Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais aagiza TRA na Shirika la Meli kumpatia taarifa za Kontena 410 zilizorundikana Bandarini

Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Nd. Mustafa Aboud Jumbe akimpokea Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla aliyefika Bandarini kukagua Maendeleo ya Uwajibikaji katika eneo hilo la Uchumi wa Taifa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla akitoa agizo la kupatiwa Ripoti kamili ya sababu za Makontena 410 ya Bidhaa tofauti kurundikana Banadarini kwa muda mrefu.

Picha na – OMPR – ZNZ


Na Othman Khamis, OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla ameziagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania {TRA} pamoja na Shirika la Meli Zanzibar kumpatia Taarifa ya kina juu ya Kontena Mia 410 zenye bidhaa mbali mbali ambazo bado zinazoendelea kurundikana ndani ya Bandari ya Zanzibar.

Alisema Mamlaka zinazozimamia usimamizi wa uingizaji huo wa Makontena lazima zichukuwe hatua kwa mujibu wa Sheria zinavyowaelekeza juu ya uingizaji na uondoshaji wa Makontena ili kuiingizia Mapato stahiki Serikali Kuu na kuepuka ubabaishaji wa baadhi ya Wafanyabiashara.

Mheshimiwa Hemed Suleiman alitoa agizo hilo alipofanya ziara fupi ya kuangalia maendeleo ya uwajibikaji kwenye Bandari Kuu ya Malindi akitekeleza ahadi yake aliyotoa kwa Uongozi wa Shirika la Bandari ya kuzuru katika eneo hilo mara kwa mara ili kujiridhisha.

Alisema tabia ya ucheleweshwaji wa Makontena inaonyesha mwanzo wa harufu ya rushwa jambo ambalo Serikali Kuu kamwe haitakubali kuridhia suala hilo wakati taratibu za uwepo wa Makontena zimeshaelekeza kuwa si zaidi ya siku 21 ambapo kinyume na hapo muhusika atalazimika kulipa fidia.

Mheshimiwa Hemed Suleiman alibainisha kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haikusudii kuwasumbua Wafanyabiashara waliokubali kuleta bidhaa Nchini lakini inachokizingatia kwa Washirika hao ni kuhakikisha wanafuata Sheria na Taratibu zilizowekwa na Mamlaka husika.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewakumbusha Viongozi na Watendaji wa Mamlaka ya Mapato, Shirika la Meli, Shirika la Bandari na taasisi nyengine zinazosimamia uingizaji wa bidhaa Nchini kuendelea kushirikiana na Taasisi za ulinzi katika kuona malengo ya Bandari yanafikiwa katika ukusanyaji wa Mapato.

Alisema suala la uaminifu katika kutekeleza wajibu na majukumu linapaswa kupewa nafasi yake miongoni mwa Viongozi na Watendaji hao ili Vifaa au bidhaa zinazoingizwa Nchini ziwe na Kiwango na uwezo kamili wa kuingia sokoni.

Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Zanzibar Nd. Nahaat Mohamed Mahfoudh alisema yapo maendeleo makubwa ya uwajibikaji ndani ya Bandari ya Bandari ya Malindi  hasa katika suala zima la kukabiliana na mrundikano wa Makontena.

Nd. Nahaat alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba hivi sasa yapo Makontena Elfu 1,120 kati ya Makontena Elfu 1,667 yaliyokuwa yamerundikana tokea mnamo Tarehe 2 Novemba Mwaka 2020.

Alisema Watendaji wa Shirika hilo wamepiga hatua kubwa ya kuyapunguza Makontena Mia 130 yaliyopelekwa katika eneo la hifadhi liliopo Saateni Mjini Zanzibar.

Naye Mwakilishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Afisi ya Zanzibar Ndugu Ali Bakari alisema Watendaji wa Mamlaka hiyo  wameshakamilisha mchakato wa kuyachambua Makontena 113 yenye Bidhaa tofauti ambapo kati ya hayo Makontena 17 wamiliki wake ambao ni Wafanyabiashara wameshakamilisha utaratibu wa Malipo.

Bwana Ali Bakari alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Makontena yaliyobakia kwa mujibu wa sheria na Taratibu za Mizigo yatalazimika kupigwa Mnada ifikapo Tarehe 20 Mwezi huu baada ya Wamiliki wake kushindwa kuyalipia katika muda uliowekwa kwa mujibu wa Taratibu za Kibandari.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.