Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe Hemed Suleiman Afungua Mkutano Mkuu wa ZATO Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla akizindua rasmi Mpango Kazi wa Jumuiya ya Makampuni ya waongoza misafara ya Watalii Zanzibar {ZAT kwa Mwaka 2020 – 2025. Picha na – OMPR – ZNZ.


Na.Othman Khamis OMPR.                                                                                                                           
Taasisi zinazojishughulisha na Sekta ya Utalii Nchini zinapaswa kutafuta njia mbadala ya kushirikiana na Wizara ya Kilimo  katika kukuza Utalii wa Kilimo      {Agri – Tourism} badala ya kuridhika na Utalii wa sasa wa Viungo ambao tayari umezoeleka sana.

Akiufungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Siku Tatu wa Makampuni ya waongoza misafara ya Watalii Zanzibar {ZATO} hapo Hoteli ya Naptune Resort Pwani Mchangani, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla alisema ni vyema vikaanzishwa vivutio vyengine vya mfumo mpya wa Watalii kuishi kwenye mashamba yenye utulivu.

Mh. Hemed Suleiman alisema Zanzibar inahitaji kuwa mfano miongoni mwa Nchi zenye nafasi ya juu katika kuendesha Utalii wa Kilimo kama zilivyo Nchi za Taiwan, Phillipine, Hawaii, Marekani na Brazil ambapo si vibaya kwa Taasisi hiyo ya kuongoza Watalii Zanzibar kwenda kwenye Nchi hizo kujifunza.

Alisema lipo shamba Moja linaloendeshwa na  Mtaalamu Mzalendo liliopo Shakani Magharibi Kusini mwa Mji wa Zanzibar ambalo tayari limekuwa mfano bora wa Utalii wa Kilimo ambapo Watalii na Wageni wanaofika eneo hilo hupikiwa chakula asilia kinacholimwa bila ya Kemikali kutoka shambani.

Alifahamisha kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane pamoja na mambo mengine imekusudia kushirikiana na Sekta Binafsi kwa ukaribu zaidi katika kukuza na kuimarisha Sekta ya Utalii ambayo hivi sasa ndio muhimili Mkuu wa Uchumi wa Taifa hili.

Mheshimiwa Hemed Suleiman alibainisha kwamba malengo hayo ya Serikali ikiwemo lile ya kupokea Watalii Laki 850,000 ifikapo Mwaka 2025 yatafikiwa kwa kushirikiana na Wadau Wakuu ambapo haiwezekani kuzungumziwa Utalii katika ukamilifu wake hapa Zanzibar bila ya kuwemo wa ZATO.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza uamuzi wa Uongozi wa Makampuni ya waongoza misafara ya Watalii Zanzibar {ZATO} katika malengo yake unaangalia zaidi muelekeo wa Utalii na Maendeleo ya Vijijini unaokwenda sambamba na malengo ya Serikali katika kukuza kipato cha Wananchi wa chini ambao asilimia kubwa iko Vijijini.

Alisema wakati umefika kwa ZATO kwa kushirikiana na wadau wengine ndani na nje ya Nchi kuimarisha eneo jengine la Makumbusho ya wazi sehemu za Vijijini ili kutoa nafasi za ajira hasa kwa Vijana wa maeneo hayo.

Mheshimiwa Hemed alieleza kwamba shehia au jumuiya za Vijana zinaweza kushirikishwa katika kuanzisha Makumbusho ya aina hiyo kwa gharama ndogo ambapo wananchi wakawaida wanaweza kuyasimamia baada ya kupatiwa Utaalamu wa kutosha.

Alifahamisha kwamba  endapo zitachukuliwa hatua hizo Wananchi wengi Vijijini watanufaika na kushawishika kuwa Sera ya Utalii kwa wote sio wimbo bali ni sera inayotekelezeka ikiwagusa wao moja kwa moja.

Alieleza kwa vile Utalii Vijijini kwa kiasi kikubwa utategemea zaidi utunzaji wa mazingira, Jumuiya  hiyo ya kuongoza Watalii ya ZATO inastahiki kusaidia kifedha Jumuiya ndogo ndogo zilizopo Vijijini ambazo zinajishughulisha na utunzaji wa mazingira.

“ Mkifanya hivi mtakuwa mnatekeleza wajibu wenu kwa Jamii{ Social Responsibility}. Msitengeneze fedha tu na kutumia, lazima mtenge faida yenu pia na kuirejesha kwa Wananchi”. Alisisitiza Mheshimiwa Hemed.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alibainisha kwamba Jumuiya ya ZATO ikiwasaidia Wananchi kuimarisha mazingira ni sawa na kujisaidia wao wenyewe Kibiashara kwa vile Utalii wa Vijijini kwa asilimia kubwa unategemea mazingira mazuri hasa.

Akizungumzia ushiriki wa Mwanamke katika kuongoza Watalii hapa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman aliuomba Uongozi wa ZATO kutafakari jinsi Mwanamke atakavyoingia katika fani hiyo kwa vile kipindi kirefu Sekta hiyo imetawaliwa na Wanaume pekee.

