Habari za Punde

Naibu Waziri Mhe.Ummy Akemea Vitendo Vya Udhalilishaji Kwa Watu Wenye Ulemavu.

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga akimchapa viboko mmoja wa vijana ambao wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya kudhalilisha watu wenye ulemavu kuombaomba mitaani.

Na: Mwandishi Wetu

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga amekemea vikali vitendo vya udhalilishaji Watu wenye Ulemavu ikiwemo suala watu ambao wamekuwa wakitumia kundi hilo kujinufaisha.

Hayo yameelezwa wakati alipofanya ziara ya kushitukiza katika maeneo mbalimbali ambayo wanahifadhiwa Watu Wenye Ulemavu katika Mtaa wa Tandale, Jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri alieleza kuwa kumekuwa na vitendo vya udhalilishaji wa watu wenye ulemavu ambavyo vimekuwa vikiendelea katika jamii na vitendo hivyo vinapelekea ukiukwaji kwa haki zao.

“Watu wenye Ulemavu wanahaki zao za msingi na ndio maana Serikali imekuwa ikuchukua hatua mbalimbali kuzuia vitendo vya udhalilishaji kwa kundi hilo na katika kulitambua hilo sheria mbalimbali zimekuwa zikitungwa lengo hasa ni kulinda maslahi na kuboresha maisha ya watu wenye ulemavu,” alisema Waziri Ummy

Alisema kuwa, wapo baadhi ya watu ambao ni kama mawakala “dealers” ambao wanawatoa watu wenye ulemavu katika mikoa mbalimbali na kuwaleta jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuwafanya ombaomba mitaani.

“Inastahajabisha kuona mtu anawachukua watu wenye ulemavu na kuwakodisha viti mwendo “wheelchair” ili wakaombe mtaani huku kila siku anachukua fedha hizo kwa wenye ulemavu lengo ikiwa ni kujinufaisha kwa maslahi binafsi,” alisema Ummy

Mheshimiwa Ummy alieleza kuwa upo umuhimu wa kufanya utambuzi mapema wa mapema wa watu wanaofanya vitendo hivyo kwa kundi hilo ili kuzuia vitendo hivyo kuendelea katika jamii.

“Serikali itahakikisha ina shughulikia suala hili la udhalilishaji wa watu wenye ulemavu ili waweze kupata haki zao, sambamba na kuwalindwa na kufanya kundi hilo liheshimike katika jamii,” alieleza Naibu Waziri Ummy

Aidha, Mheshimiwa Ummy amewataka wananchi kutowaonea aibu wahusika wanaofanya vitendo hivyo badala yake wawe huru kutoa taarifa katika vyombo vya kisheria ili wachukuliwe hatua.

Sambamba na hayo, Naibu Waziri alitumia fursa hiyo kuwaelimisha watu wenye ulemavu juu ya fursa ya mikopo inayotolewa na serikali kupitia halmashauri (2% Watu wenye Ulemavu) ili waweze kuanzisha shughuli zitakazo wapatia kipato badaya ya kuombaomba mitaani.

Kwa Upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Daniel Chongolo alikiri kupokea maelekezo yaliyotolewa na Naibu Waziri na alieleza kuwa tayari wameshachukua hatua kwa baadhi ya wahusika wanaojishughulisha na vitendo hivyo.

Naye, Bw. Steven Fotnatus alisema kuwa wapo tayari kuacha tabia ya kuombaomba mitaani maana wamegundua kuwa wamekuwa wakirubuniwa na baadhi ya watu ambao hawana nia njema nao.

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga (kulia) akizungumzia suala la udhalilishaji wa Watu wenye Ulemavu wakati wa ziara yake ya kushtukiza aliyoifanya katika maeneo mbalimbali ambayo wanahifadhiwa Watu Wenye Ulemavu Mtaa wa Tandale, Jijini Dar es Salaam. (wa tatu kutoka kushoto) ni Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Daniel Chongolo.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga akiangalia baadhi ya Viti Mwendo “Wheelchair” ambazo zimekuwa zikikodishwa kwa baadhi ya Watu wenye Ulemavu.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga akimsikiliza mtoto anayetambulika kwa jina la Neema (wenye ulemavu) (kushoto) wakati wa ziara yake ya kushtukiza aliyoifanya katika maeneo mbalimbali ambayo wanahifadhiwa Watu Wenye Ulemavu Mtaa wa Tandale, Jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga (wa nne kutoka kushoto) akizungumza na wakazi wa wanaishi karibu na Soko la Tandale wakati wa ziara yake ya kushitukiza katika maeneo mbalimbali ambayo wanahifadhiwa Watu Wenye Ulemavu Mtaa wa Tandale.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.