Habari za Punde

Kongamano la Wanahabari wa Zanzibar Kufanyika Jumatatu

Na Miza Kona Maelezo Zanzibar          27/02/2021

Jumuiya ya Wanahabari Zanzibar inatarajia kufanya Kongamano la siku moja litakalofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakili Kikwajuni tarehe 01 Machi mwaka huu

Kongamano hilo litazungumzia changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya habari nchini lenye lengo la kuhamasisha matumizi ya mawasiliano, kuimarisha mahusiano mazuri katika sekta hiyo na kujenga Zanzibar mpya.

Akizungumza na waandishi wa habari huko katika ukumbi wa Sanaa Rahaleo, Mwenyekiti wa Kamati ya Jumiya hiyo Farouk Karim amesema Mgeni rasmi katika kongamano hilo anatarajiwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi.

Amesema kuna changamoto nyingi katika sheria ya habari hivyo kongamano hilo litaelezea mapungufu yaliyomo ili kuweza kufanyiwa marekebisho na kwenda sambamba na matumizi ya mawasiliano ya habari nchini.

Amefahamisha kuwa sheria hiyo imeshapitwa na wakati imekuwa ikiwabana na  kuwakandamiza waandishi  wa habari kwa kutopata fursa mbalimbali za kijiendeleza hivyo ipo haja ya kufanyiwa marekebisho ya sheria hiyo ili wanahabari wapate nafasi zaidi.  

Aidha Mwenyekiti huyo ameeleza kuwa kongamano hilo litafungua ukurasa mpya kwa wanahabari na viongozi mbalimbali kushirikiana na vyombo vya habari katika kupata mawasiliano mazuri na kujenga uchumi wa nchi.

Kongamano hilo pia litawafanya kuwa kitu kimoja, kuwa wazalendo na kujenga upendo katika fani yao na kuleta maendeleo zaidi nchini.

“Lengo la kongamano hili wanahabari tunataka kuwa kitu kimoja, kuwa wamoja, wazalendo na kujenga upendo katika kuijenga nchi  

Nae Katibu wa Kamati ya Wanahabari Zanzibar Bi Imane Duwe amesema kuwa waandishi wanachangamoto nyingi katika uimarishaji sekta yao na hawajapata nafasi ya kuwasilisha kero zao, hivyo kongamano hilo litasaidia kufungua milango ya kuondosha matatizo yanayokabili sekta ya habari nchini

Katika kongamano hilo mada mbili zitawasilishwa na kuchangiwa mada zenyewe ni Changamoto ya Wanahabari na Maudhui ya Mitandao ya Kijamii katika kusaisdia sekta ya Habari.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.