Habari za Punde

WAWEKEZAJI WAIOMBA SERIKALI KUANGALIA UPYA TOZO ZA MIFUGO

 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul (kushoto) akiteta jambo na Mbunge wa Longido, Dkt. Stephen Kiruswa (kulia) walipokutana katika mkutano wa Wafugaji na Naibu Waziri huyo uliofanyika katika eneo la Mnada wa Mifugo liliopo katika kijiji cha Orendeke, Namanga Mpakani, Wilayani Longido, Mkoani Arusha Disemba 24, 2020. katikati ni Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel.



Na Mbaraka Kambona, Longido

Mkurugenzi wa Kiwanda cha kuchakata mazao ya mifugo cha Eliya Food Overseas, Shabbir Virjee ameiomba Serikali kuona uwezekano wa kupitia upya na kupunguza kodi na tozo za mifugo ili waweze kushindana vyema katika soko la Kimataifa na nchi jirani kama Ethiopia, Kenya, Somalia na Uganda ambazo kodi zao ni ndogo na zinawawezesha kununua na kuuza mifugo pamoja na mazao yake kwa bei nzuri.

Virjee alitoa ombi hilo kwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul alipotembelea kuona shughuli zinazofanywa katika kiwanda hicho cha kuchakata mazao ya mifugo kilichopo katika Kijiji cha Namanga Mpakani, Wilayani Longido, Mkoani Arusha Disemba 24, 2020.

Kwa Mujibu wa Virjee, kwa sasa wanalipa kodi zisizopungua tano kabla ya kusafirisha mazao ya mifugo nje ya nchi, jambo ambalo alisema limekuwa linawafanya wasiweze kushindana vizuri katika soko kwa sababu ya bei yao kuwa juu kutokana na kodi wanazolipia hapa nchini.

“Changamoto inayotukabili sisi ni kodi, tunalipa kodi zisizopungua 5, tunalipa kodi kwa Wizara ya kilimo shilingi 50 kwa kilo, Bodi ya Nyama tunalipa asilimia 1 ya thamani, Bakwata tunalipa kwa ajili ya kibali cha Halal, tunalipa kodi kwa Vibali vingine, na tunalipa asilimia 0.1 ya kodi ya mionzi, kila hatua tunalipa kodi ambazo kusema ukweli zinatufanya tushindwe kushindana na nchi jirani ambazo kodi zao ni ndogo,” alisema Virjee

Aliendelea kueleza kuwa changamoto nyingine wanayokutana nayo ni kutopatikana kwa Wanyama kama malighafi katika kiwanda hicho huku akiiomba serikali kuwasaidia ili waweze kupata Wanyama wengi  ili kiwanda kiwe na uhakika wa malighafi.

“Mhe. Waziri tunachangamoto nyingine ya kupata wanyama kama malighafi hapa kiwandani, Wafugaji wengi wanakwenda kuuza mifugo yao nchini Kenya kwa sababu ya bei nzuri huko, tunaomba tusaidiwe ili tuweze kupata malighafi ya uhakika, sisi hapa tunachinja kwa siku Mbuzi 2000 na Ngombe 400 hivyo unaweza kuona kuwa tunauhitaji mkubwa wa kuwa na uhakika wa malighafi ya kutosha kila siku,” aliongeza Virjee

Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa kama hali itaendelea hivyo uendeshaji wa kiwanda hicho utakuwa mgumu kwa sababu watashindwa kushindana katika soko la ndani hata nje, huku akisema lengo la kiwanda hicho ni kutoa ajira kwa Watanzania wasiopungua 150.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul aliwapongeza wawekezaji hao kwa jitihada kubwa walizozifanya kuwekeza kiwanda hicho ambacho kinatekeleza adhma ya Rais, Dkt. John Pombe Magufuli ya kuona Tanzania inakuwa nchi ya Viwanda na aliwahakikishia changamoto zao amezichukua na zitafanyiwa kazi.

“Nakuagiza Katibu Mkuu, Prof. Gabriel uunde timu itakayokuja kufuatilia ili kubaini hizo changamoto zote ikiwemo kwa nini Wafugaji wanapeleka mifugo yao kuuza nje ya nchi na taarifa hiyo itufikie haraka ili tuweze kuishauri serikali kutatua changamoto hizo mapema,”alisema Gekul

Pia, Waziri Gekul alimuagiza Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel kuangalia kwa namna gani Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) inavyoweza kusaidia kutatua changamoto ya upatikanaji wa malighafi katika kiwanda hicho.

‘Hiki kiwanda ni lazima tukilinde, tufanye kila linalowezekana kukilinda kiwanda hiki, ikiwemo kutoa elimu kwa wafugaji kujua uwepo wa kiwanda hiki na faida zake, ili waweze kujua kumbe wanaweza kuuza ng’ombe wao hapa hapa nchini bila kukimbilia nchi nyingine,” aliongeza Gekul

Aidha, alisema Wizara itaendelea kuwawezesha wafugaji kupitia vituo vya uhimilishaji hapa nchini kuwapatia mbegu bora zitakazowasaidia kupata ng’ombe wazuri watakao wawezesha kupata kipato kizuri kupitia viwanda vinavyochakata mazao ya mifugo nchini.

Tangu Kiwanda hicho kianze kufanya kazi miezi miwili iliyopita wameshachinja Mbuzi zaidi ya Elfu Saba (7000) na wameshaanza kupata masoko ya Kimataifa Uarabuni, Oman, Saudi Arabia na wanaendelea kufuatilia soko katika nchi ya China.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.