Mh. Hemed alisema kwa vile Shirika la kwanza la Utalii Zanzibar lilikuwa na Magari yaliyokuwa yakiendeshwa na Wanawake,  si jambo baya kulishughulikia suala hilo kwa lengo la kupanua Wigo wa ajira kwa upande wa Wanawake hapa Nchini.

“ Upo ushahidi kwa wale wanaobahatika safari za Kimataifa hushuhudia wanapofika Uwanja wa ndege wa Dubai Muungano wa Falme za Kiarabu utakuta Taxi nyingi zinazendeshwa na Wanawake ambao wamevaa vizuri”. Alisisitiza Mheshimiwa Hemed.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alikumbusha kwamba  kwa Zanzibar jambo hili sio geni ila linaonekana kufifia kidogo hasa katika kipindi cha Miaka ya hivi karibuni.

Akigusia suala la Mapapasi wanaoendesha Kazi hiyo kinyume na taratibu zilizowekwa na Serikali kupitia Mamlaka husika Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliagiza wale wasiohusika na eneo hilo wakiwemo wageni ni vyema wakaacha mara moja.

Alisema kitendo cha baadhi ya watu kujiingiza katika upapasi wakielewa kwamba hawahusiki na biashara hiyo ya kutembeza Watalii na Wageni, mbali ya kuikosesha mapato  Serikali lakini hata Jumuiya ya ZATO inavurugiwa.

Amemuagiza Waziri anayesimamia Mawasiliano na Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar kuandaa taratibu zitakazohakikisha Wana Jumiiya ya ZATO waliopo kisheria wanatekeleza majukumu yao kwa mujibu wa Sheria.

Akitoa Taarifa ya Jumuiya ya ZATO Mjumbe wa Jumuiya hiyo Bwana Khalifa Makame kwa Niaba ya Katibu Mkuu wake alisema Jumuiya ZATO inaishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kutengeneza matumaini yao na ya Wananchi kutokana na utulivu wa Kisiasa uliopo Nchini.

Bwana Khalifa alisema Jumuiya hiyo iliyoasisiwa mnamo Mwaka 1993 ikiwa na Wanachama 86 inakwenda na Dira inayozingatia Utalii wa kiwango cha juu lakini Zaidi unaojali kipao cha uhakika kitakachokidhi mahitaji ya kila Mdau.

Alisema ZATO katika hatua yake ya kujiendesha kiufanisi imefanikiwa kuwa na ushirikiano wa karibu na Mashirika ya Kimataifa ya  UNICEF na UNDP ambayo yamekuwa yakiiunga mkono Jumuiya hiyo katika Mafunzo na Semina zilizolenga kuimarisha Sekta ya Utalii Tanzania.

Akimkaribisha Mgeni Rasmi, Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Mheshimiwa Leila Mohammed Mussa  alisema maelekezo ya Rais wa Zanzibar Dr. Hussein Ali Mwinyi ya kuzitaka Wizara kushirikiana na Wadau wakuu yameanza kuchukuliwa hatua na Wizara hiyo.

Mh. Leila alisema Wizara katika hatua yake ya kufanikisha majukumu yake iliyopangiwa imeamua kuwekeza kwenye Vivutio vipya ambapo Taasisi za Umma na hata zile binafsi zinapewa fursa ya kutoa mapendekezo yao ili kufanikisha azma hiyo muhimu kwa Taifa na Jamii.

Wakitoa salamu Wawakilishi wa Mabenki ya Wazalendo Nchini yule wa CRDB Bwana Fadhil Molel  na Bwana Eladic Mwamondo wa Benki ya NMB wamesema tayari wameshatangaza rasmi kwamba Taasisi hizo za kifedha zimekusudia kuungana na Serikali katika kuona Sekta ya Utalii inakidhi mahitaji ya Uchumi wa Taifa.

Walisema kwa vile Taasisi zao zimebahatika kuwa na mitaji wa kutosha zimejitolea kutumia Wataalamu wake katika kuona mfumo wa uendeshaji wa Sekta ya Utalii hasa kipindi hichi cha Kuimarisha Uchumi wa Buluu kupitia Teknolojia ya kisasa ya Mawasiliano unakwenda kwa kasi na kuleta matumaini makubwa.

Katika mkutano huo Mkuu wa Mwaka wa Siku Tatu wa Makampuni ya waongoza misafara ya Watalii Zanzibar {ZATO} pamoja na mambo mengine umezindua Mpango Kazi wa Miaka Mitano kuanzia Mwaka 2020 -2025 pamoja na kufanya marekebisho ya Katiba yake ili iende na wakati wa sasa.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Jumuiya ya Waongoza Watalii Zanzibar {ZATO} Bwana Hassan Mzee akisema machache kabla ya Kumkaribisha Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar.

Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Mheshimiwa Leila Mohammed Mussa akisisitiza Wizara yake kuimarisha Vivutio vipya katika mpango wake wa kuimarisha Sekta ya Utalii Nchini kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla akiufungua rasmi Mkutano wa Mwaka wa  Makampuni ya waongoza misafara ya Watalii Zanzibar {ZATO hapo Hoteli ya Neptune Resort Pwani Mchangani }.

















No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.