Habari za Punde

Rais Dk Hussein Ali Mwinyi: Viongozi wa kisiasa wana dhima kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu
 

                                    STATE HOUSE ZANZIBAR

                       OFFICE OF THE PRESS SECRETARY

                                          PRESS RELEASE


Zanzibar                                                                         Disemba 10, 2020

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhadj Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Viongozi wa kisiasa wana dhima kubwa mbele  Mwenyezi Mungu na kubainisha maridhiano ya kisiasa yaliofanyika yameonyesha njia sahihi katika kudumisha umoja na mshikamano nchini.

 

Alhadj Dk. Mwinyi amesema hayo katika Dua maalum ya kuiombea nchi na viongozi wake amani, hafla iliyofanyika katika   Msikiti wa Mushawarra  uliopo Muembeshauri Jijini hapa.

  

Alisema kuna umuhimu kwa wananchi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwaongezea neema ya maridhiano yaliofanikisha uundaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, baada ya uchaguzi mkuu kumalizika.

 

Alisema viongozi wana dhima kubwa ya kuhakikisha wanadumisha amani na mshikamano na hivyo akatumia fursa hiyo kumpongeza Makamo wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharrif Hamad na Chama chake cha ACT Wazalendo kwa kukubali kushiriki katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).

 

Alisema yeye binafsi anaamini Wazanzibari wote ni kitu kimoja wakiwa na dhamira ya kuijenga Zanzibar na hivyo akawataka viongozi wa Dini kuendelea kuwaombea dua viongozi ili waendelee kuiongoza nchi kwa ufanisi.

 

 “Viongozi wana dhima kubwa kwa Mwenyezi Mungu …..maridhiano yaliofanyika yameonyesha mwelekeo sahihi  wa nchi“

 

Alieleza kuwa pamoja na Wazanzibari kuwa na mengi ya kumshukuru Mwenyezi Mungu, pia wanapaswa kuendeleza amani iliopo nchini ili kazi ya kuleta maendeleo na kukuza uchumi wa Taifa iweze kufanikiwa.

 

Alhadj Dk. Mwinyi alisema wakati wa kampeni za Uchaguzi mkuu uliopita alitowa ahadi nyingi sana  kwa wananchi ikiwemo ile ya kusisitiza kuendeleza amani na utulivu  iliopo nchini pamoja na kuwataka wananchi kuunga mkono juhudi za Serikali katika kufanikisha azma hiyo.

 

Aidha, aliwataka Wazanzibari  kufanya kazi kwa bidii kwa kila mmoja kutekeleza wajibu wake kikamilifu mahala alipo ili kuleta ustawi wa maisha  ya wananchi.

 

Alitoa shukurani kwa wananchi wote wa Zanzibar kwa hatua zao za kumtumia pongezi kwa kuleta maridhiano na kubainisha kuwa hatua hiyo  inaleta matumaini kuwa wananchi wengi wameridhia na kukubali jambo hilo.

 

Vile vile alisiitiza dhamira yake ya kuendelea kusimamia Umoja na mshikamano katika nchini ili kuharakisha kasi ya maendeleo.

 

Alhadj Dk. Mwinyi alimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kuibariki Zanzibar na  kubaki katika hali ya mani, sambamba na kuwapongeza waandaaji wa Dua hiyo kwa kuona umuhimu wa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupokea maombi yao , ikizingatiwa dua kama hiyo ilifanyika kabla ya Uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, 2020.

 

Mapema, Waziri wa Nchi (OR) Katiba, sheria,Utumishi wa Umma na Utawala Bora Haroun Ali Suleiman alitoa shukran kwa viongozi wakuu wa Kitaifa pamoja na wananchi waliohudhuria katika hafla hiyo muhimu yenye faida kubwa kwa taifa.

 

Nae, Katibu wa Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khalid  Mfaume  alisema dua hiyo inalenga kumshukuru Mwenyezi Mungu pamoja na kumuombea Dua Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhadj Dk. Hussein Ali Mwinyi na wasaidizi wake ili waweze kutekeleza vyema majukumu yao ya kitaifa.

 

Viongozi mbali mbali wa kitaifa walihudhuria katika dua hiyo wakiwemo Marais Wastaafu Alhadj Amani Abeid Karume, Alhadj Ali Mohamed Shein, Alhadj Balozi Seif Ali Idd, Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariamu Ali Mwinyi, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee, Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kaabi, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Dk. Mwinyi Talib Haji,  Mawaziri, Mwakilishi wa Mufti Mkuu kutoka Tanzania  Bara Sheikh Alhad Mussa Salum pamoja na wananchi wa Mikoa ya  Unguja.

  

Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 

 E-mail: abdya062@gmail.com

 

 

 

 

 

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.