Habari za Punde

Wanaotumbuliwa ni Wale Wanaotumia Fedha za Umma Kwa Maslahi Yao Binafsi. - Dk. Mwinyi.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambae pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Wanachama wa CCM wa Tawi la Matale Pemba baada ya kulifungua leo 5-1-2021.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduziambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi aliwataka wananchi kuondoa shaka katika utaratibu wa kutumbua kwani wanaotumbuliwa ni wale wanaotumia fedha za umma kwa maslahi yao binafsi.

Rais Dk. Hussein Mwinyi aliyasema hayo leo mara baada ya kulifungua Tawi la Chama Cha  Mapinduzi (CCM) la Matale, lililopo Jimbo la Chonga, Mkoa wa Kusini Pemba.

Alisema kuwa kinachotakiwa ni fedha za umma kutumika kwa  mambo ya umma kwani kuna changamoto nyingi nchini zikiwemo maji, afya na nyenginezo kwa hivyo, wasiposhughulikiwa wabadhirifu na wezi  maendeleo hayatopatikana.

Rais Dk. Mwinyi alisisitiza kuwa kusudi lake ni kuweka nidhamu katika matumizi ya fedha za umma ili kuleta maendeleo na kuwapongeza wanaCCM na wananchi kwa mwitikio wao kwa kuunga mkono juhudi za maendeleo zinazochukuliwa hivi sasa.

Aliwapongeza wanaCCM kwa ushindi mkubwa wa kishindo uliopatikana katika uchaguzi mkuu uliopita, na kuwapongeza wanaCCM wa Matale kwa kujenga Tawi hilola kisasa na kueleza jinsi alivyofarajika na ujenzi huo.

Aidha, aliwapongeza wale wote waliochangia ujenzi wa Tawi hilo na kumpongeza Khamis Yussuf Matale kwa ufadhili wa ujenzi wa Tawi hilo pamoja na wanachama wengine wa CCM.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa uchaguzi umekwisha na sasa ni wakati wa kazi na ili kuleta maendeleo na mafanikio kunahitajika mambo matatu makubwa ambayo ni amani, umoja na uwajibikaji.

Alisema kuwa amani ni jambo muhimu katika nchi kwani nchi haiwezi kupata maendeleo iwapo haina amani na kuwapongeza wananchi na kuwataka kuendelea kuidumisha.

Aidha, alieleza kuwa umoja ni  muhimu na mifarakano haileti maendeleo na muda mwinyi hutumika kuleta malumbano hatua ambayo hivi sasa haipo na kilichotekelezwa hivi sasa ni kuwepo kwa umoja wa kitaifa.

Rais Dk. Mwinyi aliwaomba WanaCCM kuridhia kwa sababu umoja ndio utakaoleta maendeleo na kuwataka kuwaelimisha wale wote waliokuwa hawajawa tayari kuridhia umoja huo.

Jambo la tatu la kuleta maendeleo ambalo Rais Dk. Mwinyi alilieleza ni  uwajibikaji na kutaka kila mtu awajibike kwa pale alipo ambapo matumaini yake ni kwamba mafanikio makubwa yatapatikana.

Alisema kuwa hatua anazozichukua hivi sasa Za kuwajibisha watu lengo lake ni kuweka nidhamu ya kazi Serikalini kwani kila mtu akiwa na nidhamu akiiogopa fedha ya Serikali basi fedha hizo zitatumika kwa maendeleo ya Seerikali.

Rais Dk. Mwinyi aliwahakikihishia wanaCCM na wananchi wa Matale kwamba ombi lao la barabara kwa kiwango cha lami atalitekeleza, ujenzi wa kituo cha afya pamoja na kuahidi kuwapelekea vifaa walivyoomba vikiwemo seti moja ya Compyuta, viti 80 kwa ajili ya ukumbi, meza 4 kubwa kwa ajili ya ukumbi na vyarahani vitano vya mashine kwa ajili ya kikundi cha akina mama wa Tawi hilo.

Alisisitiza kwamba asilimia kubwa ya ushindi uliopatikana mwaka huu katika uchaguzi mkuu ulipita rekodi yake ni kubwa lakini kwa mambo ya maendeleo yanayokuja rekodi hiyo itavunjwa katika uchaguzi ujao.

Alieleza kufurahishwa kwake na wanaCCM hao kwa kuendelea kuwa imara na kueleza kuwa utaratibu huo wa ujenzi wa matawi ukiendelea uimara wa chama hicho utaimarika zaidi.

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu (CCM), alisema kuwaSerikali ya Awamu ya Nane imeanza kazi na inajipanga katika kuleta maendeleo kwa wananchi na kusisitiza kwamba viwanda vingi vinakuja na zile ajira zilizoahidiwa wakati wa kampeni zinakuja na kuwataka vijana wajipange kufanya kazi.

Nae Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Abdalla Juma Mabodi alisema alisema kuwa wanaCCM wataendelea kumuunga mkono Rais Dk. Mwinyi katika juhudi zake za kuiletea Zanzibar maendeleo endelevu.

Katika risala yao wanaCCM wa Tawi la Matale iliyosomwa na Katibu wa Tawi hilo Mohammed Ali Bakari ilieleza kuwa ujenzi wa Tawi hilo umeanza Agosti 8, 2020, ambapo mpaka kukamilika kwake umegharimu TZS Milioni 83,050,000 pamoja na thamani zake chini ya usimamizi wa Mhandisi Moh’d Hamad Shehe.

Aidha, wanachama hao wa Tawi la Matale walitoa pongezi zao kwa kijana mfanyabiashara wa Matale, Khamis Yussuf Hamad (Khamis Matale), kwa  kufadhili ujenzi wa jengo hilo kwa kushirikiana na wanaCCM wengine.

Risala hiyo ilieleza kuwa jengo lao la zamani la Tawi walilolijenga katika kijiji cha jirani eneo la Jitenge lilikuwa dogo na la udongo na paa lake la makuti halikukidhi haja kwa sasa kwani wakati huo walikuwa wanaCCM 60 tu.

Risala hiyo ilieleza kuwa baada ya muda viongozi wao waliamua kutafuta eneo lilolojengwa Tawi hilo jipya hivi sasa na kujenga Tawi kubwa linaloendana na wakati uliopo kwani malengo ya CCM ni kujenga majengo ya kisasa yenye hadhi ya chama hicho.

Alisema kuwa jengo hilo lina vymba 4, Ofisi ya Tawi, Ofisi ya Wadi, Ofisi za Jumuiya zote 3 za CCM, mlango wa duka ambao ni kitega uchumi cha Tawi ambapo pia, ujenzi umezingatia wenye mahitaji maalum kwa kuweka ramps.

Pia, walimshukuru Hamad Bakari Ali  kwa kuwezesha Tawi hilo kupata huduma ya umeme na vifaa vyake vyenye gharama ya TZS Milioni 1.5.

WanaCCM hao wa Tawi la Matale waliipongeza familia ya Marehemu Ali Bakari Ali kwa kuwapatia kiwanja ambacho wamejenga jengo hilo na kumuombea dua kwa msaada wake huo.

Walimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa uongozi na usimamizi wake mahiri ambao umetoa mwanga na matumaini makubwa kwa wananchi wa Zanzibar na kuwapongeza wale wote waliochangia ujenzi wa Tawi hilo.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.