Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais akutana na Wawakilishi wa Wananchi wa County ya Kwale kutoka Mombasa Kenya

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman kati kati  akizungumza na Wawakilishi wa Wananchi wa County ya Kwale kutoka Mombasa Nchini Kenya waliofika Ofisini kwake Vuga kwa ajili ya kujitambulisha na kusalimia.
Kiongozi wa Shughuli za Serikali  Bungeni kupitia County ya Kwale Mwepupheh Jackson Ndoro aliyevaa Kanzu na Kofia akisisitiza umuhimu wa Wananchi wa Kwale Mombasa Nchini Kenya na Zanzibar kuendelea kushirikiana katika ujirani mwema.

Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo yake na Wawakilishi wa Wananchi wa County ya Kwale kutoka Mombasa Nchini Kenya.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis, OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekusudia kuirasimisha Bandari ya Shumba ili kuondosha changamoto zilizopo na kuimarisha uhusiano kati ya Wananchi wa Mombasa Kenya na Zanzibar.

Mheshimiwa Hemed ameeleza hayo wakati akizungumza na Wawakilishi wa Wananchi wa County ya Kwale kutoka Mombasa Nchini Kenya waliofika Ofisini kwake Vuga kwa ajili ya kujitambulisha na kusalimia.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendeleza ushirikiano wake na Nchi ya Kenya katika Sekta ya Afya, Kilimo, Utalii pamoja na Uchumi wa Buluu Sekta ambazo zimepewa kipaumbele na Serikali chini ya usimamizi wa Rais wake Dr. Hussein Ali Mwinyi.

Mheshimiwa Hemed alisema kwa vile Zanzibar ni Nchi ya Visiwa imeshaamua kujikita Zaidi katika kuimarisha Uchumi wa Buluu kupitia Bahari kutokana na sekta hiyo kuwagusa Wananchi waliowengi sambamba na kuzitumia vyema Rasilmali zinazopatikana.

Alieleza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane imeweka mkazo Zaidi katika kuwafikishia huduma muhimu Wananchi wake hasa kuinua hali zao za maisha kitendo kitakachowasaidia kuwaingizia kipato cha kujikimu.

Akizungumzia kuhusu suala la Ulinzi na Usalama Mheshimiwa Hemed aliwataka Viongozi hao kuendelea kuwakumbusha Wananchi wao juu ya hatua ya kufuata sheria na taratibu kwa kuzingatia nidhamu za uingiaji na utokaji Nchini.

Akitoa shukrani zake kwa niaba ya msafara huo Kiongozi wa Shughuli za Serikali  Bungeni kupitia County ya Kwale Mwepupheh Jackson Ndoro amemueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa County ya Kwale imevutiwa na muundo wa Serikali ya Mapinduzi  na hivi sasa wapo mbioni kurekebisha mfumo na muundo wao ili uweze kutoa huduma bora kwa Wananchi wake.

Mheshimiwa Mwepupheh alimthibitishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba County yake itaendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Baraza la Wawakilishi Zanzibar katika kuona uhusiano wa pande hizo mbili unazidi kuimarika.

County ya Kwale Mombasa Nchini Jamuhuri ya Kenya imekuwa na ushirikiano na Zanzibar kupitia Baraza la Kutunga Sheria la Wawakilishi Zanzibar takriban kwa miongo Mitatu sasa.

 

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.