara zake zote zilizo chini ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanziubar ili kuondosha kabisa tatizo la ufinyu wa maeneo ya Kazi.

Mhedhimiwa Hemed alisema suala hilo muhimu liko kwenye uangalizi wa nama linavyoweza kuchukuliwa hatua inayofaa kulingana na hali halisi ya upatikanaji wa nguvu za utekelezaji.

Akigusia suala la Haki za Wafanyakazi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliendelea kuwakumbusha Wakuu wa Idara na Taasisi za Umma kuhakikisha kwamba maslahi ya watendaji wao yanapatikana tena kwa wakati muwafaka.

Mh. Hemed alisema haki ya Mfanyakazi lazima iheshimiwe na pale inapopungua au kukosekana kwa wakati muwafaka  Uongozi una wajibu wa kufanya mazungumzo ya busara na Mtumishi husika ili kuepuka malalamiko yanayoweza kukwaza uwajibikaji kwa Mfanyakazi.

Mapema Katibu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Bibi Raya Issa Mselem alisema Uongozi wa Baraza la Wawakilishi hivi sasa uko katika hatua ya kuufanyia marekebisho Ukumbi wa Baraza hilo ili uendelee kutoa huduma katika kiwango kinachokubalika.

Bibi Raya alisema mrejesho wa sauti wakati wa vikao vya Baraza la Wawakilishi vinapokuwa vikiendelea ni tatizo linalofanyiwa marekebisho kwa vile lilikuwa likileta usumbufu kwa Wajumbe na hata Wanahabari.

Katibu huyo wa Baraza la Wawakilishi alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba marekebisho hayo ya sauti ndani ya Ukumbi huo yanakwenda sambamba na matengenezo ya Paa la Jengo hilo ili kuondosha hitilafu inayotokana na maji ya mvua.

Naye kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Ukimwi Zanzibar Dr. Ahmed Mohammed Khatib alisema Tume hiyo iliundwa mnamo Mwaka 2003  baada ya tatizo la uwepo wa janga la Ukimwi kutokuwa na Taasisi mahsusi ya kulisimamia udhibiti wake.

Dr. Ahmed alisema Tume hiyo imepewa Majukumu matato katika utekelezaji wake akiyaanisha kuwa ni pamoja na Rasilmali, Sera, Uratibu, kuzijengea uwezo Sekta, kutoa Taarifa  pamoja na Elimu ambayo yamepata mafanikio makubwa.

Alisema licha ya changamoto ya ufinyu wa Bajeti, Ushiriki mdogo wa baadhi ya Sekta na ongezeko la Makundi Maalum yanayohitaji kupatiwa Mikakati Maalum ya kuyadhibiti lakini bado eneo la Taarifa na Elimu limeonyesha ufanisi uliodhihirika katika upunguzaji wa kuenea kwa Virusi vya Ukimwi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.