STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar
10.12.2020
RAIS wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameeleza utayari wa Serikali
ya Awamu ya Nane katika kushirikiana na Benki ya NMB kwa ajili ya kuimarisha uchumi
pamoja na huduma za kijamii Zanzibar.
Hayo ameyasema leo
wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa Benki ya NMB Ikulu
Jijini Zanzibar ukiongozwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki hiyo Bi Ruth Zaipuna
.
Katika maelezo yake
Rais Dk. Hussein alisema kuwa Benki ya NMB imepata mafanikio makubwa hivyo,
Serikali anayoiongoza iko tayari kushirikiana na Benki hiyo katika kuimarisha
miradi mbali mbali ya kiuchumi sambamba na huduma za kijamii.
Alisema kuwa katika
kuendeleza na kuimarisha miradi ya maendeleo ikiwemo afya na elimu Serikali
anayoiongoza iko tayari kutoa ushirikiano wake kwa Benki hiyo ili iweze kuunga
mkono juhudi za Serikali katika sekta hizo ambazo wamekuwa wakitoa misaada yao.
Rais Dk. Hussein
alisema kuwa Serikali iko tayari kukopa fedha kwa ajili ya kuwatafutia maeneo
wajasiriamali ili iweze kuwasaidia katika kufanya shughuli zao.
Alisema kuwa upo
umuhimu kwa Benki hiyo katika kuwakopesha wajasiriamali wadogo wadogo ikiwa ni
pamoja na kuwasaidia katika kuwapa mitaji, kuwawekea mazingira mazuri ya
kufanyia shughuli zao sambamba na kuwapa mafunzo ili waweze kufanya shughuli
zao kwa ufanisi mzuri zaidi.
Aidha, Rais Dk.
Hussein alieleza kuwa Serikali inahitaji mashirikiano katika eneo la elimu na
afya ambapo kwa upande wa sekta ya Elimu bado msaada wa madawati unahitajika hasa
ikizingatiwa kwamba vijana wanaoandikishwa skuli ni wengi.
Hata hivyo, Rais Dk.
Hussein alisisitiza haja katika kuiunga mkono Sekta ya Afya, bado kuna mahitaji
mbali mbali yakiwemo vifaa tiba, rasilimali watu na vyenginevyo.
Pamoja na hayo, Rais
Dk. Hussein aliuhakikishia uongozi huo wa Benki ya NMB kwamba Serikali
itaendeleza ushirikiano wake na iwapo kutatokea urasimu na vikwazo vyovyote
itakavyofanyiwa Benki hiyo basi wasisite
kutoa taarifa.
Alieleza umuhimu wa
kuwepo kwa mifumo madhubuti ya kukushanya kodi ambapo alieleza utayari wa
Serikali kutumia wataalamu wake kushirikiana na Benki hiyo ya NMB katika
kuhakikisha huduma hiyo inafanikiwa na nchi kuweza kunufaika kiuchumi.
Rais Dk. Hussein alieleza
haja ya kwa upande wa miradi mikubwa kuwepo kwa mipango madhubuti ya
utekelezaji wake ambapo Benki hiyo pia, inahitajika kutoa ushirikiano wake.
Aliongeza kuwa ni
masharti ya Benki hiyo ni vyema yakaendana na uwezo wa Serikali na kuangalia mi
miradi gani benki hiyo ingeweza kushirikiana na Serikali kwa mashirikiano ya
pamoja na wataalamu waliopo.
Mapema Afisa Mtendaji
Mkuu wa Benki hiyo ya NMB, Bi Ruth Zaipuna
alimpongeza Rais Dk. Hussein Mwinyi
kwa ushindi wa kishindo alioupata huku akiahidi kwamba Benki ya NMB itaendelea
kumuunga mkono yeye na Serikali yake katika kuhakikisha uchumi wa Zanzibar
unaimarika.
Alisema kuwa benki
hiyo iko tayari kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane
katika kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo zikiwemo zile za kiuchumi na
kijamii.
Akitoa historia ya
Benki hiyo, Bi Ruth Zaipuna alisema kuwa Benki hiyo ilianzishwa kwa Sheria ya
Bunge ya ‘National Microfinance Bank’ ya mwaka 1997 baada ya kuvunjwa iliyokuwa
Benki ya Taifa ya Biashara kwa mujibu wa Sheria ya Bunge.
Alisema kuwa Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilibinafsisha Benki ya NMB kwa kuuza
asilimia 49 ya hisa zake kwa Ushirika uliokuwa ukiongozwa na Rabo Bank huku
akieleza kwamba Benki hiyo ina uwezo wa kukopesha mteja mmoja hadi kiasi cha
TZS Bilioni 230.
Aliongeza kuwa benki
hiyo ya biashara iko imara katika kutekeleza kazi zake ikiwa ni pamoja na
kusaidiana na Serikali ya Awamu ya Nane kwani imejiandaa vyema na ina mtaji wa
kutosha unaofika Tirioni 7.
Alisema kuwa Benki
hiyo iko tayari kushirikiana na Serikali kama mdau mkuu wa kifedha katika
kuongeza kasi ya utekelezaji wa dira ya Rais Dk. Hussein mwinyi ya kuimarisha
uchumi wa Zanzibar.
Aidha, kiongozi huyo
wa NMB alisema kuwa Benki hiyo iko tayari kushirikiana na Serikali katika
kuwezesha miradi ya kimkakati ya Serikali.
Pamoja na hayo, alieleza
kuwa Benki hiyo ipo tayari kutumia uwezo na uzoefu wake mkubwa wa kiteknolojia
pamoja na ubunifu katika kutoa suluhisho la huduma za kielektroniki kwa
Serikali.
Bi Zaipuna alieleza
uzoefu wa Benki hiyo katika ukusanyaji wa kodi kidigitali ambapo tayari
imeshafanya shughuli hizo kwa taasisi mbali mbali ikwemo TANAPA, NCAA,
Hospitali, Huduma za malipo kwa taasisi za Serikali, TASAF,TRA na nyenginezo.
Alieleza kuwa kwa
gawio la Serikali ya Jamhuri ya Mungano wa Tanzania kwa mwaka 2019 lilikuwa ni
TZS Bilioni 15.3.
Mtendaji Mkuu huyo wa
NMB alisema kuwa Benki yake ameweza kuchangia katika sekta ya elimu kwa kutoa
madawati yapatayo 45,000 kwa skuli za msingi na sekondari, kompyuta 1,270,
vituo vya afya 460 vilivyopokea vifaa tiba pamoja na kuchangia majanga yakiwemo
ugonjwa wa Corona kwa kutoa TZS Milioni 400.
Alisema kuwa Benki
hiyo ina ATM 17 na Mawakala zaidi ya 100 huku akieleza azma ya Benki yake ya
kuweka huduma za Kibenki za kutumia kadi za Kimataifa “Union Pay International”
(UPI) katika uwanja mpya wa Abeid Amani Karume Zanzibar.
Halikadhalika, Bi
Zaipuna alisema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina asilimia
31.8 za hisa katika benki hiyo.
Sambamba na hayo,
Mtendaji Mkuu huyo wa NMB alieleza kuwa Benki hiyo imeweza kujenga uwezo wa
wakulima na wavuvi Zanzibar wakiwemo wakulima wa chumvi na mwani ambapo pia
mikopo ya zaidi ya TZS Bilioni 3.9 imetolewa kwa zaidi ya wafanyabiashara 200
wadogo wadogo na wakati na zaidi ya wajasiriamali 500 wamefikiwa kupitia
program endelevu ya kuwajengea uwezo.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment