Habari za Punde

Taarifa Maalum kuhusu mwelekeo wa Maadhimisho ya miaka 57 ya Mapinduzi ya Zanzibar

  

TAARIFA MAALUM KUHUSU MWELEKEO WA MAADHIMISHO YA SHEREHE ZA MIAKA 57 YA  MAPINDUZI YA ZANZIBAR  

   

NDUGU WANANCHI, 


Awali ya yote nachukua fursa hii, kumshukuru Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema kwa kutujaalia afya njema na kuwa katika hali ya amani na utulivu katika nchi yetu. 

  

NDUGU WANANCHI, 

Kama tunavyoelewa kuwa, kila ifikapo tarehe 12 Januari ya kila mwaka, nchi yetu huadhimisha Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964 ambayo yamemkomboa Mzanzibari na kumpatia uhuru wa kweli katika nchi yake. Kwa kawaida maadhimisho ya Sherehe za Mapinduzi hufanyika kwa kutekeleza matukio mbalimbali na huhitimishwa kwa kilele ambacho hufanyika katika Uwanja wa Amaan Unguja au Uwanja wa Gombani Pemba.  

 

NDUGU WANANCHI, 

Kwa mwaka 2021, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeamua kuadhimisha Mapinduzi ya Zanzibar kwa kwa aina ya kipekee ambayo italeta hamasa zaidi na kuendelea kujenga uzalendo wa wananchi kwa Mapinduzi na Nchi yao.  

Kwa mnasaba huo, maadhimisho ya Sherehe za Mapinduzi kwa mwaka 2021 yatajumuisha shughuli zifuatazo: - 

i. Kutakuwa na siku ya usafi wa mazingira itakayofanyika tarehe 31/12/2020 ambayo itawashirikisha wananchi na watumishi wote wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na sekta binafsi. Wakuu wa Mikoa na Wilaya watahusika kuwaongoza wananchi katika usafi wa maeneo yatakayoainishwa kwa kila Wilaya. 

 

ii. Kutakuwa na mazoezi ya kitaifa yatakayofanyika tarehe 1/1/2021. Mazoezi haya yataanza saa 12:00 Asubuhi katika viwanja vya Mnara wa Mapinduzi Michenzani (Mapinduzi Square) kupitia Bi Ziredi, Mikunguni hadi Uwanja wa Amaani Unguja. Wananchi na watumishi wote wa Serikali na Sekta binafsi wanaombwa kushiriki katika mazoezi hayo. Mgeni Rasmi katika shughuli hii anatarajiwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dk. Hussein Ali Mwinyi.  

iii. Kufungua na kuweka mawe ya msingi katika miradi mbalimbali ya Maendeleo Unguja na Pemba, jumla ya Miradi 12 (3 Mawe ya Msingi na 9 ufunguzi) itahusika katika zoezi hili. Viongozi Wakuu wa kitaifa na Mawaziri watakuwa ndio wageni rasmi katika shughuli hizi. Wananchi wa maeneo jirani na miradi husika wanaombwa kushiriki kikamilifu katika matukio hayo. 

  

iv. Kutakuwa na maonesho ya Biashara ya Kitaifa yatakayofanyika katika viwanja vya Maisara ambapo sekta za umma na binafsi zitashiriki kikamilifu. 

 

v. Kutakuwa na mkesha wa Fashi fash zitakazopigwa kuanzia saa 6.00 usiku wa kuamkia tarehe 12 Januari, 2021 katika Viwanja vya Maisara Mjini Unguja na Tibirinzi Chakechake Pemba. Shughuli hii itatanguliwa na maonesho mbalimbali ya burudani.   

 

vi. Siku ya tarehe 12 Januari, 2021, kutafanyika maonesho ya Amsha Amsha na Mapinduzi yatakayofanywa na vikosi vyote vya Ulinzi na Usalama vilivyopo Zanzibar pamoja na maandamano ya wananchi wa Mikoa Mitano ya Zanzibar. Maonesho ya Amsha Amsha yataanzia katika viwanja vya Garagara Mtoni saa 12 asubuhi na kumalizia katika viwanja vya Mnazi Mmoja Mjini Unguja. Vikosi hivi vitajigawa katika makundi matatu ambayo yatapita njia tatu tofauti kama ifuatavyo:  

• Garagara - Maruhubi -  Saateni - Ziwani 

Polisi 

• Garagara - Maruhubi - Darajani - Ziwani 

Polisi na 

• Garagara – Darajabovu – Magomeni – Ziwani 

Polisi 

 

Baadae vikosi hivyo vitaondoka katika viwanja vya Ziwani Polisi na kuwasili katika viwanja vya Mnazi Mmoja kwa mapokezi rasmi mnamo saa 3:30 za asubuhi. Wananchi wote wanaombwa kuhudhuria kwa kujipanga katika barabara ambazo maonesho hayo yatapita pamoja na kushiriki katika shughuli ya mapokezi katika Viwanja vya Mnazi Mmoja. Mgeni Rasmi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dk. Hussein Ali Mwinyi atayapokea na baadae kutoa salamu fupi.  

 

vii. Sambamba na maonesho hayo ya Vikosi vya Ulinzi na Usalama pia kutakuwa na maandamano ya wananchi kutoka mikoa mitano ya Zanzibar  na kupokelewa rasmi katika Viwanja vya Mnazi Mmoja mnamo saa 3:00 za asubuhi.  

 

viii. Siku hiyo hiyo ya tarehe 12 Januari, 2021 ambayo ni siku ya kilele cha Sherehe za Mapinduzi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dk. Hussein Ali Mwinyi atalihutubia Taifa kupitia vyombo vya habari.  

 

ix. Pia kutakuwa na mashindano ya Kombe la Mapinduzi yatakayoshirikisha timu kutoka Unguja, Pemba na Tanzania Bara. Mashindano hayo yataanza tarehe 5 Januari, 2021 na fainali itafanyika katika Uwanja wa Amaan usiku wa tarehe 13 Januari, 2021. 

 

NDUGU WANANCHI, 

Kwa kumalizia, nichukue fursa hii kwa mara nyengine tena, kuwaomba wananchi wote Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, kushiriki kikamilifu katika shughuli hizo zote na pia nawaomba wananchi na taasisi zote za umma na binafsi kuweka usafi na kuyapamba maeneo yao ili kuzidi kuyapa haiba na hamasa katika maadhimisho yetu haya adhimu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.