Habari za Punde

Dk Mwinyi: Safari ya kuijenga Zanzibar mpya sasa imeanza


                                                        STATE HOUSE ZANZIBAR

OFFICE OF THE PRESS SECRETARY

PRESS RELEASE

Zanzibar                                                                   28.01.2021

---

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imetiliana saini Hati ya Maelewano (MOU),kati yake na Mamlaka ya Uwekezaji ya Oman inayohusu Mpango Mkuu wa Ujenzi wa Bandari huko Mangapwani/Bumbwini.

Kwa mujibu wa Hati hiyo ya Maelewano Bandari hiyo inatarajiwa kujumuisha  Bandari tofauti ikiwemo bandari ya makontena na mizigo mchanganyiko, bandari itakayohudumia meli za uvuvi, bandari ya mafuta na gesi, bandari ya kuhudumia mafuta na gesi asilia, chelezo ya matengezo ya meli pamoja na Mji wa kisasa.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameshuhudia utiaji saini huo  uliofanyika leo Ikulu Jijini Zanzibar kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mamlaka ya Uwekezaji ya Oman.

Kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar aliyesaini Hati hiyo ni Katibu Mkuu  Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Amour Hamil Bakari na kwa upande wa Mamlaka ya Uwekezaji ya Oman aliyesaini ni Meneja Mkuu wa Kampuni hiyo Sheikh Mohammed Al-Tooqi ambaye aliongoza ujumbe kutoka Mamlaka hiyo ya Oman.

Mara baada ya utiaji saini wa Hati hiyo ya Maelewano, katika hotuba yake aliyoitoa Rais Dk. Mwinyi kwa wananchi kupitia vyombo vya habari vilivyokuwepo katika hafla hiyo alisema kuwa safari ya kuijenga Zanzibar sasa imeanza.

Alisema kuwa Serikali inaanza na bandari kwa sababu ndio uchumi wa Zanzibar hasa ikizingatiwa kwamba bandari hiyo itakuwa kubwa na ya kisasa.

“Sasa tumeanza safari yetu ya maendeleo na moja ya miradi ya kwanza kabisa kwa Serikali ya Awamu ya Nane utakuwa ni huu” alisema Dk. Mwinyi.

Rais Dk. Mwinyi alisisitiza uharaka wa jambo hilo huku akieleza kuwa kuna bandari mbili zimekusudiwa ikiwemo ile ya Mpigaduri ambayo patajengwa bandari ya Uvuvi ambapo mapema ya wiki ya mwanzo ya mwezi ujao utiaji saini Hati ya Maelewano wa bandari hiyo utafanyika.

Alisema kuwa bandari hiyo haitokuwa ya uvuvi pekee bali itahusisha miundombinu, viwanda pamoja na vyuo vya masuala ya bahari na bandari hiyo itakuwa ni tofauti na mipango iliyokuwa hapo awali.

Aliongeza kuwa Bandari ya Malindi lengo ni kuifanya iwe ya utalii, kwani ina eneo dogo na tayari hivi sasa imo ndani ya sehemu ya uhifadhi wa Mji Mkongwe.

Alisema kuwa shughuli zote za biashara  zikiwemo biashara za usafiri na usafirishaji zitahamia Mangapwani na eneo hilo la Malindi liwe eneo la kitalii ambapo mandhari ya eneo hilo itabadilika ambapo pia, utalii wa Mji Mkongwe nao utabadilika.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Mwinyi alieleza azma yake ya kuwa mambo hayo yaliyokusudiwa kufanyika kwa haraka ili Zanzibar iweze kuwa ni kitovu cha biashara pamoja na utalii.

Alieleza mambo makubwa na mazuri ambayo yatakuwepo katika eneo la mradi wa Mangwapwani na kuipongeza Mamlaka ya Uwekezaji ya Oman kwa kukubali kufanya kazi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika maono mapya ya kuwa na bandari ya kisasa.

Alieleza matarajio yake ya kufanyika kwa haraka kazi hiyo ili utekelezaji wake uanze mara moja na kusisitiza kwamba itakuwa ni busara iwapo kazi hiyo itafanyika ndani ya miezi mitatu  kwani hakuna miaka mingi ya kuzungumza na kuna miaka mitano ya kutekeleza na kuomba ifanyike kwa muda huo badala ya miezi sita iliyopo kwenye Mkataba kwani anaamini Mamlaka hiyo iko tayari na Serikali nayo iko tayari.

Mapema Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Rahma Kassim Ali alisema kuwa ujenzi wa Bandari unaotarajiwa kufanyika Mangapwani/Bumbwini ni moja ya dhana sahihi ya kuimarisha uwekezaji na hatimae kuleta matokeo bora kwa wananchi wa Zanzibar.

Alisema kuwa Mpango Mkuu huo unakusudio la kuubadilisha muonekano wa hivi sasa katika maeneo ya Mangapwani/Bumbwini ambapo pia, Serikali itajenga Mji wa Kisasa utakaojumuisha huduma mbali mbali zitakazosaidia uendeshaji wa bandari hizo.

Aidha, kwa maelezo ya Waziri huyo katika meneo hayo patatengwa eneo maalum la ujenzi wa viwanda.

Alisema kuwa baada ya Mpango huo kukamilika, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaelekeza nguvu zake katika kuutekeleza pamoja na kufungua milango ya kuwashirikisha na kuwakaribisha wawekezaji mbali mbali kuja kuwekeza katika ujenzi wa bandari hizo na maeneo hayo ikiwemo ujenzi wa viwanda.

Aidha, alisema kuwa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi kwa kushirikiana na Taasisi mbali mbali za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaahidi kutekeleza maelekezo ya Rais na kufanya kazi kwa bidii, uzalendo na uaminifu katika kusimamia na kutekeleza yaliyoainishwa katika Hati hiyo ya Maelewano.

Sambamba na hayo, Waziri huyo alieleza kwamba tangu kuanza kwa uongozi wa Rais Dk. Mwinyi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane imefungua fursa mbali mbali za uwekezaji ikiwa ni pamoja na kuendelea kuchukua hatua madhubuti katika kusimamia uwekezaji zenye maslahi mapana ya wananchi wa Zanzibar.

Nae Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji ya Oman Sheikh Mohamed Al Taooqi alieleza azma ya Mamlaka hiyo ya kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kutekeleza Mpango huo.

Alieleza mafanikio makubwa yatakayopatikana baada ya kukamilika kwa mpango huo huku akisisitiza mashirikiano ya pamoja katika kuhakikisha jambo hilo linafanyika kwa haraka huku akieleza utayari wa Mamlaka hiyo kuanza kazi.

Utiaji saini Hati ya Maelewano inayohusu Mpango Mkuu wa Ujenzi katika Bandari ya hiyo ya Mangapwani ni miongoni mwa hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane katika kutekeleza Sera yake ya Uchumi wa Buluu.

Aidha, hatua hiyo ni miongoni mwa mafanikio makubwa ya Serikali ya Awamu ya Nane chini ya uongozi wa Dk. Hussein Mwinyi kuelekea siku mia tokea alipoapishwa kushika wadhifa wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

1 comment:

  1. Ni jambo jema sn Dr Hussein amedhamiria Allah ampe nguvu.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.