Habari za Punde

Makamu wa Rais Mhe Hemed auzindua rasmi Masjid Sultan , Maungani

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla akisalimiana na Viongozi na Waumini wa Dini ya Kiislamu alipofika kwa ajili ya kuufungua rasmi Msikiti wa Ijumaa wa Maungani { Masjid Sultan}.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla akikata utepe kuashiria akiuzindua rasmi Msikiti  wa Ijumaa wa Maungani uitwao Masjid Sultan uliojengwa na Taasisi ya Al Noor Charitable Agency for need.
Muonekano wa Msikiti wa Ijumaa wa Sultan uliopo katika Mtaa wa Maungani Wilaya ya Magharibi B ambao umezinduliwa rasmi na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman
Waumini wa dini ya Kislamu wa Maungani na vitongoji vyake wakifuatilia Hotuba ya Ijumaa kwenye Msikiti Mpya wa Kijiji hicho uliozinduliwa rasmi hivi punde
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman kati kati akiwa pamoja na Mkurugenzi wa Al Noor Charitable Agencry For Need Sheikh Nadhir  Mahfoudh Kushoto yake na Kulia yake ni Naibu Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Mahmoud Mussa Wadi wakifuatilia matrukio yaliyojiri ndani ya Msikiti wa Ijumaa wa Maungani
Mwakilishi wa Taasisi ya Al Noor Charitable Agency For Need Sheikh Mohamed Suleiman Akisoma risala kwa niaba ya Uongozi wa Taasisi hiyo kwenye hafla ya uzinduzi wa msikiti wa Ijumaa wa Maungani.
Waumini wa dini ya Kislamu wa Maungani na vitongoji vyake wakifuatilia Hotuba ya mgeni rasmi kwenye Msikiti Mpya wa Kijiji hicho uliozinduliwa rasmi hivi punde.
Naibu Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Mahmoud Mussa Wadi akiwakumbusha Waumini na Wananchi waendelee kuwa na haya ikiwa ibada ya kujiepusha na maovu mengi yaliyowazunguuka.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na Waumini wa Dini ya Kiislamu baada ya kuufungua Rasmi Msikiti wa Ijumaa wa Sultan { Masjid Sultan} uliojengwa katika Kijiji cha Maungani Wilaya ya Magharibi B.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla akimkabidhi rasmi Ufunguo wa Msikiti Imamu Mkuu wa Masjid Sultan  Sheikh Shaib Mbarouk Abdulla baada ya kuufungua rasmi.

Mkurugenzi wa Al Noor Charitable Agencry For Need Sheikh Nadhir  Mahfoudh kushoto akimkabidhi zawadi maalum Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla baada ya kukamilika kwa sherehe za uzinduzi wa Msiki wa Ijumaa wa Maungani.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis, OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla amezitaka Kamati za Waumini wa Dini ya Kiislamu zinazopewa majukumu la kusimamia uendeshaji wa Misikiti kutumia fursa ya uwepo wa Nyumba hizo za Ibada kwenye maeneo yao kwa kuendeleza Ibada katika misingi ya Umoja, Amani na mshikamano.

Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na Waumini wa Dinmi ya Kiislamu baada ya kuufungua Rasmi Msikiti wa Ijumaa wa Sultan { Masjid Sultan} uliojengwa katika Kijiji cha Maungani Wilaya ya Magharibi B hafla iliyoambatana na Ibada ya sala ya Ijumaa.

Alisema misikiti inayotumiwa katika ibada za sala ndio majengo yanayopaswa pia kuendelezwa Madrasa ili kuleta faida inayohuisha taaluma inayokuwa Mkombozi kwa Jamii hasa katika maandalizi ya Kizazi Kipya.

