STATE HOUSE
ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS
SECRETARY
PRESS
RELEASE
Zanzibar Disemba 26, 2020
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amevitaka vyombo vya Ulinzi na Usalama
kufanya uchunguzi wa haraka ili kubaini
chanzo cha ajali ya kuporomoka sehemu ya
jengo la makumbusho la Taifa la Beit al Ajab iliyotokea Disemba 25, mwaka huu.
Dk. Mwinyi ametoa agizo hilo leo,
wakati alipofanya ziara ya kutembelea Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja kwa lengo
la kutoa rambi rambi kwa wafiwa pamoja na kuwapa pole majeruhi wa
ajali hiyo.
Amevitaka vyombo hivyo kufanya uchunguzi
wa kina na wa haraka ili kubaini chanzo cha tukio zima la kuporomoka sehemu ya
jengo hilo na kuleta maafa kwa wananchi, ili Serikali iweze kuchukua hatua
madhubuti na kwa haraka.
Alisema msiba uliotokea ni wa Taifa na
hivyo akawapa pole wafiwa pamoja na kuwaombea dua majeruhi wa tukio hilo ili
waweze kupona kwa haraka na kurudi katika shughuli za ujenzi wa Taifa.
Aidha, amezitaka mamlaka mbali mbali,
ikiwemo mji Mkongwe, Shirika la Nyumba pamoja na taasisi ya Wakfu na Mali ya
Amana kufanya tathmin ya haraka ya majengo yote yalioko katika hali mbaya, ili
yaweze kufungwa na tathmin hiyo iweze kuielekeza Serikali namna ya kuyafanyia matengenezo ili kuepusha ajali kama
hiyo.
Alisema Serikali itagharamia mazishi
ya wananchi waliopoteza maisha kutokana na ajali hiyo, sambamba na kuchukua hatua
nyingine ili kuhakikisha matukio ya aina hiyo
hayatokei tena.
Katika hatua nyengine, Dk. Mwinyi alitembelea majeruhi wa jali
hiyo waliolazwa hospitalini hapo pamoja na wagonjwa mbali mbali wanaohitaji
matibabu kutokana na sababu mbali mbali
ikiwemo ajali.
Alieleza kuwa majeruhi waliopatwa na
ajali ya kuangukiwa na sehemu ya jengo la Beit Al Ajaib wanahudumiwa vizuri na
kusema Serikali itachukua hatua muhimu ili kuhakikisha changamoto ya upungufu
wa vifaa pamoja na dawa inapatiwa ufumbuzi.
Rais Dk. Mwinyi aliwapongeza
wafanyakazi wa Hospitali hiyo, wakiwemo madaktari na wauguzi kwa kazi kubwa na
nzuri wanayofanya kuwahudumia wagonjwa na kuwataka kuongeza juhudi.
Kutokana na tukio la kuporomoka sejemu ya jengo la Beit
al Ajaib, wananchi Burhani Ali Makune (35) mkaazi wa Mtoni Kidatu pamoja na
Pande Makame Haji (25) mkaazi wa Bumbwini walifariki dunia, wakati ambapo Hemed
Mattar Abdalla (39), Dhamir Salum Dhamir (37) pamoja na Ali Ramadhan Juma (23)
wanaendelea na matibabu Hospitalini hapo.
Katika ziara hiyo Dk. Mwinyi
aliongozwa na Kaimu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Simai Mohamed Said, Naibu
Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Halima Maulid Salum pamoja na Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Rufaa Mnazimmoja Marijani Msafiri
Marijani.
Abdi
Shamna, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422
Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822
E-mail:
abdya062@gmail.com
No comments:
Post a Comment