Mh. Hemed Suleiman alitahadharisha kwamba ipo misikiti yenye wafuasi wanaopendelea kushabikia vurugu na mifarakano ambayo hatimae baadhi ya Waumini huamua kuikimbia na kutafuta Misikiti iliyo salama.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaomba Waumini wa Dini ya Kiislamu wa Masjid Sultan pamoja na Misikiti mengine Nchini kuhakikisha kwamba Nyumba zao za Ibada wanazitumia katika miongozo stahiki ili iendelee kusaidia kutunza Amani na kuepuka cheche zinazoibua vurugu.

Aliupongeza Uongozi wa Taasisi ya Kiislamu ya Al Noor Charitable Agency na Wadau walioshirikiana kufanikisha ujenzi wa Msikiti huo ikiwa ni kitendo kinachoashiria uchamungu wao uliotukuka katika kumuamini Mwenyezi Mungu na siku ya Hesabu huku wakisimamisha sala na kutoa zaka.

Akizungumzia changamoto ya Kodi ya Vifaa na Bidhaa za Misaada zinazoingizwa Nchini ya Taasisi hiyo kwa ajili ya Misaada kwa Jamii Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema suala hilo linazungumzika kwa vile Serikali Kuu wakati wote hupendelea kuona kile inachokisamehe katika kodi lazima kiwafikie Walengwa ambao ni Wananchi.

Alisema wapo Wafanyabiashara wastaarabu na waungwana wanaokubali muda wote wa Biashara zao wamekuwa wakizingatia Sheria, Taratibu na hata Kanuni zinazowekwa na Serikali kupitia Taasisi zake.

Hata hivyo Mheshimiwa Hemed alibainisha kwamba Serikali Kuu imekuwa ikupunguza Kodi kwa baadhi ya Bidhaa wanazoingiza Wafanyabiashara Nchini lakini matokeo yake haziwafaidishi Wananchi kutokana na Wafanyabiashara hao wakorofi kuendelea kuuza bidhaa zao kwa bei ya juu.

“ Fedha ya Serikali inayokusanywa katika misingi ya kodi na mapato mengine hata kama itakuwa ni shilingi elfu Moja basi lazima iheshimiwe”. Alisisitiza Mheshimiwa Hemed.

Akisoma risala kwa niaba ya Uongozi wa Taasisi ya Al Noor Charitable Agency For Need Sheikh Mohamed Suleiman alisema Taasisi hiyo tayari imeshajenga Misikiti 26 ikiambatana na Madrasa katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba na kuleta Ukombozi katika upatikanaji wa huduma za Kijamii.

Sheikh Mohamed alisema Al Noor Charitable Agency For Need iliyoasissiwa mnamo Tarehe 5 Septemba Mwaka 2003 inatekeleza Kazi za uchimbaji wa Visima, kuhudumia Watoto Yatima pamoja na ugawaji wa misaada na zaka hasa wakati wa kipindi cha mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Alieleza kwamba Taasisi hiyo katika kuendelea kusaididana na Serikali Kuu tayari inasimamia Skuli ya Kiislamu, Redio ya Kijamii sambamba na kusafirisha Mahujaji wanakwenda Maka Nchini Saudi Arabia kwa ajili ya kutekeleza Ibada ya Hijja ikiwa ni nguzo ya Tano na ya mwisho ya Uislamu.

Akitoa taarifa ya Mradi wa Ujenzi wa Msikiti huo Mkurugenzi Mkuu wa Al Noor Charitable Agency For Need Sheikh Nadhir  Mahfoudh alisema Jengo hilo lililojengwa katika kipindi cha Miezi Tisa lina uwezo wa kusaliwa na Waumini wapatao Mia Tano kwa wakati Mmoja.

Sheikh Mahfoudh alisema mazingira ya Msikiti huo yameambatana na ujenzi wa Madarasa Manne yenye uwezo wa kuchukuwa Wanafunzi Mia Nne sehemu ya kuoshea Maiti, kupamba maiti pamoja na stoo ya hifadhi ya vifaa vya Majengo hayo.


 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.